Rais
wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema hatavumilia kuona baadhi ya
watu wanafanya vitendo vya chokochoko za kidini kwa nia ya kutaka
kugawanya Watanzania.
Akizungumza kwenye Maulidi ya kuzaliwa
Mtume Mohamad (SAW) katika Msikiti wa Majumuiyat wa Temeke jijini Dar es
Salaam juzi, Dk Shein alisema mgawanyiko kati ya Watanzania ni kitu
kisichokubalika daima.
Kwenye sherehe hiyo iliyoandaliwa na
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum, ilihudhuriwa na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk.
Reginald Mengi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha na viongozi mbalimbali.
Dk. Shein alisema msingi wa dini ya
kiislamu ni usawa wa binadamu kwa kila mmoja kumpenda mwenzake, ni kosa
kubwa kutumia dini kwa kudhulumu maisha ya mtu au mali zake.
Aliwasisitizia waumini hao warudi kwenye dini na kuangalia misingi yake pamoja na hadithi za Mtume (SAW).
Alisema Zanzibar ina historia kubwa ya
watu wa dini zote kuishi kwa pamoja kama ndugu na yaliyotokea kwa
viongozi wa dini kuuawa ni matukio mageni yanayotakiwa kuondolewa
haraka.
Awali mlezi wa msikiti huo, Rais Mstaafu
Alhaj Ali Hassan Mwinyi alisema lazima Watanzania walinde amani yao
iliyodumu kwa miaka mingi.
Alitahadharisha endapo waumini wa kiislamu
wakitaka kuwadhuru wakristo kwa namna yoyote, na wakristo nao wakawa na
nia kama hiyo, nchi haitakuwa salama na hakuna atakayefurahia maisha.
"Tanzania ni ya sisi sote, ndani tupo wa
dini na makabila mbalimbali, hivyo inatulazimu tupendane na kuishi kwa
pamoja kulinda utamaduni wetu wa upendo," alisisitiza mzee Mwinyi.
Kwa upande wa Sheikh Majid Salehe, alisema
wanasiasa waepuke kuwajaza watu maneno ya uongo na kusababisha
maandamano na kuchukia serikali yao.
Sheikh huyo aliongeza kwamba endapo
wanasiasa wakitumia njia hiyo watakuwa wanakwenda kinyume na matakwa ya
dini na itasababisha nchi kukosa amani.
Alipongeza hatua ya Sheikh ya mkoa kutetea
kwa nguvu zote suala zima la amani, kitendo hicho ni kufuata kwa
vitendo mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo, Alhaji Salum ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, aliwatunuku watu
mbalimbali vyeti vya kutambua mchango wao wa kulinda amani nchini.
Waliotunukiwa vyeti hivyo ni Dk. Mengi,
Lowassa, Waziri Nahodha, Waziri wa Viwanda, Dk. Abdallah Kigoda na Mkuu
wa Mkoa wa Said Meck Sadick.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment