WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 28, 2013

Nyerere: Wasomi wameiharibu Elimu; Wafungua shule kwa pupa; Watoa “elimu kimbizi”



 Picture
Hapa nimefuatisha kwa maneno, asilimia kubwa alichokizungumza hayati Mwalimu Nyerere katika hotuba aliyoitoa mwaka 1985 mjini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Chama Cha Elimu ya Watu Wazima (CHAWATA). Anasema:
Kama Taifa, tunastahili kujikumbusha tena umuhimu wa aina zetu mbalimbali za elimu, na mkazo wetu mbalimbali wa elimu.

Nilipokuwa nikizungumza na Watalalamu wa Elimu safari moja Arusha, karibuni hivi, nilijitahidi sana, kuwaomba wataalamu wetu wa elimu, waipe elimu yetu uhuru na hatua zake mbalimbali, umuhimu unaostahili. Bila hivyo tutapoteza fedha, tutapoteza wakati, tutajivunja moyo kwa sababu tunatoa mkazo katika elimu, ambao haulingani na mahitaji yetu.

Sasa hivi nchini, karibu kwa watu wote pamoja --nina hakika na wataalamu kama ninyi, wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima-- kuna “demand” kubwa ajabu, ya elimu ya sekondari. Kubwa ajabu. Nasikia wilaya zingine wana mipango watakuwa na watafungua tatu tatu, elimu ya sekondari, na wanafurahi kabisa wenyewe wanaona wanafanya jambo la ajabu kabisa, la kufungua sekondari tatu, wengine nne, kuna mashindano ya ajabu sana. Mazuri? Mazuri!

Lakini ni mashindano ya pupa bila kufikiri.

Pupa tu. Bila kukaa na kufikiri maana yake nini. Unasema nini? Elimu hii mnayoisema hata maana yake ni nini? Na hatima yake ni nini?

Kila ukifikiri, ukikaa na kufikiria sana, ni “escapism”. Si kukabili kweli. Si kulitizama tatizo letu la Tanzania la elimu na maendeleo ukasema tunaihitaji elimu hii kwa sababu bila hii hatuna maendeleo. Si maana yake. Ni “elimu ya ukimbizi”.

Viongozi wa Serikali, wa Chama na “Professionals” hawa wa elimu, wanatuongoza katika elimu ya ukimbizi. Ya kukimbia matatizo. Si elimu ya kutatua matatizo. Hapana. Ni elimu ya kukimbia matatizo. Ni elimu ya kutukimbiza tutoke vijijini. Hawatupi elimu turudi vijijini tukae vijijini na kubadili mazingira yetu yale ambayo haturidhiki nayo, tuliyabadili kwa sababu ya elimu tuliyopata, hapana. Elimu wanayotupa ni ya kukimbia kutoka vijijini. Na hasa inayotokana kabisa na jambo la kufanya kazi kwa mkono. (Elimu) Ya kwenda ofisini.

Marehemu Karume, alikuwa ananiambia, “Lakini mwalimu, elimu hii mnayowapa vijana hawa yoooooote, ya kwenda maofisini, na tuwape meza, Mwalimu tutafuta miti Tanzania!”

Anasema mwalimu tutafuta miti, tutapata wapi meza nyingi namna hiyo? Alikuwa ana-exaggerate lakini niliwahi kumsikia Mmarekani mmoja anasema, “ exaggeration is the art of teaching.” Lakini alikuwa (Karume) ana-point.

Tunaelimisha watu kwenda maofisini. Tumeharibu kabisa mawazo ya watu wetu juu ya elimu, na viongozi wa mawazo haya ni wasomi. Viongozi wa mawazo haya ya kupotosha katika jambo la elimu ni wasomi. Anakujia mtu, “Mwalimu mwanangu ameshindwa, sasa sijui nitafanya nini.” Huyo mtoto wake anayesema ameshindwa, amemaliza elimu ya miaka saba. Taifa limejitahidi limempa elimu kijana huyu miaka saba. Anasema, mwanangu ameshindwa sasa sijui nitafanya nini. Mchukue. Nasema, “nimchukue nimpeleke wapi” Mimi nimchukue nimwingize katika kubeba wakimbizi, wanatoka Butiama. Nibebe wakimbizi kutoka Butiama, kila nikitoka Butiama nina kundi la wakimbizi. Anasema, “nenda naye Mwalimu, mpe kazi yoyote tu Mwalimu, hata ya kusafisha madirisha ofisini kwako.” Mimi nina madirisha mangapi hayo?

Nilijitahidi siku hiyo kusema na Wataalamu wa Tanzania, jamani, hivi ndivyo, elimu hii tunayoitoa, ya ukimbizi --na si Tanzania peke yake, hizi nchi zinazoitwa “third world” zote kabisa-- zenyewe “internally” kila moja ndani yake, Tanzania yenyewe ina kazi hizi za ofisini, zaidi zinafanywa mijini na vijijini kidogo kidogo, elimu ya maana zaidi kwa Tanzania wanavyoiona ndugu zetu, ni elimu inayomhamisha mtu kutoka kijijini kwenda mjini. Elimu ya “secondary”. Na kweli ni elimu ya kuhamisha tu kwa sababu kijana wetu huyu wa “secondary” akiipata elimu yake ile jinsi mlivyompa, akibaki Butiama ni “liability”. Ni “liability” kwa mama yake, kwa shangazi yake, kila mtu (kwa sababau) “he can't work”. Hakufundishwa kufanya kazi. Amefundishwa kukimbia, kwa hiyo pale kijijini anakuwa ni tatizo kubwa. Mtu amesoma miaka 11 au 12 lakini kijijini ni tatizo kabisa kwa sababu ya aina ya elimu aliyopewa.

Nilijitahidi kuwaeleza ndugu zangu, wataalamu wa elimu hapa Tanzania, elimu tunayoitaka, elimu kubwa kupita zote ni ile ambayo tumeipa jina la kweli kweli (yaani) Elimu ya Msingi. Ndiyo msingi wa elimu  yetu. Sasa msingi hauwi mbovu bwana! Msingi hauwi mbovu. Utaalamu wako na nguvu zako, kwa sababu elimu yako yote itabebwa na ule msingi. Msingi hujengwa imara kabisa. Na lazima elimu ya msingi, ijengwe imara kabisa. Maliza kwanza msingi kabla hujajenga huku juu, ama sivyo litaanguka jumba lako. Sasa wote hao wanaokazana tunataka kuongeza “secondary” ni hawa wanaotaka kujenga mapaa mazito wakati msingi hakuna. Jumba litaanguka! Wamekazana na mapaa tu, paa paa... msingi upo?

Hivi nilipokuwa nyumbani juzi nimesikitika sana, wanakuja walimu nazungumza nao, walimu wa elimu ya msingi, wananiambia, “Mzee, siyo kwamba hatuna shule, (bali) hatuna madaftari, hatuna kalamu za kutosha, nyumba za walimu hazitoshi, madarasa hayatoshi.” Mwalimu mmoja ananiambia safari hii wanafunzi wangu wa darasa la saba katika kufanya mtihani wao, imebidi kila mmoja kutoka nyumbani aje na vigoda viwili --kimoja akalie, kimoja aandikie-- na sisi waongozaji wa elimu tupo, lakini tumekazana tunataka kujenga masekondari mengine matatu,  mengine manne, mengine matano katika mkoa, lakini je, msingi tayari? Mmekamilisha msingi? Muwanyime hawa Watanzania, mamilioni, muwanyime nyie elimu yao “minimum”, mkazane na kuongeza elimu kwa watu wengine ambayo hata hatuihitaji kwa Taifa, isipokuwa ni mzazi anataka kumkimbiza mtoto wake tu, kila mmoja apate nafasi ya kumkimbiza mtoto wake.

Tukamilishe elimu ya msingi. Ndiyo elimu “number one”. Miaka saba elimu nzuri. Na miaka saba si muda mfupi hata kidogo. Kama vifaa vinatosha, walimu wanatosha, mishahara yao mizuri, mazingira yao mazuri, nyumba wanazo, miaka saba ni muda mzuri sana wa elimu. Si nchi nyingi sana zinatoa elimu ya miaka saba. Ni muda mrefu sana.

Pili baada ya hapo, ni elimu ya kuwaendeleza hawa. Bado “attention” kwa Watanzania wote. Ni elimu ya kuwawezesha kufanya kazi, siyo kukimbia kazi. Elimu ya kuwawezesha Watanzania kwa maana elimu ni ya Watanzania. Ni elimu ya Taifa. Elimu ya taifa haiwezi kuwa kwa watu wachache tu, ni kwa walio wengi. Na wote sasa wanasoma. Tungekuwa tunafikiria elimu ni kuwawezesha wananchi wetu kuandika, kusoma na kuhesabu, hii tungeifuta tu. Si ni sisi tusiojua kusoma tukishakufa si basi? Wengine wote watakaobaki watajua kusoma na kuandika na kuhesabu na sisi wengine saa 11 imefika, wengine saa 11 na nusu, kama ingekuwa “problem” ni hiyo, ninyi CHAWATA mngekuwa hamna kazi kwa maana kweli jambo la kujua kusoma, kuandika na kuhesabu linafutwa katika elimu ya msingi. Kila “generation” zinazokuja zinajua kusoma na kuandika lakini, elimu wanayoitaka ni elimu ya kufanyia kazi. Ni elimu ya ufundi na kukomaa kwa mawazo. Mawazo yanayoelekea kwenye kazi na kuendesha mazingira yetu.

Nimejitahidi kueleza. Tumejitahidi huko nyuma kusisitiza shule za ufundi. Hawataki watu wetu. Hasa ninyi wasimamizi wa elimu. Hawataki! Hawazungumzi. Hivi sasa, hivi Tanzania... michango mingi ni michango ya shule za elimu ya ukimbizi. Si elimu ya ufundi ya kuwawezesha vijana, kijana huyu mwenye elimu ambaye akiipata elimu hii, akirudi kwa mama yake, mama yake anamwona mkombozi huyu kwa sababu ana kazi anayoweza kuifanya.

Picture
Julius Kambarage Nyerere
Januari 13, 1985
Akifunga Mkutano wa Chama Che Elimu ya Watu Wazima (CHAWATA)  Dodoma

Source: http://www.wavuti.com

No comments:

Post a Comment