HOFU ya udini imetamalaki. Ni hofu ya kweli, maana, udini umeanza kuvuna roho zetu.
Kupitia safu hii nimepata kuandika mwaka mmoja uliopita, kuwa nchi
yetu muda si mrefu itaingia katika mparaganyiko wa kijamii
utakaotokana na siasa kuchanganyika na dini. Tayari tumeshafika hapo.
Inasikitisha.
Ndugu zangu, mbegu za chuki za kidini zimeshapandwa. Zimeanza sasa
kuchipua. Kama tutatanguliza busara na hekima, basi, hatujachelewa. Tuna
lazima ya kuing’oa na mizizi yake, miche yote ya udini iliyochipua, na
ambayo, kuna hata baadhi ya wanasiasa, wanadiriki kuimwagilia maji ili
isinyauke, kwamba ina manufaa kwao. Ni manufaa ya kisiasa.
Na hakika, ni busara na hekima, kwa mwanadamu kutambua na kuheshimu
mamlaka iliyopo na zaidi, inayotokana na watu. Kutambua na kuheshimu
mamlaka inayotokana na sheria, kanuni na taratibu za mahali husika,
hivyo basi, mamlaka inayotokana na Katiba ya wakati huo. Na mwanadamu
huyo, midhari amefanya mawili hayo, ana lazima ya kufanya jambo la
tatu; kuyaenzi mamlaka hayo.
Yawezekana kabisa, kuwa katika kuyapata mamlaka hayo kukawa na
mapungufu ya sheria, kanuni na taratibu. Lakini, hayo yasipewe nafasi
ya kufanya mchakato wa kisiasa katika jamii ukakwama. Maana, siasa ina
maana ya majadiliano endelevu. Ni majadiliano yasiyo koma. Muhimu
katika siasa ni kubaki katika meza ya majadiliano.
Tunapokandamiza kwa makusudi mkondo wa siasa usichukue nafasi yake,
na hapa pia kwa maana ya kukandamiza siasa za upinzani, basi,
tunaruhusu uwepo wa ombwe la kisiasa. Hivyo, nguvu hasi za kijamii
hupenya kwa urahisi kuziba ombwe hilo. Ni pamoja na makundi ya kidini
yenye misimamo mikali na ya hatari kwa amani ya taifa.
Maana, katika nchi yetu tumeanza kuziona dalili mbaya za siasa
kuchanganyika na dini. Na Uchaguzi Mkuu uliopita umetoa ishara mbaya.
Ishara za nchi yetu kukumbwa na siasa zilizochanganyika na udini .
Watanzania tuliwashuhudi baadhi ya viongozi wa kidini; Uislamu na
Ukristo, wakitumia nyumba za ibada, si kwa kazi ya kiroho, kazi ya
kuhubiri yaliyo mema kwa mwanadamu, bali viongozi hao wa kidini
wamefanya kazi ya siasa. Kazi ya kuhutubia mambo ya siasa na kutoa
maelekezo ya kisiasa ya moja kwa moja.
Hayo yamefanyika misikitini na makanisani, ni hatari. Jambo hili
linaiweka rehani amani ya nchi yetu. Linahatarisha Umoja wetu wa
Kitaifa. Maana, makanisani na misikitini wanakusanyika Watanzania wa
itikadi tofauti za kisiasa, na wengine ni watoto, hawajawa tayari
kupokea hotuba za kisiasa, bali watoto wako tayari kupokea mahubiri na
mafundisho ya kiroho.
Tumefika mahala, kiongozi wa kidini anatamka kwenye nyumba ya
ibada; “Msiwachague wale wenye kutoa kofia na fulana”. Mwingine
anatamka; “ Msiwachue watakaotuletea vita”. Katika mifano hiyo miwili
ya kauli ni dhahiri, kuwa bila kutaja ni akina nani wenye kutoa kofia
na fulana waumini wameshawajua ni akina nani. Na bila kuwataja hao
‘watakaotuletea vita’ waumini wameshawajua ni akina nani. Hayo mawili
hayawezekani yakawa ni mafumbo magumu kwa waumini kutoka kwa viongozi wa
dini.
Hapo inapandikizwa sumu ya chuki miongoni mwa waumini, maana,
waumini hawana itikadi zinazofanana. Hapo viongozi wa dini
wanashiriki kutenda maovu. Kuwagawa wananchi katika misingi ya udini.
Maana, nao , kwa mgongo wa imani, wanashiriki kutoa hukumu bila ya
wenye kuhukumiwa kupewa nafasi ya kujitetetea.
Wahenga wetu walisema” Kamba ukatikia pabovu”. Kamwe huwezi
kuwavuruga Watanzania na kuwafanya wachinjane kwa sababu za kudai kuna
upendeleo wa ukabila au wa kisiasa. Nchi hii ina makabila zaidi ya 125
na utitiri wa vyama vya siasa.
Mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa
wachinjane ni kwenye masuala ya imani, ni kwenye dini. Tusikubali dini
iwe ndiwe penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania.
Hakika, ni wajibu wetu wa kizalendo kuyazungumza haya kinagaubaga,
kuwa hapa kuna tatizo linalotunyemelea. Tatizo la udini. Maana,
Watanzania sisi tuna hulka ya ajabu kidogo. Wakati mwingine tunaamini
kuwa kama jambo unalinyamazia, basi halipo hata kama lipo. Tatizo
unaliona, lakini unachofanya ni kunyamaza kimya tu. Kinachofanyika hapo
ni kufagilia tatizo chini ya jamvi badala ya kufanya jitihada ya
kuliondoa.
Na waumini wanaamini, kuwa Shehe haongopi na Padri au Mchungaji vivyo
hivyo. Inakuwaje basi, pale Shehe, Mchungaji au Padri anapotenda
dhambi ya kusema uongo? Dhambi ya kufanya maonevu? Waumini, kama vile
wanakondoo, watakuwa wamekosa wachungaji. Na hao viongozi wa kidini
watakuwa ni sehemu ya kuchochea machafuko katika jamii.
Naam, sasa ni dhahiri, kuwa dini imejichanganya na siasa. Na huu si mseto mwema kwa nchi yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Source: Raia Mwema: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment