Na Fidelis Butahe, Mwananchi, Dar es Salaam
Dar es Salaam. Ikulu imetoa kauli inayopingana na ile ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu hatima ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Itifaki cha wizara hiyo Anthony Itatiro, ambaye anatuhumiwa pamoja na maofisa wengine wa wizara hiyo kupanga njama ya kuchota Sh3 bilioni baada ya kubuni safari feki ya Rais.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti hili jana kuwa Serikali imeshachukua hatua za kinidhamu dhidi ya Itatiro kwa kumvua hadhi ya ubalozi na kutenguliwa na nafasi yake ya ukurugenzi wa Itifaki.
Hata hivyo, kauli ya Sefue ambaye ndiye Mkuu wa Utumishi serikalini, inapingana na ile iliyotolewa juzi na Naibu Waziri katika wizara hiyo, Juma Mahadhi ambaye alikaririwa akisema kwamba Itatiro bado yuko kazini na kwamba suala lake lilikuwa likisubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete.
Mahadhi alitoa kauli hiyo alipobanwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa, ambaye pia ni
Mbunge wa Monduli aliyehoji hatima ya tuhuma hizo wakati wa kikao cha
kamati hiyo.
Hata hivyo, jana Sefue akizungumza na Mwananchi alisema: “Uteuzi wake umetenguliwa baada ya kutokea hilo tatizo, hatua ya kinidhamu tuliyomchukulia ni kumwondoa katika nafasi hiyo pia hata ule wadhifa wake wa ubalozi pia tumemwondolea.”
Sefue alisema nafasi ya Mkuu wa Itifaki iliyokuwa
ikishikiliwa na Itatiro hivi sasa anakaimu mtu aliyemtaja kuwa ni Andi
Mwandemba na kwamba hatua hizo zimechukuliwa mwaka huu, lakini akasema
hakumbuki tarehe.
Alipoulizwa hatua zaidi ambazo atachukuliwa kigogo huyo alijibu; “Itatiro atatafutiwa kazi nyingine ambayo ni ya chini zaidi kuliko aliyokuwa nayo awali, yaani cheo cha chini kuliko alichokuwa nacho.”
Sefue alieleza kuwa utaratibu uko wazi kwamba
linapogundulika jambo ambalo siyo la kawaida hatua za kinidhamu ni
lazima zichukuliwe.
“Inapogundulika kuwa mambo hayaendi vizuri hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe ili iwe funzo kwa wengine,” aliongeza Sefue, ambaye ni Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
Alipoulizwa kama ni hatua stahili kwa kumvua
wadhifa mtu anayehusishwa katika njama za kutaka kuchota kiasi cha Sh3
bilioni, alijibu kuwa hiyo ni hatua ya kinidhamu na pia ni fundisho kwa
wengine.
Kauli ya Mahadhi
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alimhoji Mahadhi kuhusu jaribio la wizi lililofanywa na maofisa wa wizara yake baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam juzi.
Mahadhi alisema wizara ilichukuahatua dhidi ya maofisa wa ngazi za chini wakati suala la Itatiro lilikuwa mikononi mwa Rais Kikwete kutokana na wadhifa wake.
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alimhoji Mahadhi kuhusu jaribio la wizi lililofanywa na maofisa wa wizara yake baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam juzi.
Mahadhi alisema wizara ilichukuahatua dhidi ya maofisa wa ngazi za chini wakati suala la Itatiro lilikuwa mikononi mwa Rais Kikwete kutokana na wadhifa wake.
Naibu waziri huyo alidai walichukua hatua hiyo
kufuatia ushauri waliopewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na Mkaguzi wa Ndani walioendesha uchunguzi wa njama hiyo.
“Takukuru na mkaguzi waliona hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa hao na ndiyo wakashauri wachukuliwe hatua kali za
kinidhamu,” alisema Mahadhi.
Itatiro na maofisa wanne wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walituhumiwa mwaka jana kupanga
njama za kuchota kiasi hicho cha fedha bila ya kuwapo kwa ziara ya Rais
kwenda nchi yoyote ya kigeni.
Mpango huo unadaiwa kusukwa Juni mwaka jana kwa maofisa hao kwa kuitaka Wizara ya Fedha kutoa kiasi hicho cha fedha.
source: Mwananchi
HIYO HATUA MLIO CHUKUA HAITOSHI KABISA, INATAKIWA WAFIKISHWE MAHAKAMANI ILI IWE FUNDISHO KWA WENGINE, HACHENI KUONEANA HURUMA HILO NI KOSA KISHERIA WAFIKISHWE MAHAKAMANI HARAKA SANA. TUFANYE KAMA WACHINA.
ReplyDelete