Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba
Maoni yaliyotolewa na wananchi kwa ajili ya kuunda katiba mpya
hayataingizwa yote kwenye rasimu ya katiba, bali yatakayoingizwa ni yale
tu yatakayopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Waziri Mkuu
mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alipozungumza na waandishi wa habari,
jijini Dar es Salaam jana, kuhusu uundwaji wa mabaraza ya katiba ya
wilaya yatakayopitia rasimu ya katiba mpya na kutoa maoni yake.
Alisema uamuzi huo unatokana na kuwapo kwa maoni yaliyotolewa na
wananchi yanayokinzana, hivyo kuyaingiza yote kunaweza kufanya vifungu
vya katiba moja kupingana vyenyewe kwa vyenyewe.
Jaji Warioba alisema kuwa rasimu ya katiba mpya itaanza kupitiwa na
mabaraza ya katiba ya wilaya na kutoa maoni yao, kuanzia Juni, baada ya
uandaaji wa rasimu hiyo kukamilika Mei, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kwa kuzingatia hitaji hilo la kisheria,
Tume iliandaa Mwongozo unaoelekeza uundwaji na uendeshaji wa mabaraza
hayo.
Jaji Warioba alisema kuwa Mwongozo huo umechapishwa katika magazeti
mbalimbali na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ili wananchi na wadau
wengine waweze kuusoma na kuuzingatia.
Alisema Tume pia imechapisha vitabu vyenye mwongozo huo na
kuvisambaza kwa ofisi za wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa miji,
manispaa na majiji kwa Tanzania Bara ili wawafikishie wananchi katika
mitaa na vijiji.
Jaji Warioba alisema kwa Zanzibar, Mwongozo umesambazwa kwa ofisi
za wakuu wa wilaya, baraza la manispaa na katibu wa halmashauri za mji
ili wawafikishie wananchi katika shehia zao.
Alisema kwa mujibu wa Mwongozo huo, kuanzia leo, wananchi wenye
sifa na wanaopenda kuwa wajumbe wa mabaraza hayo, wataanza kuwasilisha
maombi yao kwa maofisa watendaji wa vijiji au mitaa kwa Tanzania Bara na
kwa masheha kwa upande wa Zanzibar.
Jaji Warioba alisema mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ni Machi 20,
mwaka huu na kwamba mwananchi anayependa kuomba nafasi ya kuwa mjumbe
wa baraza la katiba anatakiwa awe ni raia wa Tanzania, awe na umri wa
miaka 18 au zaidi, awe na uwezo wa kusoma na kuandika.
Pia awe mkazi wa kudumu wa kijiji/mtaa/shehia husika, awe ni mtu
mwenye hekima, busara na uadilifu na awe ni mtu mwenye uwezo wa
kujieleza na kupambanua mambo.
Vilevile mwombaji anatakiwa kuandika barua mbili, ambazo
ataziwasilisha ofisi ya mtendaji wa kijiji au mtaa kwa Tanzania Bara na
kwa sheha kwa Zanzibar.
Jaji Warioba alisema barua moja itabaki ofisini na ya pili atabaki
nayo baada ya kutiwa saini na kugongwa mhuri kuthibitisha kuwa ombi
lake limepokelewa.
Alisema barua ya maombi iwe na majina kamili yamwombaji, jinsi
yake, umri wake, elimu yake, kazi yake na sehemu anayoishi katika
kijiji, mtaa au shehia husika.
Jaji Warioba alisema baada ya muda wa kuwasilisha maombi kukamilika
Machi 20, mwaka huu, orodha ya majina ya waombaji itabandikwa katika
eneo la wazi na mbao za matangazo za ofisi ya mtendaji wa mtaa, kijiji
au shehia ili wananchi waweze kuona majina yote ya waombaji na kama wana
sifa.
Alisema katika Mwongozo wake, Tume imeelekeza orodha hiyo ibandikwe
katika maeneo ya wazi na mbao za matangazo Machi 22 hadi 28, mwaka huu.
Jaji Warioba alisema kuanzia Machi 30 hadi Aprili 3,
mwaka huu, kutafanyika mikutano mikuu ya mitaa, vijiji au shehia
kwa Zanzibar ili kufanya uteuzi wa wagombea kupitia mikutano na kwamba,
kura za siri zitapigwa.
Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, mikutano hiyo itaitishwa na afisa mtendaji wa kijiji au mtaa husika.
Jaji Warioba alisema mkutano huo utaendeshwa na mwenyekiti wa
kijiji au mtaa husika na ofisa mtendaji wa kijiji au mtaa atakuwa katibu
wa mkutano huo na ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi wote
walioomba kuingia kwenye baraza la katiba la wilaya.
Alisema katika mikutano hiyo, Tume imeelekeza kuwa wajumbe wote wa
mkutano mkuu maalum watapiga kura za siri wakianza kwa kumchagua mtu
mzima mmoja, ambaye anaweza kuwa mwanamke au mwanaume.
Baada ya hapo, wajumbe watapiga kura ya siri ya kumchagua mwanamke
mmoja na kufuatiwa na wajumbe kupiga kura ya siri ya kumchagua kijana
mmoja, ambaye anaweza kuwa mwanaume au mwanamke mwenye miaka kati ya 18
na 35.
Alisema mwisho, wajumbe wote watapiga kura ya siri ya kumchagua mtu
mwingine yeyote kutoka miongoni mwa wananchi walioomba kuwa wajumbe wa
baraza la katiba la wilaya.
Jaji Warioba alisema majina ya wananchi walioteuliwa na mitaa au
vijiji yatawasilishwa katika vikao maalum vya kamati za maendeleo za
kata vitakavyofanyika kati ya Aprili 5-9 ili kuchagua wawakilishi wanne
wa kata.
Alisema baada ya hapo, Aprili 13-17, majina ya wananchi
waliochaguliwa katika mkutano maalum wa kamati za mendeleo za kata
yatatakiwa kuwasilishwa kwa mkurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa
na kwamba, kata husika ipo kwa Tanzania Bara.
Jaji Warioba alisema kwa mkurugenzi wa baraza la manispaa, katibu
wa halmashauri ya mji au wilaya ilipo shehia kwa Zanzibar, ambaye
atawasilisha kwa katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya
uteuzi rasmi wa kuwa mjumbe wa baraza la katiba la wilaya husika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment