Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi wangu, mpenzi wangu,
Mbona uko mbali nami? Nakuhitaji sana mpenzi, nakuwazia sana, sina
raha tukiwa mbalimbali hivi. Napenda kujua kama u mzima kila wakati na
kusikia sauti yako nzito ikinijali kama unavyonijali kila siku.
Nakumiss mpenzi wangu ... mpaka namwaga hata ung’eng’e kwa ajili yako.
Pili, mwandani wangu wa maisha, naomba unisaidie kitu kimoja. Si
kuna yule binamu yangu anasoma shule moja ya ukata huko. Na ili asome
amelazimika kupanga karibu na shule. Sasa baada ya kumsikiliza mgeni
wa bosi wiki hii, nashindwa hata kulala, na nikilala naamka natoa jasho
kutokana na jinamizi zinavyonizonga.
Kisa chenyewe ni hicho. Wakati bosi anabugia supu yake asubuhi
asubuhi kabla ya kujipeleka kazini, tukasikia hodi. Kumbe ni mama
mmoja anayetoka jimboni kwa bosi. Baada ya kumwamkia bosi kwa heshima
anazostahili mheshimiwa, bosi akamwambia ajieleze haraka maana anaenda
kwenye mikutano. Basi mama akaanza.
‘Samahani kukusumbua mheshimiwa lakini nimeshindwa kuvumilia.
Tumesisitiziwa umuhimu wa elimu hadi tunafanyiwa msako wa nyumba hadi
nyumba kama vile sisi ni wahalifu.’
‘Ndiyo. Lazima mpeleke watoto wenyewe shuleni. Mtukufu Rais amesema’
‘Sijabisha. Lakini kwa nini tunatakiwa kupeleka watoto wetu shuleni?’
Bosi akajibu kwa dharau.
‘We mama usipoteze muda wangu. Wanaenda shule ili wapate elimu.’
‘Ahaa. Sawa kabisa. Na kama shule haitoi elimu?’
‘Una maana gani? Kama shule si shule, elimu itapatikana wapi? Kwa nini nimpeleke mwanangu mdomoni mwa mamba?’
‘Mbona sikuelewi.’
‘Unajua mwanangu ametongozwa na walimu wangapi? Walimu wenyewe wote ni vodafasta ...’
‘We! Acha kutumia lugha ya namna hii. Hata mtukufu Rais ...’
‘Amekataza lakini ndio ukweli wenyewe. Bila shaka wako wanaojua
kufundisha lakini katika shule ya mwanangu hakuna. Na ufasta wao ni
katika kutongoza tu.’
‘Basi ni rahisi sana. Ni kiasi cha kuwashtaki kwa mwalimu mkuu.’
‘Usinichekeshe mheshimiwa. Yeye ndiye kiongozi, na kwa mujibu wa mwanangu wanajua wanafunzi watatu ambao anatembea nao.’
Lo, mpenzi, hapo bosi akabaki kimya kidogo. Kumbe mama ndio kwanza anaanza.
‘Lakini si hivyo tu, mheshimiwa. Naomba nikupe tu kwa muhtasari
nilivyoambiwa na wanafunzi wenyewe nilipoamua kufuatilia nilivyoambiwa
na mwanangu. Kwanza wanafunzi wengi wanalazimika kupanga katika nyumba
za watu binafsi hali ambayo ni hatari sana. Makazi wanayopanga
wanafunzi hawa si salama, si bora, si sanifu na wala hayatoi mwanya
muafaka kwa wanafunzi kujiendeleza. Mzazi anapompangishia mtoto chumba,
kutokana na maisha kuwa magumu anashindwa kumtimizia kila kitu na hivyo
ananunua unga, dagaa, mafuta ya taa basi.
Wanafunzi wengi wanalala chini, kwa kutandika mifuko ya ‘salfet’ ama
gunia. Shida kubwa inakuja siku za mvua ambapo wakati mwingine nyumba
huvuja na maji kuwaingilia, ama maji ya mvua kupenya na kuingia ndani,
na kuna kipindi cha sisimizi na wadudu. Nilipoongea nao, wanafunzi
walilalamikia sana suala la sisimizi kuwaingilia.
Walisema pia kwamba chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa mahindi na
dagaa, na wengi wao wanapewa kiasi cha kumaliza mwezi mmoja ama wakati
mwingine hakitoshelezi. Inapotokea mahitaji haya yamekwisha kabla ya
kuletewa basi inabidi mwanafunzi aishi maisha ya kudandia kwa marafiki
wenye chakula japo si wakati wote, ni rahisi maana kila mtu ana hali
ngumu na anajitahidi kufikisha mwisho wa mwezi.
Upande wa kusoma jioni, hakuna umeme, hivyo wanafunzi wanatumia
zaidi kibatari cha mafuta ya taa ili mradi mafuta yawepo. Sasa kweli
wanasoma kwa misingi hiyo mheshimiwa?’
‘Mbona haya mambo ni ya kawaida, mama. Hata sisi tulisoma kwa shida. Kinachohitajika ni ari ya kusoma, watafanikiwa tu.’
‘Bila mwalimu? Hao wanafunzi wako Kidato cha Nne lakini hawajawahi
kuwa na mwalimu wa Kiingereza hata siku moja. Na hata upande wa walimu
wengine, taaluma yao ni haba kiasi kwamba wanawazidi wanafunzi kidogo
sana.’
‘Wajisomee basi. Kazi yenu kungoja serikali ikufanyie kila kitu.’
‘Sawa mheshimiwa. Nakuomba siku moja uje uone kama kweli utasoma
katika shule kama hizo. Au bora zaidi, mtume watoto wenu kusoma katika
shule hizo za ukata.’
Bosi akaanza kukasirika.
‘Yaani unataka kubadilisha hata jina. Serikali inahangaika weeee
kuwaandalia watoto nafasi ya kusoma sekondari katika kila kata waziita
shule za ukata?’
Lakini yule mama hakutaka kurudi nyuma.
‘Kama si za ukata, basi leteni watoto wenu. Mtaambiwa ukweli.
Mimi mwenyewe nilishtuka sana kuwasikiliza hawa wasichana. Ndiyo
maana nimekuja. Kwa sababu kama hali ndiyo hiyo, nakuambia bora
nifungwe kuliko kumpeleka mwanangu katika shule kama hizo.’
‘Wewe umetumwa nini?’
‘Ndiyo nimetumwa. Nimetumwa na wazazi wenzangu ambao wanaumia,
wanalia kila siku bila kusikilizwa. Ngoja nikupe sehemu ya mwisho ya
mazungumzo yangu na wasichana wale. Nilipowauliza wanafanyaje kuhusu
gharama zao zingine walinijibu hivyo’
‘Mama, ukweli ni kwamba hakuna uwezo wa kupata mahitaji yetu.
Ukitaka mafuta ya kupaka mwili, unatenga ya kula na kupaka, hakuna
mafuta maalumu kwa ajili ya mwili. Nguo za ndani ndo hizo hizo za labda
kama una bwana mwenye vihela kidogo ...’
Hapo nilishtuka sana mheshimiwa. Yaani tunawapeleka watoto wetu
kwenye uwanja wa UKIMWI moja kwa moja. Lakini nilijikaza na kuzidi
kuwauliza kuhusu masuala ya Bwana. Majibu yao yakanikatisha tamaa.
‘Mama kwa nini tukufiche maana inatuumiza na sisi. Inabidi uwe na
wanaume angalau watatu, kila mmoja akikupa shilingi elfu moja kwa wiki
uongo, unaweza kununua angalau sabuni au kumaliza kodi ya pango.’
Nikawauliza kama hawa wanaume ndio walimu tu maana niliona walimu ni wanne tu. Walicheka tu.
‘Mwalimu ndiye bora ndiyo maana mnaweza kujikuta mko zaidi ya wanne
na mnajuana na hakuna kitu mtafanyana bali kuvumilia kila mtu ale kwa
wakati wake. Maana anayetembea na mwalimu huyo ni tajiri maana mwalimu
anatoa dau kubwa kama elfu tano kwa mwezi na hapa kati akikupa shilingi
mia tano si haba. Wanafunzi wanaotembea na walimu wanajiona sana na
huwezi kuwafanya chochote. Na ukithubutu kusema shule utaihama mwenyewe
maana utakuwa unakula bakora kila kukicha, na usiombe mwalimu akuite
ofisini maana utatandikwa kama ng’ombe. Na hapo ukute alishakutongoza
ukamkataa, utajuta kuzaliwa. Sasa mama utafanya nini? Na ukimkosa
mwalimu, basi utatafuta hawa wa bei ndogo mitaani.’
Mimi mpenzi wakati nasikiliza maelezo yote hayo, nilikuwa namkumbuka
binamu yangu. Yuko salama kweli? Au yeye naye analazimika kuishi
maisha kama hayo. Mwishoni nilishindwa kujizuia, nikaangua kilio.
‘Maskini binamu yangu ...’
Bosi akashtuka.
‘We Hidaya unasema nini?’
Ikabidi nivunge kidogo maana mimi sitakiwi kukaa na kusikiliza mazungumzo na wageni.’
‘Samahani baba, nilipata habari asubuhi kwamba binamu yangu anaumwa sana. Nikamkumbuka tu.’
‘Basi toka hapa. Unatusumbua.’
Kwa hiyo mpenzi ilibidi nitoke lakini wakati natoka nikamsikia yule
mama akisema kwaamba baada ya kusikia yote hayo, yeye na wenzake
wamewatoa watoto wao shule moja kwa moja na kama anataka awaletee
polisi kuwakamata maana hawawezi kuwaacha watoto katika mazingira
hatarishi kama hayo.’
Na kweli. Katika hali kama hiyo kuna faida gani kuwa na shule?
Kama serikali haina uwezo wa kuhakikisha kwamba shule zake zinajenga
badala ya kubomoa kwa nini watudanganye kwamba watoto wanapata elimu
huku wakipata mimba au UKIMWI badala yake? Nakuomba sana mpenzi wangu
uende ukamwone binamu maana sasa roho haitulii.
Akupendaye hata uwe mbali namna gani
source raia Mwema: Hidaya
No comments:
Post a Comment