TULIAHIDI
kwamba wiki hii tutaangalia athari za urais wa Uhuru Kenyatta. Kwa
kutangazwa Rais mteule wa Kenya Uhuru na Naibu wake, William Ruto
wamefaulu hadi sasa kukikiuka kiunzi kimoja. Kuna vizingiti vingine
viwili vinavyowakabili ambavyo lazima wavidakie. Vyote ni vya
kisheria.
Cha kwanza ni kesi mbili zinazofikishwa Jumatano hii mbele ya
Mahakama ya Juu ya Kenya (Supreme Court) zenye kuitaka Tume Huru ya
Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iyabatilishe matokeo iliyoyatoa usiku wa
kuamkia Jumamosi na yaliyoonyesha kwamba walioshinda uchaguzi wa urais
ni Uhuru na Ruto.
Moja ya kesi hizo imefikishwa mahakamani na Muungano wa CORD wenye
kuongozwa na Raila Odinga, kiongozi wa ODM, aliyekua mpinzani mkuu wa
Uhuru katika uchaguzi wa urais. Ya pili imewasilishwa mahakamani na
asasi ya kiraia. Kesi hizo lazima zisikilizwe siku 14 baada ya mashtaka
kufunguliwa.
Hizo zitakua kesi za mwanzo zenye uzito kuwahi kusikilizwa na
Mahakama ya Juu tangu Mahakama hiyo iundwe miaka miwili iliyopita.
Kesi hizo zitasikilizwa na majaji watano. Majaji hao wakiamua kwamba
kweli palifanyika mizungu na ghiliba nyingine katika uendeshwaji wa
uchaguzi na hasa katika kuhesabu kura basi Mahakama ya Juu yanaweza
yakaubatilisha uchaguzi wa urais.
Ukifikiwa uamuzi huo basi uchaguzi wa urais itabidi ufanywe upya katika muda wa siku 60 kutoka siku itapotolewa hukumu hiyo.
La majaji wakiamua kwamba uchaguzi uliendeshwa kihalali basi Uhuru
na Ruto watabidi walishwe viapo vya kuzishika nyadhifa zao katika muda
wa siku 14 kutoka siku waliotangazwa kuwa ndio washindi.
Wafuasi wa Raila wamegawika kuhusu kesi hiyo. Kuna wenye kuunga
mkono kufunguliwa mashtaka hayo lakini wapo pia wenye kuhisi ya kwamba
lau CORD itashindwa mahakamani basi Raila anaweza akajiharibia jina
lake. Wengine wanasema kwamba wao wamekwishakubali kwamba upande wao
umeshindwa na hawataki taifa ligubikwe na hali ya wasiwasi.
Lakini ilivyo ni kwamba Raila aliyezoea kumpiga madongo Uhuru na kumsengenya kwa mafumbo sasa ameazimia kummaliza mahakamani.
Kizingiti cha pili kinachowakabili akina Uhuru na Ruto ni kesi yao
mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini
Hague, Uholanzi.
La ajabu ni kwamba kesi hiyo, kinyume na ilivyotarajiwa, ni moja ya
mambo yaliochangia kuwajenga washtakiwa hao wawili waliokua wagombea
wenza katika uchaguzi uliopita.
Kesi hiyo pia ndio iliyowafanya wazidi kushirikiana. Chambilecho ubeti mmoja wa kale hivi sasa Uhuru na Ruto wamekua:
‘Ni chanda na pete
Ulimi na mate
Uta na upote…’
Ulimi na mate
Uta na upote…’
Hivi karibuni kuwamekuwako dalili kwamba kesi dhidi ya Uhuru imekua
ikidhoufika na ndio maana haikua ajabu kwamba Mahakama ya ICC siku ya
Jumatatu iliyafuta mashtaka yote aliokuwa akishtakiwa Bwana Francis
Muthaura, katibu wa zamani wa baraza la mawaziri, aliyeshtakiwa pamoja
na Uhuru.
Kabla ya uchaguzi wa Machi 4 tulikuwa hatwishi kuambiwa kwamba kesi
hizo zilizo mbele ya Mahakama ya ICC zitauhatarisha uchaguzi usiweze
hata kufanyika.
Pili tukiambiwa kwamba kesi hizo zitakua suala kuu la kujadiliwa kwenye kampeni za uchaguzi.Yote hayo mawili hayakutokea.
Hata hivyo kwa vile Uhuru na Ruto wameshatangazwa na Tume ya
Uchaguzi kuwa ndio washindi wa kinyanganyiro cha urais lazima tukae
kitako na kuutafakari mustakbali wa urais wa waheshimiwa hao wawili
wanaokabiliwa na mashtaka ya jinai.
Kesi zote hizo mbili hivi sasa zimeahirishwa; ya Ruto inatazamiwa kusikilizwa Mei na ya Uhuru mwezi Julai.
Wawili hao wamekua wakishikilia kuwa hawana nia ya kuzikwepa kesi za
Hague.Kwa hivyo wanasema watakua wakifunga safari kwenda Hague
kuhudhuria vikao vya kesi kila pale wanapohitajika kwenda huko.
Mji wa Hague uko masafa ya kilomita 10,542.1 kutoka Nairobi kwa
safari ya gari au kilomita 6,676 kwa safari ya ndege. Safari ya gari
kati ya miji hiyo ni ya muda wa takriban siku sita na saa tano wakati
safari ya ndege ni ya saa nane na nusu.
Urais na umakamu wake ni kazi. Ni kazi ya kila siku (haina mapumziko
ya kawaida ya Ijumaa au Jumapili) na saa zote wenye nyadhifa hizo
wanatakiwa wawe hadhir na tayari kukabiliana na changamoto yoyote
itayozuka wakati wowote ule naiwe mchana naiwe usiku.
Ndipo watu wakawa wanajiuliza:“Uhuru na Ruto watawezaje kutekeleza
majukumu ya kazi zao endapo watakua hawapo nchini na wapo mahakamani
Hague wakijibu mashtaka?”
Miongoni mwa majukumu ya Rais na naibu wake ni kuhudhuria na
kuongoza vikao vya baraza la mawaziri ambalo kwa kawaida linakutana
mara moja kwa wiki. Sasa ikiwa Rais na naibu wake watakua wanakosekana
mara kwa mara katika vikao hivyo serikali itakua inaendeshwa bila ya
viongozi wake wakuu na pingine hata bila ya dira.
Isitoshe, baraza la mawaziri kadhalika huwa na kamati ndogo kadhaa
zenye jukumu la kulishauri baraza zima pamoja na Rais. Bila ya shaka
patazuka mushkili katika kazi za kamati hizo endapo Rais atakua
anakosekana kwa vipindi vya muda mrefu katika vikao vya baraza la
mawaziri. Tusisahau kwamba yeye Rais ndiye moyo wa baraza hilo, ni
kiungo muhimu cha shughuli zote za baraza la mawaziri.
Halafu kuna suala la majeshi. Rais ni amiri jeshi wa majeshi yote ya
Kenya na ndiye mwenye mamlaka ya uongozi wa majeshi hayo. Kwa sasa
majeshi ya Kenya yanakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama
isizowahi kuzikabili kabla.
Hali ya usalama ndani ya nchi ni ya wasiwasi na majeshi ya Kenya yamo vitani kupambana na magaidi wa Al-Shabaab nchini Somalia.
Katika nyanja hiyo ya usalama ni Rais pekee mwenye uwezo wa kikatiba
wa kutangaza hali ya hatari nchini. Na ni yeye pekee mwenye uwezo wa
kutangaza vita. Taarifa zote nyeti za usalama wa taifa zinamfikia yeye.
Naibu wa Rais, kwa upande wake, ndiye mwenyekiti wa kamati ya
usalama ya baraza la mawaziri. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Waziri
wa Usalama wa Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Sheria na
Shughuli za Kikatiba, Waziri wa Fedha, Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu
wa Idara ya Utumishi wa Umma.
Kamati hiyo ndio yenye kumshauri Rais kuhusu mambo ya usalama na ndio yenye kujitwika jukumu la kuhakikisha usalama wa taifa.
Hivyo, hali ya usalama nchini huenda ikasambaratika endapo Rais au
naibu wake atakua anatakikana awe anakwenda Hague kila mara kwa sababu
ya kesi. Wote wanahitajika nchini kwa sababu wote wana majukumu nyeti
kuhusika na usalama na ulinzi wa taifa.
Pamoja na hayo niliyokwishayataja kuna shughuli nyingi nyingine
ambazo pia zinamhitaji Rais na naibu wake wawe watu wasiobabaishwa na
mambo kama ya kesi ya ICC.
Safari za mara kwa mara za kwenda Hague kuhudhuria vikao vya kesi
bila ya shaka zitaziathiri vibaya kazi za Rais na naibu wake.
Aidha, kazi hizo zitazidi kutatanika kwa vile viongozi hao wawili
watakua si makini. Wanatakiwa wawe na akili zilizotulia kushughulikia
mambo ya kitaifa na sio mara kwa mara wawe wana wahka kuhusu
yanayotokea katika mahakama ya ICC na nini yatakuwa matokeo ya kesi yao
na majaaliwa yao.
Jambo jingine litaloweza kuwatia mtegoni ni msimamo wa nchi
nyingine. Nchi jirani za Kenya kwa jumla hazina tatizo na kuchaguliwa
kwa Uhuru. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari Uhuru anakubalika
zaidi miongoni mwa marais wa Afrika ya Mashariki na wa nchi za Maziwa
Makuu kushinda Raila.
Tunajua kwamba kuna kiongozi mmoja mkuu wa eneo hili ambaye hata
kumuona Raila hataki seuze kuwa na maingiliano naye. Na hawa ni watu
ambao zamani walikuwa wakisikilizana. Kwa hivyo, kwa upande wa
majirani Uhuru hatokuwa na tatizo.
Tatizo atalipata kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi — hasa
Uingereza, Marekani na Jumuiya ya Ulaya. Nchi hizi zimedhamiria kumtia
adabu kwa msimamo wake wa kutokubali kuyumbishwa asisimame katika
uchaguzi uliopita. Hii ndio sababu inayowafanya wengi watie shaka
kwamba nchi hizo zikitaka Raila asipambane na mgombea atayeweza
kumshinda.
Na haya ndio yanayowafanya baadhi ya wachanganuzi wa siasa za Kenya
waamini kwamba madola ya Magharibi tangu mwanzo yakimtaka Raila awe
rais mpya wa Kenya. Wengine wamefika hadi hata ya kumuelezea Raila
kuwa ni ‘kibaraka’ wa madola ya Magharibi yakiwa pamoja na Israel.Swali
linalozidi kuulizwa ni: ‘Nini ambacho Raila ameiziahidi nchi za
Magharibi na kwa nini?’
Tunavyoelewa ni kwamba katika miaka miwili mitatu hivi iliyopita
mahusiano kati ya nchi za Magharibi na Kenya yaliporomoka wakati
serikali ya Rais Mwai Kibaki ilipoigeukia China kwa misaada, hasa katika
ujenzi wa miundombinu.Ilifika hadi hata balozi wa Ufaransa akabidi
alalamike hadharani kwamba anapata shida kubwa kupangiwa muda wa
kuonana na Kibaki.
Kabla ya uchaguzi baadhi ya madola ya Magharibi yalitoa vitisho
vilivyotafsiriwa kuwa ni jaribio lao la kuwataka wapigaji kura wa Kenya
wasimchague Uhuru na mwenza wake. Hayakusema kama yataiwekea Kenya
vikwazo lakini wengi walichukulia kwamba hayo ndio yaliokusudiwa.
Mfano wa Sudan na wa Rais wake Omar Hassan al Bashir ulitolewa. Kwa
mtazamo wangu hizo ni ndaro tu za madola ya Magharibi. Kenya si
Sudan.
Nchi za Magharibi na hasa Uingereza zina maslahi makubwa ya kiuchumi
nchini Kenya na hazitotaka rasilmali zao na maslahi yao yadhurike kwa
hatua zao dhidi ya Kenya kwa sababu viongozi wake ni Uhuru na Ruto.
Wala Kenya si Iran kwani tunajua sababu hasa inayoyafanya madola ya
Magharibi yaziandame nchi hizo mbili. Serikali ya Kenya haina Uislamu
unaoyataabisha madola hayo katika Iran na Sudan.
source: Raia Mwema: Ahmed Rajab
No comments:
Post a Comment