Msiba mzito umetufika leo, wasomaji wa fasihi na walimwengu kwa ujumla. Chinua Achebe amefariki, akiwa na umri wa miaka 82.
Maarufu kama muasisi wa fasihi ya ki-Ingereza katika Afrika, Chinua Achebe ametoa mchango mkubwa katika uandishi, mchango ambao uliiweka Afrika mahala pazuri katika ramani ya fasihi ya dunia.
Tangu alipochapisha riwaya yake maarufu, Things Fall Apart, hadi kufariki kwake, Achebe ameandika riwaya, hadithi fupi, na insha kuhusu fasihi, uandishi, siasa na utamaduni. Amefanya mahojiano mengi, ambayo, kwa bahati nzuri yanapatikana mtandaoni au katika vitabu na majarida.
Achebe aliamini kwa dhati kuwa jukumu la msanii ni kuwa mwalimu wa jamii. Yeye mwenyewe amezingati wajibu huo tangu ujana wake, alipochapisha Things Fall Apart, hadi kurariki kwake. Amewafundisha waAfrika mengi kuhusu jamii yao, udhaifu na uwezo wao, na amewafundisha walimwengu kuwaona waAfrika kwa mtazamo tofauti na ule wa wakoloni. Amewafundisha walimwengu maana ya ubinadamu, ambayo inavuka mipaka ya kabila, taifa, dini, jinsia au nchi.
Sikupata fursa ya kukutana uso kwa uso na Chinua Achebe, bali nimesoma na kufundisha maandishi yake mara kwa mara. Nashukuru pia kuwa nilipata wazo la kuandika mwongozo wa Things Fall Apart. Kwa namna hiyo ya kusoma na kutafakari maandishi yake, najiona kama vile nami nimekutana na mwandishi huyu. Nimalizie tu kwa kusema kwamba kwa mchango wake mkubwa kwa walimwengu, Achebe atakumbukwa daima.
Source Hapa Kwetu
No comments:
Post a Comment