Na Debora Ngajilo na Andrew Msechu
Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewashukuru wananchi pamoja na Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kushinda nafasi hiyo huku akiahidi kuijenga upya Kenya.
Uhuru amesema ataweka kipaumbele kwenye kutunza rasilimali za nchi na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote, pia kuwawezesha wanawake na vijana.
Katika hotuba yake aliyotoa muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi jana, Kenyatta alisema anawashukuru wagombea alioshirikiana nao katika mchakato wote wa uchaguzi na kuwakaribisha kuungana.
“Nawashukuru wagombea wenzangu wote kwa kujitolea kwa moyo kushiriki katika kinyang’anyiro hiki kwa kuwa jambo hilo limezidi kuonyesha demokrasia iliyopo nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa anaahidi kushirikiana vyema na wagombea hao akiwamo Raila Odinga kwa ajili ya kuijenga upya nchi yao, akiwakaribisha na kuwataka waondoe kinyongo kutokana na ushindi alioupata.
“Tulianza zoezi zima kama timu na nitashirikiana nanyi kama timu, ikiwamo kuhakikisha tunafuata yale yote yaliyopo kwenye katiba hususan kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake anayostahili.”
Kiongozi huyo pia aliwashukuru watu mbalimbali waliofanikisha uchaguzi huo kwenda vyema ikiwamo vyombo vya habari katika nchi hiyo ambavyo vilikwenda sambamba katika kuripoti matukio yote ya uchaguzi, pamoja na vyombo vya usalama vilivyosimamia chaguzi hizo.
“Usalama bado ni tatizo katika nchi yetu, lakini ningependa kuvishukuru vyombo husika kwa kufanikisha tunavyozidi kuendelea suala hilo litakuwa vizuri,” alisema.
Uhuru alieleza hayo baada ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) kumtangaza kuwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika Machi 4 akiwa amegombea kwa tiketi ya muungano wa Jubilee.
Uhuru aliibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizohitajika ili kupata ushindi kulingana na mahitaji ya Katiba Mpya ya nchi.
Matokeo yaliyotolewa na IEBC yanaonyesha kuwa Uhuru alipata kura 6,173,433 ambazo ni asilimia 50.07 huku mpinzani wake Raila Odinga akipata 5,340,546 ambazo ni asilimia 43.28.
Kwa ushindi huo, Uhuru amepata idadi kubwa ya kura inayohitajika na Katiba Mpya ambayo ni zaidi ya asilimia 50+1 na kuzuia uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi.
Uhuru pamoja na mgombea mwenza wake, William Ruto wamepata ushindi huo huku wakiwa wanakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Ushindi huo umepingwa na mpinzani mkuu wa Uhuru, mgombea urais kupitia muungano wa Cord, Raila Odinga ambaye amesema ‘kamwe hawatayatambua’ na kuahidi kuyapinga mahakamani.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Odinga alisema anajiandaa kwenda mahakamani kupinga matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru.
Odinga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa matokeo yaliyotolewa na tume hiyo yalikuwa yamehujumiwa hasa baada ya kutokea hitilafu katika mitambo ya elektroniki iliyokuwa inatumiwa katika shughuli hiyo.
“IEBC imerudia makosa yaleyale ya uchaguzi mkuu wa 2007, kwa kuwa tuna mahakama tunayoiamini tunaomba watu wetu watulie hadi mahakama itakapotoa uamuzi. Wenzetu pia wajiepushe na aina yoyote ya ghasia,” alisema.
Alisema kwamba hana tatizo la kushindwa iwapo ameshindwa kihalali, lakini kwa matokeo haya ana jukumu kubwa la kupinga mahakamani ili kulinda mahitaji na heshima ya wapiga kura.
Aidha, alisema kugoma kwa mitambo hiyo kulichanganya mambo katika shughuli ya kuhesabu kura.
Alisema kuwa baada ya kutokea hitilafu, kura alizokuwa amepata katika maeneo bunge ambayo ni ngome zake, ziliongezwa kwenye hesabu ya kura za muungano pinzani wa Jubilee.
Siku moja kabla ya kutangaza matokeo hayo, IEBC ilikiri kuwa matatizo yaliyosababishwa na mtambo wake wa kupeperusha matangazo ni pamoja na kuongeza mara nane kura zilizoharibika.
Baadhi ya wananchi walieleza kuwa na wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoonekana kuharibika, kwani zilikuwa kura zaidi ya 300,000 ambapo kwa sasa zimepungua mpaka kufika idadi ya kura 80,000, baada ya kuhakiki kura hizo kwa mara ya pili.
Pingamizi lao lilikataliwa
Mapema wiki hii, wakati shughuli ya kuhesabu kura za urais ilikuwa inafanyika, wanaharakati walifungua kesi mahakamani kutaka uchaguzi usimamishwe kutokana na hitilafu mbalimbali zilizotokea , lakini mahakama kuu ilitupilia mbali kesi yao ikisema kuwa haina uwezo wa kufanya uamuzi katika kesi hiyo, na kuwa ni mahakama ya juu zaidi pekee inayoweza kusikiliza kesi hiyo.
Matokeo hayo na mivutano yote iliyopo kwa sasa vinatokea baada ya siku tano tangu Wakenya kupiga kura kuchagua rais, magavana, maseneta, wabunge, wawakilishi wanawake na wawakilishi wodi.
Tume ya uchaguzi ilichukua zaidi ya saa tano kukagua hesabu ya kura hizo kabla ya kutangaza matokeo hayo jana mchana.
Kwa mujibu wa maagizo yaliyopo katika Katiba Mpya ya nchi hiyo, mshindi wa uchaguzi anatakiwa kutangazwa iwapo tu ametimiza masharti ya kikatiba ya kutangazwa kuwa rais wa nne wa Kenya.
Pamoja na ushindi wa kura kwa zaidi ya asilimia 50 lazima awe ameshinda asilimia 25 katika nusu ya kaunti zote 47 nchini Kenya.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment