RAIS Jakaya Kikwete amewaagiza
polisi, wakuu wa mikoa na wa wilaya kutofanya ajizi kwenye suala la wachochezi
wa kidini, bali wachukue hatua stahiki na kwa haraka ili kuendeleza amani ya nchi.
Kikwete alitoboa hayo kupitia hotuba
yake ya mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi kwa Taifa kupitia vyombo vya
habari Dar es Salaam.
“ Nimewakumbusha polisi na mamlaka
husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo.
Wawachukulie hatua stahiki wale wote
wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao ajizi nyumba
ya njaa”, alisema.
Alisema kuwa wachochezi wa
mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa
Watanzania wasiokuwa na hatia akiwataka wakuu wa wilaya na mikoa kutimiza
ipasavyo wajibu wao kama walinzi wa amani.
Alisema wakati wote Serikali haitasita
kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu
vitakatifu vya dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine
Kuhusu matokeo mabovu ya mtihani wa
kidato cha nne mwaka 2012, Rais Kikwete alitaka utafiti ufanyike ili kujua
chanzo na kusisitiza kwamba bila utafiti wa kina kufanyika ,
tatizo hilo linaweza kuwa kubwa na kuligharimu taifa.
“Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani
huo na kati yao, waliofaulu ni 126,851 sawa na asilimia 34.5, wanafunzi
240,903 ambao ni asilimia 65.5 hawakufaulu. Kwa ulinganifu, matokeo hayo
ni mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi
karibuni.
Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya
nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika,”alisema Rais Kikwete
na kuongeza:
“Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne
mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki
kabisa.
Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu
kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia
34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali,
ni kubwa sana.”
Rais Kikwete alisema kuwa mambo hayo,
ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya
kuliangalia suala zima la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake.
“Hii
itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo
mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni.
Tusipofanya
hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa
Serikali,”alisema Kikwete.
Rais
katika hotuba yake pia alizungumzia suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC) ambapo alifafanua kwamba nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) walikubaliana kupeleka vikosi vya kulinda
usalama nchini humo wakiungwa mkono na Umoja wa Mataifa utakaolifanya jeshi
hilo kuwa sehemu ya vikosi vyake vya kulinda amani DRC (MONUSCO)
“Tumepeleka
walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini tusipeleke Kingo...: Kama
nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni
jambo lenye maslahi makubwa kwetu.
Ina
maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika
kutokuwapo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu,”
alisema Rais Kikwete.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment