Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuchunguza ajali ya meli ya MV. Skagit
iliyotokea tarehe 18.7.2012
ilipokuwa ikitokea Dare s Salaam kwenda
Zanzibar imependekeza kuchukuliwa
hatua za kisheria na kinidhamu watu
saba kwa makosa mbali mbali
yaliyochangia kutokea kwa ajali hiyo
ili kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji
kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa
baharini na watendaji wa Taasisi
zinazosimamia suala hilo na kuepusha
ajali za mara kwa mara.
Akitoa taarifa ya Tume hiyo kwa
Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara
ya Habari Maelezo Mnazimmoja, Katibu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee
amewataja watu waliopendekezwa kuchukuliwa
hatua za kisheria ni mmiliki wa
MV.Skagit ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni
ya Seagull Sea Transport Said
Abdul-rahman Juma, Nahodha wa meli hiyo
Makame Mussa Makame na Meneja wa
Kampuni hiyo tawi la Dar es salaam Omar
Hassan Mkonje.
Amesema kutokana na matendo yao ya kuwa
karibu mno na sababu zilizopelekea
kutokea kwa ajali hiyo, Tume
imependekeza watu hao washtakiwe kwa kosa la
kusababisha vifo kutokana na uzembe.
Mmiliki wa kampuni hiyo amefanya kosa
la kufanya biashara ya usafiri wa
baharini kwa kutumia chombo ambacho
hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria na
kutumia chombo ambacho hakikutimiza
masharti ya ukaguzi kwa mujibu wa
sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar
namba 5 ya mwaka 2006, kumuajiri
nahodha bila ya kuwa na cheti cha
umahiri cha daraja la tano na kuruhusu
meli kupakia idadi kubwa ya abiria
kinyume na uwezo wake.
Abdulhamid amesema taarifa hiyo imesema
Nahodha Makame Mussa ametenda kosa
la kuendesha meli akiwa hana cheti,
kushindwa kuwaandaa abiria kujiokoa
wala kutoa taarifa ya dharura,
kuendesha meli hali ya kuwa si salama na
kuruhusu kupakia abiria 431 badala ya
250 iliyoainishwa kwenye cheti cha
abiria.
Watu waliopendekezwa
kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni aliekuwa Mkaguzi
wa meli na Kaimu Mrajisi wa meli kutoka
Mamlaka ya usafiri wa baharini
Zanzibar Juma Seif Juma, Mkaguzi wa
kujitegemea Capt. Saad Shafi Adam na
Maafisa wa usalama wa bandari ya Dar es
Salaam Johari Mikidadi Ndumbati na
Peter Ndimbwa Mwasi kwa kushindwa kudhibiti
uingizaji wa abiria katika meli
ya MV. Skagit siku iliyopata ajali
ikiwa ni kinyume na majukumu yao ya kazi.
Taarifa hiyo imetoa mapendekezo ya
kuimarisha Sheria na kanuni za usafiri
wa baharini namba 5 ya 2006 kwa
kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu
ikiwemo kuweka utaratibu wa kisheria
utakaowalazimisha wafanyabiashara wa
usafiri wa baharini kuwa na utaratibu
wa kuuza tiket za safari pamoja na
kutengeneza urodha ya wasafiri kwa njia
ya electroniki na kuweka utaratibu
wa kisheria unaowalazimisha uongozi wa
kampuni unaoendesha biashara ya
usafiri wa baharini kuwa na taaluma ya
masuala ya usafiri wa baharini.
Aidha Abdulhamid amesema Tume hiyo
imependekeza Kampuni kuwalipa fidia
abiria wote waliokuwemo ndani ya
meli. Kwa waliofariki walipwe thamani ya
kiwango cha mshahara wa chini cha muda
wa miezi 80 na walionusurika na
kupata ulemavu walipwe asilima 75 ya
kiwango cha waliofariki na watu
wengine walionusurika bila ya kupata
majeraha yoyote walipwe asilimia 50 ya
kiwango walicholipwa
waliofariki.
Katika ajali hiyo watu 81 wakiwemo raia
watatu wa kigeni walifariki na
maiti zao zilipatikana na
kuzikwa, 212 walipotea na 154 waliokolewa wakiwa
hai wakiwemo raia 15 wa kigeni.
Katibu Mkuu Kiongozi amesema Tume
imeeleza sababu za kutokea ajali hiyo
kuwa ni upepo mkali, muundo wa meli
ilioruhusu abiria wengi kukaa juu,
mwendo wa kasi, nahodha kukosa ujuzi na
umahiri na abiria kuwa wengi kupita
kiwango chake.
Amesmea Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imekubaliana na mapendekezo yote
yaliyotolewa na Tume hiyo iliyokuwa na
wajumbe 10 chini ya mwenyekiti wake
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar
Abdulhakim Ameir Issa.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment