Kamishsina wa Polisi Musa Ali Musa
akitoa ufafanuzi
Na Patricia
Kimelemeta
UJIO wa Askari wa Shirika la Upelelezi
la Marekani (FBI) nchini na kuanza kufanya kazi, umewezesha kuanza kunaswa kwa
baadhi ya watu, wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Padre Evarist Mushi (55) wa
Kanisa Katoliki Unguja, visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
Mwananchi Jumamosi Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa
Ali Musa alithibitisha kwamba jeshi lake limekuwa likishirikiana na FBI katika
upelelezi huo na kwamba idadi ya waliokamatwa imeongezeka.
“Ni kweli tumekuwa tukishirikiana na
FBI katika upelelezi ili kuhakikisha kuwa, wahusika wa tukio la kuuawa kwa
Padri Mushi wanakamatwa. Hii itasaidia kupunguza vitendo vinavyohusishwa na
matukio ya kigaidi yakiwamo mauaji,”alisema Kamishna Musa.
Alisema kuwa hilo linafanyika ili
kuhakikisha kuwa, zoezi la kuwakamata wahusika wa uhalifu huo linafanikiwa kwa
kiasi kikubwa, jambo alilosema linaweza kupunguza matukio ya mauaji.
Alibainisha kwamba hadi sasa kuna
ongezeko la idadi ya watu waliokamatwa na kwamba watu hao wanaendelea kuhojiwa,
huku wengine wakishikiliwa kwa sababu maalumu.
Kamishna Musa alifafanua kuwa
kutokana na zoezi hilo watu watakaobainika kuhusika na mauaji hayo watafikishwa
kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua zaidi.
Padri Evaristus Mushi aliuawa Februari
17, mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa katika
pikipiki aina ya Vespa, wakati akienda kuongoza misa katika Kanisa la Mtakatifu
Theresia la Beit el Rass.
Juzi, Kamishna Musa aliliambia Gazeti
hili kwa njia ya simu kwamba wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar kufanya
uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi.
Alisema kuwa wapelelezi hao tayari
wameanza kazi hiyo kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri
huyo aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” alisema Kamishna Mussa bila ya
kutaja wanatoka nchi gani.
Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni
lini wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni
siri za polisi na kwamba zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya
Serikali, vililithibitishia Mwananchi kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka
wauaji wa Padri Mushi.
Kutua
kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya
Kikwete katika salamu zake za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi, kuwa
amewaagiza polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo
vingine vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika
kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Awali,
akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa Rais Kikwete ameidhinisha Serikali
kugharamia wapelelezi kutoka nje, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi alihusisha tukio hilo na vitendo vya ugaidi.
Ujio
huo wa FBI pia unaweza kuhusishwa moja kwa moja na dhamira iliyoonyeshwa mapema
na Serikali ya Marekani kuwa ipo tayari kusaidia upelelezi wa mauaji hayo.
Dhamira
hiyo ilibainishwa katika salamu za rambirambi za kifo hicho zilizotolewa na
Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Vyanzo
mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza kuwa kabla ya kuanza kwa
operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya mazungumzo na Waziri Nchimbi na
viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya kuangalia namna watakavyofanya
shughuli hiyo.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment