Ni kweli malengo ya Mkukuta yanafikiwa?
Picha zinazowaonesha wakazi wa vijijini ambao
wanapaswa kukwamuliwa kupitia Mkukuta
BISHOP HILUKA
Dar es Salaam
MKUKUTA ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu chake kikiwa ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania. Hivi sasa tuna Mkukuta II ambao umeboreshwa kutoka katika Mkakati wa kwanza wa kupunguza umaskini uliozinduliwa Oktoba mwaka 2000 na kutekelezwa kuanzia 2005 hadi 2010.
Malengo ya Mkukuta yamejikita katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, ambapo eneo hili lina malengo sita likiwemo la kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini.
Kwamba wakazi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni wakulima wadogo watajengewa uwezo wa kuongeza tija na kupata faida ndani na nje ya sekta ya kilimo. Wakiwezeshwa kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo na kujengewa uwezo wa kuongeza thamani mazao wazalishayo ili waweze kupata faida.
Pia ilibuniwa kuwa wakazi wa sehemu hizo wajengewe uwezo wa kutumia raslimali zinazowazunguka ili kuongeza michango inayotokana na wanyama pori, misitu na uvuvi katika vipato vya jumuiya za vijijini.
Ukweli sioni juhudi za kivitendo zaidi ya nadharia katika kukamilisha malengo ya Mkukuta, sioni viongozi wakihamasisha wakulima vijijini kuzalisha mazao yenye faida kubwa na kuongeza upatikanaji wa nyenzo za kilimo na matumizi sahihi ya teknolojia sambamba na mbinu za usimamizi wa mavuno katika kaya za vijijini na kukuza miradi inayoongeza thamani katika kilimo, uvuvi mifugo na bidhaa za misituni.
Sioni watendaji wakitoa mafunzo ya stadi za maisha na ujasiriamali kwa watu wa vijijini hususani wanawake na vijana, kwani kundi hili ndio limekuwa likiathirika sana na hivyo wengi wao hukimbilia mijini wakidhani kuna unafuu na wengi wanaokosa elimu hiyo hupunjwa mazao na hivyo kubaki katika hali ya umaskini. Elimu ya ujasiriamali na mitaji ndiyo suluhisho pekee la kuwakwamua.
Ninachoona ni kukosekana miundombinu; barabara na umeme imekuwa kiwazo kikubwa cha juhudi za kujikwamua kiuchumi kwa wakazi wengi wa vijijini. Barabara zisizounganika zinakwaza usafirishaji wa mazao na kupata tija kwa wakati muafaka. Mazao mengi huozea mashambani hasa wakati wa msimu wa matunda
Pia wakulima wameendelea kuendesha kilimo cha kujikimu miaka yote kwa kutegemea mvua, uzalishaji ni duni, nguvu kazi ni haba na vitendea kazi ni duni. Hata zile pesa zilizowahi kutolewa na serikali wakati fulani katika kila mkoa, maarufu kama mabilioni ya JK, hazikuwasaidia walengwa na inasemwa kulikuwa na ugumu mkubwa wa kuzipata kutokana na masharti magumu ambayo walalahoi wasingeyaweza.
Kumekuwa na fursa finyu ya kupata mitaji na mikopo kwa wakazi wengi wa vijijini. Kupanda kwa bei ya mafuta ya taa, huku umeme na gesi vikiwa ni anasa kwa wananchi wa kawaida wa Tanzania, na kukosekana njia mbadala ya kupunguza matumizi halisi ya nishati ya kupikia ni changamoto kwa wengi katika kufikia malengo ya Mkukuta.
Mambo haya ndiyo sababu ya kuwa na asilimia moja tu ya watu, tena wenye asili ya mabara ya nje kumiliki uchumi wa Tanzania. Hii ni hatari kubwa, zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania kuendelea kumilikiwa na wageni, huku kukiwa na kilio kikubwa cha Watanzania wazawa, kutaka wajengewe mazingira mazuri ya uwezeshaji ili kumiliki uchumi wa nchi yao kupitia migodi mikubwa ya madini na maeneo nyeti ya kiuchumi!
Tangu uhuru Watanzania wengi hawajawahi kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wa nchi yao. Uchumi wa nchi umeendelea kutawaliwa na wageni wakishirikiana na Watanzania wachache. Inashangaza sana kuona tuna ardhi nzuri, tuna madini na rasilimali kibao lakini tunaendelea kuwa masikini wa kutupwa, tukitegemea misaada ya wahisani ili kuendesha maisha yetu!
Huduma za jamii; elimu na afya zimedorora mno, shule za serikali zimebaki majengo tu, walimu hawatoshi, vitendea kazi kwa walimu havitoshi na zana za kujifunzia kwa wanafunzi havikidhi mahitaji halisi, madawati hayatoshi na hivyo watoto wengi wanakaa chini wakati wakisoma, na michango na ada sasa ni kero na vikwazo kwa watoto wengi kupata elimu.
Shule za serikali zimekuwa kama biashara, ada na michango inaanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu. Ubaguzi katika elimu umekuwa rasmi, kwani kuna shule za matajiri na zile za watoto wa masikini, shule za matajiri zikiwa na huduma zote muhimu na za kisasa, wakati zile za walalahoi ziko hoi bin taaban.
Watoto wengi wa masikini sasa hawaendi shule na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, jambo linaloongeza umasikini miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa inakadiriwa kuwa wananchi karibu asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika.
Hospitali na zahanati za serikali sasa si mahali pa kuokoa maisha ya watu bali ni mahali pa kufia ndiyo maana wakati fulani watu waliona tegemeo pekee la kupata tiba ni Loliondo kwa Babu, na wakubwa wanakwenda India kwani hospitalini hakuna dawa na huduma zingine muhimu za matibabu.
Mkukuta hauwezi kufanikiwa kama Serikali itaendelea kuwa tegemezi, bajeti ya serikali kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa wageni kwa asilimia 35, na hivyo kusababisha manyanyaso na kuingiliwa kwa uhuru wetu kwa kupangiwa mambo ya kufanya na hawa wanaojiita wawekezaji. Hatuwezi kufanikiwa katika Mkukuta kwa mfumo huu, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana.
No comments:
Post a Comment