Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa safari ya CCM kuingia Ikulu 2015 imefika mwisho.
Hayo yalielezwa na wabunge wa Kanda ya
Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara katika mkutano
uliofanyika mjini Maswa ambako ndiko yaliyoko makao makuu ya kanda
hiyo.
Wabunge hao waliokuwa wameongozana na
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Taifa la chama hicho, Shilugushela
Nyangaki, walieleza kuwa pamoja na chama hicho kuwa madarakani kwa miaka
51 bado wananchi wa Tanzania ni masikini wa kutupwa kutokana na sera
za CCM.
Katika mkutano huo wabunge hao, Rahel
Mashishanga (Viti Maalum), jimbo la Shinyanga, Silvester Kasulumbayi,
mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Meshack Opolukwa mbunge wa jimbo la
Meatu na mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi John Shibuda, walisema
serikali ya CCM imewatelekeza wananchi wake katika sekta za elimu, afya,
maji miundombinu na hata chakula.
Wakizungumzia elimu hususani matokeo ya
kidato cha nne, Mashishanga na Opolukwa walisema kuwa mitaala ya elimu
kuanzia shule za msingi hadi sekondari ni mibovu na hata kufanya vibaya
kwa wanafunzi wengi wa kidato cha nne mwaka 2012 ni kutokana na mgomo
baridi wa walimu kuanzia shule za awali hadi vyuoni.
Walisema kuwa kuwapo kwa hali hiyo sasa
Tanzania itarajie kuwa na taifa mbumbumbu kutokana na mfumo mbaya wa
elimu na kushauri kuwa serikali iwajali walimu kwani wamekuwa wakifanya
kazi katika mazingira magumu.
Kuhusu afya, wabunge hao walisema kuwa
wananchi wamekuwa wakihaha kupata madawa na kuwapo kwa migomo baridi kwa
madaktari na wauguzi hasa maeneo ya vijijini.
Opolukwa alisema kuwa serikali ya CCM
imekuwa ikifanya mzaha na elimu kwani watoto wanaofaulu ni wasiojua
kusoma na kuandika huku waziri mwenye dhamana akikataa kuwajibika kwa
kujiuzulu .
Wakizungumzia kutelekezwa kwa wakulima wa
zao la pamba, Opolukwa alisema wakulima wameshindwa kunufaika na kilimo
cha zao hilo hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakinunua mbegu ya pamba
kwa Sh. 1,200 kwa kilo na kuuza kilo moja kwa Sh. 660 jambo ambalo
halimsaidia mkulima kumwondolea umasikini.
Naye Shibuda alisema kuwa serikali ya CCM
imekuwa ikikopa fedha nyingi badala ya kuzitumia kuwasaidia wakulima
imekuwa inatumia mabilioni kwa anasa na safari lukuki za viongozi nje
wakiambatana na msafara mkubwa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment