Ndugu zangu,
Kuna simulizi ya kwenye Biblia. Enzi za Mfalme Suleiman kuna watu waliolalamika sana, kuwa wanaishi kwenye manyanyasiko mno.
Kukawa na vijana waliokuwa na kiu ya kutaka mabadiliko ya uongozi wa mfalme. Walitaka watawaliwe na mfalme kijana.
Wazee walipoombwa ushauri wakatamka; kuwa vijana mara nyingi hupungukiwa na busara. Hivyo, si lazima mfalme awe kijana.
Vijana wale wakakaidi ushauri wa
wazee. Wakampata Mfalme kijana. Naye alipokuwa madarakani, alitenda mara
mbili ya dhambi alizotenda mtawala aliyetangulia.
Mfano, kama mtawala aliyepita alitoa
adhabu ya kuchapa kwa mjeledi, basi, mfalme kijana yeye alitaka atumie
rungu. Hakukuwa na nafuu walioitarajia.
Ndugu zangu,
Juma la kwanza tu baada ya Bunge
kuanza mwaka 2010, nikiwa njiani kutoka Singida nilisimama Dodoma. Hapo
nilipata bahati ya kukutana na mmoja wa Wabunge vijana kutoka kambi ya
upinzani.
Tulikaa na kunywa chai pamoja.
Alinitaka pia ushauri katika kazi yake. Hakika,niliingiwa na matumaini
makubwa juu ya fikra zake za kimaendeleo pale alipoanza mazungumzo.
Mathalan, kati ya dhambi kadhaa zinazofanywa na wabunge alizoziona,
akaniambia juu ya kustaajabishwa kwake na tabia ya Wabunge kufoji risiti
za safari zao ili wapate fedha zaidi.
“ Yaani kaka Maggid, sikujua kuwa
Wabunge hawa wanafanya mambo kama watoto wa shule. Yaani Mbunge
anahangaika kufoji risiti za mafuta na kudai kuwa ametokea mahali fulani
kuja hapa Dodoma wakati sio!” Aliniambia kwa uchungu mbunge yule
kijana.
Lakini, mashaka yakanijia pale nilipomwuliza;
“ Sasa ukitoka hapa Dodoma umejiandaa
na kipi cha kwenda kuwaambia wapiga kura wako kwenye mkutano wako wa
kwanza wa hadhara baada ya kikao chako cha kwanza Bungeni?”
Mbunge yule kijana aliniangalia na kuniambia; “ Naenda kwanza Dar kuhangaikia gari yangu mpya!”
Nikawa nimekatishwa tamaa na Mbunge
yule kijana. Kwamba katika juma la kwanza tu la kukaa Bungeni, tayari
ameanza kufikiria kuhangaikia masuala yake binafsi, na si masuala ya
wananchi waliompigia kura!
Naambiwa, naye siku hizi anapomaliza vikao vya kuongea hata na jamaa zake tu, haraka sana hukimbilia kutoa ‘ bahasha za nauli’.
Siku hizi mbunge yule kijana ana gari zaidi ya ile aliyokwenda kuichukua Dar. Amekuwa mbunge-mfanyabiashara.
Sifikirii tena kwenda kumpa ushauri
mbunge yule kijana, maana, naweza kuambulia kudhalilishwa kwa kupewa
‘bahasha ya nauli’ ya kurudia nyumbani kwangu.
Naam, ni heri ya ndugu yangu John
Komba, hata akisemwa kuwa anasinzia Bungeni, bado ana mchango kwa jamii;
kwa nyimbo zake zenye kuburudisha na kuelimisha.
Ndio, nchi hii inahitaji mabadiliko ya
kimsingi, lakini, ni vizuri kutambua, kuwa wengine tunaofikiri kuwa
wanaweza kutusaidia katika kuyafikia mabadiliko hayo, hawana tofauti
kabisa na baadhi ya tunaofikiria hawatufai.
Na hutokea, kuwa dhambi wafanyayo, na
watakayoifanya, yumkini yaweza kuwa ni mara mbili ya inayofanywa na
baadhi ya waliopo sasa.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
No comments:
Post a Comment