WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 28, 2012

Magufuli aja juu kwa nesi kunyofoa drip za watoto 7



Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameingilia kati sakata la muuguzi afya (nesi) wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita la kuwanyofolea chupa za maji ya dawa (drip) watoto saba waliolazwa hospitalini hapo.
Kutokana na tukio hilo ambalo lingeweza kusababisha vifo, Waziri Magufuli alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Chato kumkamata na kumfikisha mahakamani nesi huyo (jina tunalihifadhi) kwa kitendo hicho.

Inadaiwa kuwa nesi huyo alifikia maamuzi ya kuwaadhibu watoto kwa kuwakatia dawa baada wazazi wao kukataa kufanya usafi kwenye vyoo vya hospitali hiyo.
Tukio hilo ambalo limetokea jana majira ya asubuhi liliwalazimisha wazazi wa watoto hao kufanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa watoto hao walipiga simu kwa Katibu wa Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi aliyewasili hopitalini hapo akifuatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.
Akizungumza na wagonjwa, madaktari na wauguzi (manesi) na wahudumu wa afya, Dk. Magufuli alisema kitendo kilichofanywa na nesi huyo hakistahili kufumbiwa macho kwa kuwa kililenga kupoteza uhai wa wagonjwa waliokuwa wanaendelea kutumia dawa kutokana na maelekezo waliyopewa na madaktari.
Alisema kutokana na malalamiko mengi ya wagonjwa kuhusiana na huduma za afya zinazotolewa hospitalini hapo, kuna haja ya kutafuta mwarobaini wa kutibu vitendo vya ukiukwaji wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.
Kufuatia hali hiyo, Magufuli alimwagiza OCD wa Chato, Leonard Nyaoga, kuhakikisha Jeshi lake linamsaka na kumfikisha mahakamani nesi huyo kwa tuhuma za kutaka kusababisha vifo vya watu saba kinyume cha sheria.
Vilevile amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Shaban Ntarambe, kumsimamisha kazi mara moja wakati taratibu za kisheria zikiwa zinaendelea na kwamba hatakiwi kuonekana akitoa huduma kwenye hospitali hiyo kwa kuwa kitendo chake kimethibitisha kuwa hana sifa za kuwa muuguzi.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, ambaye aliongozana na Waziri Magufuli, alisema serikali inalishughulikia tukio hilo mpaka hapo sheria itakapochukua mkondo wake kwa kuwa kitendo kilichofanywa na muuguzi huyo siyo cha kiuungwana.
Mpongolo aliwataka wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu kutoa ushirikiano kwa viongozi wa hospitali yanapotokea matukio ambayo yanaweza kuhatarisha maisha kutokana na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya watumishi.
Pia, aliahidi kuunda kamati maalum itakayochunguza huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo kufuatia malalamiko mengi ya wananchi.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Pius Buchukundi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba ofisi yake imekwisha kuchukua hatua za kuhakikisha mtumishi huyo anawajibishwa kulingana na kosa alilotenda.
Dk. Buchukundi alisema kitendo cha watoto saba kuondolewa maji yenye dawa hakikufanywa kwa maelekezo ya uongozi wa hospitali hiyo bali ni maamuzi binafsi ya mtumishi huyo kwa matakwa yake binafsi.
Aliwahakikishia wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo kuwa tukio kama hilo halitajitokeza tena.
Aliwataja watoto ambao walinyofolewa drip kuwa ni Edward Robert (4), mkazi wa kijiji cha Nyamirembe; Kashinje Lukanya (12), mkazi wa Busaka; Iren Nasib (3), mkazi wa Bwanga; Naomi Tumain (5), mkazi wa Kachwamba; Yunis William (3), mkazi wa Kasala; Asteria Siajali (2), mkazi wa Kahumo na Alphonce Makolobelo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Ester Misungwi, Sindikwi Mkubulo na William Masai, waliipongeza hatua ya Waziri Magufuli kuhakikisha mhusika wa tukio hilo anakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hizo.
Juhudi za NIPASHE kumpata muuguzi huyo ili kuzungumzia tukio hilo la aina yake katika fani ya utabibu hazikuzaa matunda jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment