KESHO ni siku muhimu sana kwa wananchi wa
Jamhuri ya Kenya. Hiyo ndiyo siku wananchi hao watakapofanya Uchaguzi
Mkuu kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo, kuanzia
Rais, wabunge na wengine wa ngazi za kati na za chini.
Tunasema ni siku muhimu sana kwa wananchi hao wa Kenya kwa sababu moja kubwa. Uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2007 uligubikwa na vurugu, mauaji na umwagaji damu wa watu wasio na hatia, hali ambayo Wakenya walikuwa hawajawahi kuishuhudia tangu nchi yao ilipopata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1963.
Hata baada ya amani kurejea nchini humo kutokana na juhudi zilizofanywa na wasuluhishi wa kimataifa kwa kuwashawishi washindani wakuu kuunda Serikali ya Mseto, maelfu ya wananchi walibaki bila makazi kutokana na vurugu za uchaguzi huo na mpaka leo wamebaki katika makambi kama wakimbizi wakitegemea msaada kutoka ndani na jumuiya ya kimataifa.
Hivyo, uchaguzi wa kesho una umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Kenya. Kwa kuwa vurugu za mwaka 2007 zilichafua taswira ya nchi hiyo mbele ya dunia, kesho Wakenya watataka waihakikishie jumuiya ya kimataifa kwamba Kenya Hakuna Matata, kwa maana kwamba Kenya ni nchi ya amani na kwamba vurugu, umwagaji damu na mauaji ya kikabila yaliyotokea katika uchaguzi huo hakika ilikuwa bahati mbaya.
Kwa maneno mengine, uchaguzi wa kesho ni fursa
muhimu na ya pekee kabisa kwa wananchi wa Kenya kuuonyesha ulimwengu
kwamba nchi hiyo ina siasa za kistaarabu na utamaduni wa kuvumiliana,
baada ya matukio ya mwaka 2007 yaliyoipaka matope na dunia kuiona kama
nchi ya visasi, ukabila na maangamizi.
Imeonekana bayana kwamba wananchi wa Kenya,
wakiwamo wanasiasa na wagombea katika ngazi mbalimbali katika uchaguzi
utakaofanyika kesho nchini humo, wamepata somo la kutosha kutokana na
vurugu za uchaguzi uliopita. Katika kampeni zao za kutaka kuungwa mkono,
wagombea wote mara hii wameonekana kuhimiza utaifa, amani, umoja,
mshikamano na wamelaani vikali utamaduni wa kuwagawa wananchi katika
misingi ya dini na ukabila.
Ni kwa sababu hiyo tunasema uchaguzi wa kesho nchini humo utafanyika kwa amani na kumalizika salama. Rais Mwai Kibaki anayemaliza muda wake wa uongozi ameshatamka pasipo kutafuna maneno kwamba ataikabidhi nchi kwa mgombea atakayeshinda uchaguzi huo kihalali na kuthibitishwa na mamlaka zote husika kwa mujibu wa Katiba ya Kenya. Sisi wa Mwananchi tunawatakia Wakenya uchaguzi mwema na wa amani hapo kesho.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment