Hayo
ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na
utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi sana Watanzania
wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu. –
Kikwete (Hotuba ya Mwisho wa Mwezi Februari, 2013)
KUNA kila dalili kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa muumini wa
propaganda ya historia mpya ya Tanganyika ambayo imekuwa ikienezwa
chini kwa chini na ambayo imepata mashabiki.
Kwa muda mrefu sasa katika hotuba zake mbalimbali Rais Kikwete
amekuwa akijitahidi ama kujilinganisha na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere na kumuonesha kuwa yeye Kikwete amefanya mengi kuliko Nyerere
au kwa namna moja au nyingine kuanza taratibu kulifuta jina la Nyerere
na mchango wake wa pekee.
Anaamini kafanya mengi kuliko Nyerere
Mojawapo ya mambo ambayo yanatokea kwenye utawala wowote ambao
umebakia na muhula mmoja tu wa kuongoza ni kujaribu kutengeneza
kumbukumbu (legacy).
Karibu marais wote katika nchi za kidemokrasia wanapofikia miaka
michache kabla ya muhula wao kwisha hujaribu kufanya mambo ambayo jamii
zinazokuja nyuma zitawakumbuka. Sasa hivi Rais Kikwete yuko katika
wakati kama huo ambapo anajaribu sana kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo
vitamkumbuka kwa mengi.
Yeye mwenyewe anaamini kuwa amefanya mambo mengi sana ya maendeleo na
amejitamba hivyo mara kadhaa akijilinganisha na viongozi
waliotangulia.
Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa CCM
yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma mwezi mmoja uliopita Rais Kikwete
alitangaza kuwa anataka pale atakapoondoka madarakani akumbukwe kama
“bwana maendeleo”. Sababu ni kuwa anaamini kuwa utawala wake umeleta
maendeleo mengi kuliko wengine waliomtangulia.
Ukimuuliza mtu anayeamini nadharia hii utaona kuwa wote watakuonesha
‘wingi’ wa vitu ambavyo vimefanywa na utawala wa RaisKikwete.
Mrundikano wa magari, majengo mapya, barabara, hospitali, vyuo, shule
na vingine vingi. Watu wanaoamini maendeleo kama ‘ongezeko la kiasi’
watakimbia kwa haraka kuonesha “vitu” kama dalili ya maendeleo. Hawa
husema “mbona wakati wa Nyerere hatukuwa na x, y, na z” na kwa vile
hivyo “x, y, na z” vipo chini ya utawala wa Kikwete basi Kikwete
kafanya mengi kuliko Nyerere.
Sasa kuna ukweli wa aina yake na usiopingika katika hili. Hata hivyo
ni ukweli ambao unavutia watu wasiofikiri. Nyerere ameanza kuongoza
Tanzania akiwa na madaktari 12 na wahandisi wawili wazalendo. Nyerere
alipoanza kuongoza hakukuwa na chuo kikuu cha Tanganyika, walitegemea
Chuo Kikuu cha Makerere ambacho sehemu ya Tanzania ilikuwa ni tawi
lake.
Wakati Nyerere anaanza hivyo hakuna rasilimali watu ambazo Kikwete
leo anazo. Lakini matokeo yake ni tofauti. Wakati Nyerere anaondoka
madarakani uwezo wa kujua kusoma na kuandika ulikuwa umefikia asilimia
91 hivi; leo Kikwete pamoja na shule, vyuo, walimu na misaada lukuki
wanaojua kusoma na kuandika ni kama asilimia 69 hivi! Na cha kuudhi
zaidi (kama kuna namna ya kuudhika zaidi) ni kuwa pamoja na mabilioni
yote ambayo Kikwete ameyatumia kwenye elimu leo hii watoto wetu
wanafeli vibaya zaidi kuliko wakati wowote tangu tupate uhuru! Ati
bwana maendeleo!
Lakini kubwa zaidi ni hili la historia mpya ya Tanganyika. Katika
hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari ambayo seemu yake nimeinukuu
hapo juu Kikwete anajaribu kufanya kiile ambacho kimekuwa kinafanywa na
baadhi ya watu sasa hivi cha kuandika upya historiaya Tanganyika ambayo
inapunguza, kudharau na kwa namna Fulani kukejeli mchango wa kipekee
wa Baba waTaifa MwalimuNyerere.
Je, amani yetu ililetwa na mababu?
Katika simulizi hii mpya amani tunayoiona sasa hivi haikutokana na juhudi za kipekee na mchango wa kipekee wa Nyerere.
Kumhusisha Nyerere na amani hii ni kumpa sifa asiyostahili. Hivyo,
katika simulizi hili jipya Nyerere “aliikuta” amani hii na hakufanya
lolote lile la kipekee la kuhakikisha kuwa katika Tanganyika mpya amani
itamalaki. Na wapo wenye kuamini hili.
Uamuzi wa busara
Bahati mbaya sana historia ina ushahidi wa tofauti sana. Matukio
makubwa kadhaa wakati wa uongozi wa Mwalimu yalichangia sana
kuhakikisha kuwa amani katika Tanzania inadumu. Kwanza ni ule uamuzi wa
kura tatu wa mwaka 1958.
Huu ulikuwa ni mmoja wa uamuzi wa kimkakati ambao ulibadilisha kabisa
mwelekeo wa siasa za nchi yetu. Uamuzi huu wa busara ulihakikisha kuwa
TANU inakuwa na nafasi ya pekee ya kushinda uchaguzi ule.
Hata hivyo nyuma ya mkakati ule ilikuwapo nia ya wazi ya kuvuruga
mpango wa kundi dogo la baadhi ya viongozi ambao walikuwa wanataka
kuingiza udini katika siasa.
Kujiuzulu waziri mkuu
Mojawapo ya uamuzi wa kijasiri kabisa wa Baba wa Taifa na ambao
ulichangia sana kuongeza umoja, amani na utulivu wa nchini pale
alipoamua kujiuzulu uwaziri mkuu ili vkuijenga TANU.
Ikumbukwe kuwa Nyerere alishazunguka karibu Tanganyika yote kabla ya
Uhuru kueneza TANU lakini mara hii ya pili Nyerere alikuwa anazunguka
kuwapa Watanganyika nafasi ya kujitambua kama taifa moja na watu wamoja
chini ya TANU. Ilikuwa ni muda wa kujenga utaifa zaidi – wakoloni
hawakutuachia hisia ya utaifa bali nchi moja yenye makabila mbalimbali
na hali mbalimbali za maisha.
Misukosuko ya miaka kumi ya kwanza
Kama kuna wakati mgumu katika historia ya nchi yetu ni hii miaka 10
ya kwanza. Wanaosema Nyerere hakuwa na nafasi ya pekee katika kuleta na
kudumisha amani yetu hawajui historia yetu. Wamezoea mazungumzo ya
barazani. Ndani ya miaka 10 ya kwanza ya Uhuru, Nyerere alikumbana na
changamoto ambazo hakuna rais mwingine baada yake amekutana nazo.
HAKUNA. Baadhi ya changamoto hizo:
- Baa la Njaa (mara tu baada ya Uhuru)
- Mvurugano wa kidini na kuvunjika kwa EAMWS
- Kuvunja baraza la machifu wa kikabila
- Maasi ya jeshi
- Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano
- Siasa za kimataifa za vita baridi
- Kuendelea kwa ukoloni kusini mwa Afrika
- Njama za kuipindua serikali
- Mgongano ndani ya TANU
Lakini ni kutokana uongozi hodari wa hekima wa Baba wa Taifa
Tanzania ikapita salama. Wapo waliojeruhiwa, wapo walioumizwa lakini
taifa letu likapita salama. Na hoja inaweza kujengwa kuwa hata miaka
kumi ya pili (1971-1981) ilikuja na changamoto za aina yake ambazo
Kikwete hajazipitia na zote zilikuwa zinahusiana na amani na utulivu na
usalama wa Tanzania. Leo hii wengine tunajiuliza hivi Kikwete angekuwa
rais katika kipindi cha kwanza au cha pili cha miaka kumi, mtu ambaye
hata hajui kwa nini Tanzania ni masikini kweli Tanzania ingekuwapo?
Ni kwa sababu hiyo Watanzania wanapaswa kuangalia upya jaribio la
viongozi wachache kuficha udhaifu wao kwa kuubeza na kuukejeli kiaina
uongozi adimu wa Baba wa Taifa. Watanzania wawasikilize jinsi
wanavyojaribu kupuuzia mchango huo wakiamini kwa kufanya hivyo
wanawaridhisha (appease) mashabiki wao.
Uzuri ni kuwa historia itasimama kamili kuonesha mchango wa pekee,
uliotukuka, na usiona mfano wa Baba wa Taifa katika kuleta, kulinda, na
kudumisha amani.
Amani hii inapovunjwa leo hii, wakulaumiwa ni hawa hawa. Hawawezi
kukwepa kwani walipewa nchi salama salmini sasa inaweza kuvunjika
mikononi mwao, na wananchi wake wakibaki majeruhi wa siasa dhaifu
zilizoshindwa.
source: Raia Mwema: Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment