NIMEPATA kuyaandika
haya, kuwa tunawapitisha watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye
matope. Kwa nini?
Kwenye
moja ya mashairi ya Marcelino Dos Santos wa Msumbiji anasema; "We Must
Plant". Kwa maana ya tuna lazima ya kupanda. Dos Santos hazungumzii
kupanda mbegu za mahindi au mtama, bali kupanda fikra za kimapinduzi kwa
wanajamii. Fikra zitakazowasaidia kutoka katika hali iliyopo na kwenda kwenye
hali nyingine iliyo bora zaidi.
Uvumi
wa Freemasons unaosambaa sasa kwenye jamii ni dhana ya kufikirika kama
ilivyokuwa kwa Babu wa Loliondo. Ya Babu wa Loliondo yalianza kwa uvumi
wa magazetini na hatimaye kugeuka kuwa moja ya majanga ya kitaifa.
Leo
Watanzania tunajua, kuwa pamoja na kutangazwa sana, Babu wa Loliondo
hajamtibu hata mgonjwa mmoja. Badala yake, amechangia kwenye vifo na mateso ya
wengi. Hakika, ni sisi Watanzania ndio tuliokuwa ' wagonjwa' wa
kuendekeza abracadabra za Babu wa Loliondo.
Na
uvumi huu wa sasa wa Freemasons ni abrakadabra nyingine
tunayolishwa Watanzania. Ni habari za kupotosha jamii, ikiwamo jamii
kuaminishwa kuwa wanachama wa jumuiya ya Freemasons ni watu matajiri na kuwa
anayejiunga na Freemasons atapata utajiri wa haraka.
Kwamba
Freemasons inahusishwa pia na nguvu za giza ikiwamo imani za kimashetani.
Walioanzisha upotoshaji huu wanajua kuwa hiyo Freemasons ni jumuiya ya
kimataifa kama ilivyo kwa Rottery na Lions Club ambazo uanachama wake haupo
wazi kwa yeyote yule bila kupitia wanachama wenyewe. Lakini haimaanishi kuwa
wanachama wa jumuiya hizo wanajipatia utajiri wa haraka kwa kushiriki
‘abrakadabra’ .
Leo
hii hapa Tanzania kuna vijana wanaoshinda vijiweni wakiwaza tu namna ya
kujiunga na Freemasons badala ya kufanya kazi. Na Freemasons pia imekuwa njia
ya baadhi ya wanajamii kutetea uvivu wao. Freemasons inatumika pia
kuwaandama wenye kufanya kazi kwa bidii na kujipatia mafanikio. Maana, leo hata
anayenunua pikipiki mpya ataitwa ‘ Freemason!’
Ni
wakati sasa kwa serikali kutoa tamko juu ya hili la uvumi wa Freemasons. Iweke
wazi kuwa jambo hili linakuzwa na kuwa kuna upotoshaji unaofanywa kwa makusudi.
Maana, uvumi huu ukiachwa uendelee unaweza kutuletea madhara makubwa huko
tuendako.
Tunajua,
kuwa leo wamejitokeza matapeli wanaowahadaa wanajamii kuwa wao ni Freemasons na
kuwa wanaweza kuwasaidia wengine kujiunga na mtandao huo. Wamejitokeza pia
waganga wa kienyeji wenye kufanya utapeli kwa kutangaza kuwa wana uwezo wa ‘
kiganga’ wa kuwasaidia wateja wao kujiunga na Freemasons. Wapo wanajamii
wanaopoteza fedha na mali zao kwa kutapeliwa juu ya hili la Freemasons. Ndiyo
maana, kuwa ni wajibu wa serikali kuingilia kati kuwanusuru watu wake.
Ndiyo,
watu wetu wako kwenye giza. Kuna upumbavu unaendelea kwenye jamii. Ni wajibu wa
serikali yao kuwasaidia kwa kuwamulikia mwanga. Na kuna tofauti ya ujinga na
upumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka; “Kusoma si kuufuta ujinga, bali
ni kuupunguza”.
Kila
mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si
kosa, hata profesa anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za kuchomea mhindi
mbichi. Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda
profesa.
Lakini
upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na
uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndiyo maana
binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga
wake. Kuwa na ujinga wa jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani
anayeelewa kila jambo?
Na
mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza
kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemuuliza swali hilo. Naye akanijibu;
” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri.
Nilidhani angetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea
majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.
Wanadamu
tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndiko njia mojawapo ya
kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu
mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya
kuendekeza abrakadabra za Freemasons ni kielelezo cha
Watanzania, kama ilivyokuwa kwa Babu wa Loliondo, kuamua kuacha kufikiri.
Ndiyo, kuna waliojifunika vilemba vya ujinga. Wako gizani, wanahitaji
mwanga. Nahitimisha.
source:
Raia mwema: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment