Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma.
Mwenyekiti wa CUF
Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma.
Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na wanachama wa CCM na CUF
mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kigoma kuanza ziara ya siku
mbili ya kichama Mkoani humo.
Na Hassan Hamad OMKR
Tanzania inahitaji
mabadiliko kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa sambamba na kutoa elimu na
huduma bora kwa wakulima ili waweze kuendeleza kilimo chenye tija.
Hayo yameelezwa na
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa
akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya
Kasulu Mkoani Kigoma.
Amesema Tanzania
imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutba inayokubali kuotesha mazao mbali mbali,
lakini bado hakujakuwepo na mikakati imara ya kuendeleza kilimo, jambo ambalo
linapaswa kufanyiwa kazi kwa maslahi ya wananchi.
Prof.
Lipumba amefahamisha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa inayoweza
kufanya vizuri katika kilimo kutokana na kuwepo kwa maziwa na mito ya kudumu
ambayo inaweza kutumika kwa kilimo cha mboga mboga na umwagiliaji, na kusaidia
kukuza kipato cha wakulima.
Sambamba na hilo
Prof. Lipumba amewataka wakulima kutilia mkazo mazao ya nafaka yakiwemo mahindi
na maharage, kutoka na kuongezeka kwa bei ya mazao hayo katika soko la
dunia.
Mwenyekiti huyo wa
CUF Taifa pia amesisitiza haja ya kuwepo kwa mikakati ya makusudi ya kuongeza
ajira kwa vijana ili kuwanusuru kujiingiza katika vitendo viovu.
“Ukosefu wa ajira
unatisha, na ikiwa vijana hawana ajira wanaweza kushawishika kufanya jambo
lolote ambalo linaweza kuliletea madhara Taifa”, alifafanua Prof. Lipumba.
Akizungumzia kuhusu
mchakato wa katiba, Prof. Lipumba ametaka katiba mpya ijayo itamke wazi kuwa
maliasili za Tanzania na mali ya Watanzania na iweke itaratibu ambao Watanzania
wataweza kunufaika na rasilimali hizo.
Amesema iwapo
wananchi watanufaika moja kwa moja na rasilimali zao za nchi wataweza
kuzilinda na kuziendeleza, lakini vyenginevyo rasilimali hizo zinaweza kuleta
maafa badala ya neema kama zilivyo baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria na
Equatorial Guinea.
Kwa mujibu wa Prof.
Lipumba Tanzania ina utajiri wa rasilimali mbali mbali zikiwemo madini, mafuta
na gesi asilia ambapo katika siku za hivi karibuni Kampuni moja ya Norway
iligundua gesi yenye futi za ujazo trilioni 5 katika kisima kimoja pekee,
ambapo jumla inakisiwa kuwepo na gesi trilioni 30 futi za ujazo.
Amesema rasilimaji
zipo nyingi lakini zinahitaji kuwepo na uongozi wenye dira utakaozingatia
mgawanyo wa rasilimali hizo kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema CUF kitasimamia
sera yake ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki
zake za msingi zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.
Amesema tatizo kubwa la
Tanzania ni mipango duni ya kiuchumi, na kuwashauri wananchi kukiunga mkono
chama hicho ili kiweze kurekebisha kasoro zilizopo na kuimarisha uchumi wa
nchi.
Kabla ya mkutano huo,
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliupongeza
uongozi wa Mkoa huo kutokana na ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa vyama vya
siasa, na kwamba kufanya hivyo ni kuonesha ukomavu wa kisiasa.
Katika uwanja wa ndege wa
Kigoma Maalim Seif alipokelewa na viongozi wa mkoa huo pamoja na wafuasi wa CUF
na Chama Cha Mapinduzi.
Mkutano huo ni sehemu ya
Operesheni mchakamchaka hadi 2015 iliyozinduliwa na chama hicho kwa ajili ya
kutembelea mikoa mbali mbali ya Tanzania kutoa uelewa kwa wananchi ili hatimaye
waweze kujiunga na chama hicho.
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment