Neno La Leo; Na Tuyaishi Maisha Ya Kadiri...
Ndugu zangu,
DUNIANI hakuna miujiza katika
kuyafikia mafanikio. Hakuna njia za mkato pia. Ni sharti tufanye kazi
kwa bidii. Tusiwe ni watu wenye kutanguliza taamaa na hata kuwadhulumu
wengine. Tuyaishi maisha ya kadiri. Ni kwa kuyafanya yale yaliyo ndani
ya uwezo wetu. Si kuishi kwa kufikiri wengine wanavyotaka uishi.
Maana, ni wachache duniani walioweza
kufanya miujiza kama tunayoambiwa kwenye vitabu vya dini; Bwana Yesu yu
miongoni mwa wachache hao. Tunasoma, kuwa Mafalisayo walimshangaa Yesu
na mafanikio yake. Wakatamka; “ Hivi ni Yesu huyu huyu mwana wa Joseph
fundi Seremala!”
Naam, mwanadamu usitazame tu
alipofikia sasa mwanadamu mwenzako kwenye safari yake. Jitahidi
uangalie mwanzo wa safari yake. Alikotokea. Ndipo hapo utayapata ya
kujifunza.
Papa Francis wa Kanisa Katoliki
amefikia kiwango cha juu cha mafanikio kwenye ngazi ya kanisa. Ni rahisi
kumwangalia hapo alipo, lakini ni muhimu kuiangalia safari yake
ilipoanzia.
Tunasoma leo, kuwa Papa Francis ni
mtu wa kadiri. Muda wote wa uhai wake amejitahidi kuishi maisha ya
kadiri. Papa si mtu wa makuu. Na kule Vatican wanashangazwa hata na
mavazi yake yasio gharama kubwa, ikiwamo viatu pia.
Hapa kwetu Tanzania Julius Nyerere ni
mfano wa viongozi walioishi maisha ya kadiri. Mwalimu aliishi kama
alivyohubiri. Ni mfano wa kuigwa.
Ni Neno La Leo
Maggid Mjengwa,
Iringa
No comments:
Post a Comment