LICHA
ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza kumwajibisha Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake wajiuzulu kutokana na matokeo
mabaya ya mtihani wa kidato cha nne 2012, chama hicho kimesema yapo pale
pale. Chama hicho
kimewaomba wananchi wote waliochoshwa na kufelishwa kwa watoto wao,
kunyimwa elimu bora wajitokeze kuandamana kwa nguvu zote, na wanafunzi
wote waliofeli pia wajitokeze kudai elimu bora kwani ni haki yao.
Akizungumza
kwa simu na gazeti hili (Tanzania Daima) jana na kutoa msimamo huo,
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema "wananchi wajitokeze kwa
wingi ili kilio chao kisikike duniani kote."
Alisisitiza
kuwa maandamano hayo yatafanyika mbele ya ugeni wa Rais wa China, Xi
Jinping ili kufikisha kilio hicho na kamwe haikubaliani na sababu ya
serikali kuyazuia kwa sababu ya ugeni huo.
Alisema
maandamano hayo yatasaidia kupuuza kunakofanywa na Serikali ya CCM
kuonwe na dunia nzima maana vyombo vyote vya habari vitafuatilia tukio
hilo.
Mbowe
aliongeza kuwa, "Watanzania waliochoshwa na ubabaishaji katika elimu
wajitokeze, kulaani kitendo cha Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu
wake, Philipo Mulugo kulindwa na serikali, badala ya kuwajibishwa kwa
matokeo mabaya ya watoto wa Kitanzania."
Alipoulizwa
itakuwaje maana kutakuwa na ugeni wa Rais wa China nchini, sababu
ambayo hata serikali imeitumia ili kuyazuia maandamano hayo, Mbowe
alijibu: "Kilio chetu hakikuja na Rais wa China, kama Serikali ya CCM
wanaona aibu kumwajibisha waziri mmoja na naibu wake, basi wasubiri aibu
ya dunia kuona jinsi Tanzania inavyoendeshwa kibabe, ikiwa haina elimu
bora.
"Tumetangaza
maandamano wiki tatu zilizopita, hatukuwa na taarifa na ujio wa Rais wa
China, lakini jinsi Mungu alivyo upande wetu amemleta Rais wa China,
kweli Mungu ni mwema, hakuna tena nafasi ya kusubiri kuficha ubovu
katika sekta ya elimu nchini, ndani ya siku ambayo CHADEMA waliandaa
maandamano ili dunia nzima isikie kilio cha Watanzania kuhusu elimu.
"Sababu
kuwa CCM nao wameandaa maandamano kupinga maandamano ya CHADEMA hazina
msingi ni kutowajibika kwa Jeshi la Polisi. Hatukatazi maandamano,
polisi wapange ratiba siku tofauti, sisi tutaandamana kumpinga waziri
ili kama CCM wataandamana kumpongeza waziri wao wapangiwe siku yao, ila
sisi tulitangaza mapema na barua tulipeleka kwa mujibu wa sheria za nchi
yetu."
Alipoulizwa
kwanini asisubiri Tume ya Waziri Mkuu itoe majibu, Mbowe alisema:
"Hatuna shida na Tume ya Waziri Mkuu, matatizo ya elimu katika nchi yetu
yapo wazi, tukizungumza bungeni wanatuchakachua, na sasa huku nje
wanatukejeli, tunataka ifike mahali wajue kuwa nchi hii ni yetu sote, na
Watanzania wanapaswa kusikilizwa kilio chao."
Kwa
mujibu wa Mbowe, maandalizi ya maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika
katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, yamekamilika.
Jana,
Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa barua iliyosainiwa na mkurugenzi wake,
Assah Mwambene kuzuia maandamano yaliyokuwa yafanyike Jumatatu ijayo
katika mikoa ya Mbeya na Arusha tu.
Taarifa hiyo haikuzungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wala Mwanza.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, serikali ilisema kuwa maandamano ya
CHADEMA yalipangwa kuhusisha wananchama kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa,
Njombe na Ruvuma, na kuongeza kuwa CCM ilipanga kufanya maandamanno yake
mkoani Arusha kupinga kusudio la CHADEMA kuandamana, wakieleza kwamba
wana imani na tume maalumu ya Waziri Mkuu inayochunguza tatizo la
kufanya vibaya wanafunzi wa kidato cha nne.
Awali
CHADEMA walitangaza maandamano yatakayofanyika katika kanda nne. Kanda
ya Kusini yatafanyika Mbeya; Kanda ya Ziwa yatafanyika Mwanza; Kanda ya
Kaskazini yatafanyika Arusha, na Kanda ya Mashariki yatafanyika Dar es
Salaam.
Tanzania
Daima ilipomuuliza Mkurugenzi wa Maelezo imekuwaje yeye akawa msemaji
wa jambo hili, alijibu: "Mimi ni msemaji wa serikali, hata Ikulu
naisemea, hivyo usiulize kwanini naisemea polisi."
---
CHANZO: Tanzania Daima la Machi 24, 2013
CHANZO: Tanzania Daima la Machi 24, 2013
No comments:
Post a Comment