Kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima.
Kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima,
amesema kuwa atakuwa tayari kusaini mkataba mpya wa kuichezea Yanga
katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara endapo watampa dola za
Marekani 150,000 (Sh. milioni 240).
Mkataba wa Niyonzima aliyejiunga na Yanga mwaka juzi akitokea APR ya Rwanda unamalizika mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka kwao Kigali,
Rwanda ambako amekwenda kuitumikia nchi yake inayokabiliwa na mechi
dhidi ya Mali Jumapili, Niyonzima, alisema hataki kurudia makosa
aliyofanya mwaka jana.
Niyonzima alisema anaamini kuwa hicho kiwango cha fedha ndiyo dau
lake kwa sasa au zaidi na ameamua kuwaambia Yanga kutokana na hatua yao
ya kukataa kumruhusu mwaka jana kujiunga na El Mereikh ya Sudan
iliyokuwa imekubali kumlipa kiasi hicho.
Kiungo huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa lake (Amavubi),
aliongeza kuwa hivi sasa kazi ya kuzungumzia mkataba wake itafanywa na
wakala wake.
"Mambo nahitaji yafanyiwe kazi kabla sijaamua kuendelea kubaki Yanga, ikiwamo kuongezewa mshahara,'' alisema Niyonzima.
Kiungo huyo kipenzi cha mashabiki wa Yanga aliongeza kuwa hataki
kupoteza nafasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati alipokuwa
akiichezea APR ambao hawakuwa tayari kumruhusu kirahisi kuondoka ndani
ya timu hiyo inayotetea ubingwa wake wa ligi Kuu ya Rwanda.
Akizungumzia matakwa hayo ya Niyonzima, Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Yanga, Seif Ahmed, aliiambia NIPASHE jana kuwa wako katika
mipango ya kuwapa mikataba mipya wachezaji wao wote wanaowahitaji
kuendelea kuwa nao kabla ya kumalizika kwa ligi.
Hata hivyo, Ahmed alisema hawawezi kusema ni lini watakamilisha
kazi hiyo kwani hiyo ni mipango ya viongozi wa klabu kwa kushirikiana na
benchi kao la ufundi.
Niyonzima na Mrisho Ngassa wa Simba waliivutia El Mereikh baada ya
kuonyesha kiwango kizuri katika mashindano ya Kombe la Chalenji
yaliyofanyika mwaka jana nchini Uganda lakini Ngassa aliamua kuikacha
timu hiyo kwa madai kwamba anazingatia maslahi yake na siyo kukimbilia
kucheza nje. Nafasi ya nyota hao ilichukuliwa na Selemani Ndikumana
kutoka Interclub ya Burundi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment