- Kila jambo ni kwa masafa mafupi, hata jengo la Bunge
MSOMAJI
utakumbuka kwamba nimekuwa nikisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na
mipango inayoangalia masafa marefu, kwa sababu hapa ndipo kwetu,
tumefika na wala hatuna kwingine tunakoelekea.
Kwa bahati mbaya sana tunendelea kufanya mambo yetu kana kwamba
tunapita njia. Nimekuwa nikitoa mifano kadhaa, lakini kila uchao naona
mifano mingine ya kufanya mambo yetu kwa haraka haraka kama vile kuna
mahali tunakokimbilia.
Majuzi nilikuwa na majadiliano makali yaliyoishia kuwa ubishi badala
ya kuwa ni mabadilishano ya mawazo na mashindano ya fikra. Tulikuwa
tunajadili hoja yangu kwamba jamii iliyodhamiria kujiletea mabadiliko
inajionyesha kwa kila kitu inachofanya, kuanzia ujenzi wa makazi,
miundo ya uzalishaji, mifumo ya elimu, misingi ya ulinzi na usalama, na
kadhalika.
Nilikuwa natoa rai (na rai hiyo nairejea leo) kwamba tunajenga
majumba ambayo hayaonyeshi uimara na umakini unaoashiria kwamba tupo
hapa kuishi na kudumu daima -umu. Hatuhami mwaka ujao wala miaka 500
ijayo.
Hili, kimsingi, ni tatizo la Afrika nzima, na linadhihirisha jinsi
ambavyo hatuna uwezo wa kuangalia maisha ya taifa letu kwa masafa ya
miaka elfu au zaidi ijayo.
Tuangalie majumba tunayojenga, hata majengo ya idara zinazostahili
hadhi ya juu, ni majumba yasiyo kuwa na haiba yoyote. Mfano wa moja kwa
moja ni jengo la Bunge lililojengwa mjini Dodoma katika miaka ya hivi
karibuni, na ambalo halinipi kabisa taswira ya jengo la baraza kuu la
utunzi wa sheria na usimamizi juu ya serikali.
Jengo la Bunge lililoko Dodoma lingeweza kabisa kutumika kama jengo
la maonyesho ya teknolojia ya kompyuta au maonyesho ya vifaa vya
maabara, au hata ukumbi wa disko, lakini siyo jengo la Bunge kwa sababu
halionyeshi haiba ya kasri ambalo ndani yake mambo mazito yanajadiliwa
na kuamuliwa.
Aidha nashuku kwamba muda hautakuwa mrefu kabla jengo la Dodoma
halijahitaji ukarabati mkubwa kutokana na matumizi ya vifaa duni katika
ujenzi wake.
Hatuhitaji kwenda mbali kuona kinyume cha jengo la Dodoma,
tunapoangalia jengo la Karimjee ambalo ndilo lilikuwa na ukumbi ambamo
Bunge lilikuwa likiketi. Tofauti kabisa.
Tumetembea sana bara Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko, ambako
tumejionea wenyewe jinsi majengo, hata ya shughuli zisizokuwa za dola,
yaliyojengwa karne ya 11 bado yamesimama leo hii na yanawafanya kila
wanaoyaangalia kutekwa na mastaajabu.
Tumeona jumba la Ikulu ya Marekani, jengo la Congress, jengo la
Mahakama Kuu ya Marekani, Westminster, Whitehall (Uingereza), makao
makuu ya Serikali ya India na Mahakama Kuu ya nchi hiyo, na kadhalika.
Kwetu Waafrika, majengo yenye hadhi kama hayo niliyoyataja ni yale
yaliyoachwa na mkoloni, kwa sababu mkoloni, angalau katika baadhi ya
makoloni yake, alikuwa na fikra za kubakia milele, na kwa sababu hiyo
alijenga vitu vya kudumu.
Inashangaza, basi, kwamba sisi ambao ndio tungetakiwa tuwe na
mwelekeo wa kudumu kwa kuwa hapa ni kwetu, sisi ndio tunaojenga viota
vya kujishikiza, kana kwamba tunajibanza kwa muda tukisubiri muda wa
kuendelea na safari yetu. Ajabu iliyoje.
Katika miaka ya mwanzo ya sabini baadhi ya majengo adhimu ya Jiji la
Dar es Salaam, kama vile Kaiserhoffya zamani na Splendid Hotel,
yalivunjwa na badala yake tukasimamisha maboksi yasiyo na sura wala
roho. Mwanza pia wakabomoa Mwanza Hotel na kuweka boksi lao mahali
pake.
Katika hili sina budi kumshukuru yeyote aliyechukua uamuzi wa
kuinusuru iliyokuwa Dar es Salaam Club ya enzi za ukoloni, kasha ikawa
Fordhani Hotel na sasa ndiyo makao makuu ya Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jengo lile linafanana kidogo na shughuli inayofanyika humo, lakini
mengine mengi ni vichekesho. Kuna wakati katika miaka ya sabini
ilizungumzwa kwamba jingo lile livunjwe tuweke boksi jingine.
Mtaalamu mmoja aliandika kitabu kwa jina “The Edifice Complex” ambamo
anaeleza uzito wamuonekano wa jengo katika saikolojia ya watu
mbalimbali. Kasri kubwa zilizosimikwa kama mahala pa ibada zilijengwa
kwa njia ambayo ilimfanya kila aliyeingia humo, au hata alitazame
kutoka nje, kufanya heshima, na hata woga.
St Paul’s jijini London, au Kadedraliya Cologne, au Msikiti wa Samawi
(Blue Mosque) na Sulaymaniaya Istanbul, ni mahali ambapo kila muumini
anayeingia anahisi kwamba yuko mbele ya nguvu kuu, na viwango vya
upuuzi na mawazo ya hovyo vinapungua sana.
Hii ni kweli kwa hayo majengo niliyoyataja huko nje, lakini hata
hapa kwetu nyumbani tunaona nyumba za ibada zinazozalisha hisia za
adabu na heshima.
Majengo ya Warumi wa kale, pamoja na barabara zao, majengo ya
Wayunani, pamoja na mahekalu yao, piramidi za Misri kabla ya hapo,
vyote vilijengwa na jamii zilizojiona kama za kudumu, jamii
zisizoondosheka
Msomaji anaweza akashangaa ni kwa nini nimechukua nafasi kubwa
kujadili suala la majengo, lakini napenda kumhakikishia kwamba majengo
na usanifu wake, huonyesha umahiri wa jamii husika na umakini katika
kufanya mambo yake. Pia ni chanzo cha fahari mbele ya jamii nyingine au
mataifa mengine.
Jamii inayoshindwa kusimamisha majengo ya nguvu yaliyosanifiwa na
wajuzi wa hisabati zilizopangiliwa wakishirikiana na wana sanaa
wanaojua kuuunganisha kilichoimara na kinachopendeza, jamii ya namna
hiyo itakuwa ya kubabaisha kila siku, itakuwa inatafuta vitu rahisi,
vyepesi na visivyodumu. Vitu vya mpito.
Hata ikiambiwa elimu yake imekufa kabisa, jamii ya aina hiyo itaunda
kamati ya haraka haraka ili kutuliza ghadhabu za wanajamii wachache
wanaouliza maswali, kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu, magumu
mno.
source: Raia Mwema Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment