WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 21, 2012

Utafiti: Umaarufu Wa JK Waporomoka


 

KUONGEZEKA kwa matukio ya rushwa nchini kumesababisha umaarufu wa Rais Jakaya Kikwete kushuka kwa asilimia 20 katika miaka minne iliyopita, utafiti mpya unaonyesha.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA) kati ya Mei na Juni 2012 unaonyesha kwamba kiwango cha Rais Kikwete kukubalika kimeshuka kutoka asilimia 90 mwaka 2008 hadi asilimia 71 mwaka huu.
Pia, mwaka huu watu saba kati ya kumi walioshiriki katika utafiti huo waliihusisha ofisi ya Rais kwa rushwa na kwamba hali hiyo ni tofauti na mwaka  2008 ambapo walikuwa  watu watano kati ya 10, utafiti huo ulieleza.
Rais Kikwete ambaye hivi karibuni alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CCM, wakati akizungumza na mamia ya makada wa chama hicho Dar es Salaam alikiri kwamba watu wengi wamepoteza imani na  chama hicho kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi.
Katika maelezo yake, Kikwete alisema kuwa ni lazima kurejesha imani ya wananchi kwa chama hicho na kufanya uchunguzi ili kujua wapi kilipokosea.

Utafiti huo ujulikanao kama Afrobarometer Tanzania, uliotolewa jana Dar es Salaam pia umeonyesha kuwa asilimia 90 ya watu waliohojiwa hawakuridhika na utendaji kazi wa Rais kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Utafiti huo ni mfululizo wa tafiti linganishi zinazohusisha tabia ya jamii unaofanywa katika nchi 35 barani Afrika kati ya mwaka 2011 hadi 2013.

Afrobarometer  ni utafiti unaoonyesha  mitazamo ya umma juu ya demokrasia na mbadala wake, tathmini ya ubora wa utawala na utendaji wa kiuchumi.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Huduma ya Utafiti wa Repoa, Jamal Msami  alisema kwa wastani mwaka 2012 watu wengi zaidi waliishutumu Serikali kushindwa kuimarisha uchumi wa nchi kuliko ilivyokuwa mwaka 2008.

Alisema kuwa katika utafiti huo watu wengi walizungumzia kuporomoka kwa uchumi wa nchi na uhaba wa vyakula vya aina mbalimbali pamoja na kuwapo kiwango cha utoaji wa huduma kwa jamii kutoridhisha.

“Kwa ujumla, tafiti inatoa taswira hasi kwa utendaji wa Serikali katika nyanja zote kwa kipindi hicho cha miaka minne,” alisema.

Licha ya tathmini ya utendaji mbaya wa Serikali, Watanzania bado wana matumaini ya kuwa Serikali itaweza kutatua mambo muhimu katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema kuwa Watanzania walipoulizwa juu ya uwezekano wa Serikali kutatua matatizo muhimu zaidi, asilimia 66 ya waliohojiwa walionyesha kuwa na imani kwamba inaweza, kiwango ambacho ni tofauti na cha 2008 ambapo mtu mmoja kati ya kumi ndio alionyesha kutokuwa na imani na jambo hilo.
Katika ngazi ya kitaifa, asilimia 8 ya watu wazima walisema kuwa watoto wao walipewa chakula wakiwa shuleni, katika mpango unaoendelea nchini wa chakula bure shuleni.

Alisema  katika utafiti huo asilimia 66 ya watu wazima waliulalamikia ubora wa ufundishaji wa wanafunzi katika shule za msingi, kwamba utafiti wa mwaka huu unatoa misingi muhimu na ya kutosha kwa ajili kufikiri upya mikakati ya utendaji katika kukuza ubora wa ufundishaji.

Alisema kuwa tafiti za mwaka 2008 na mwaka huu zinaonyesha hali halisi ya maisha waliyonayo Watanzania.

”Si jambo la kushangaza kama karibu theluthi mbili (asilimia 64) ya Watanzania watu wazima hawakuwa na kazi ya kuwawezesha  kulipwa mshahara yao, ikilinganishwa na asilimia 56 mwaka ya  2008,” aliongeza.
Alisema asilimia 53 na 54 ya watu waliohojiwa katika kipindi cha utafiti huo walisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, tangu 2008 waliwahi kula mlo mmoja tu kwa siku.
Baadaye akizungumza na waandishi wa habari mara baada kutangazwa kwa matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe alisema licha ya utafiti huo kuonyesha kwamba imani ya umma imepungua kwa Rais, lakini baadhi yao wana matumaini kwamba hali itatengemaa siku zijazo.
Profesa Wangwe alisema kupungua kwa imani ya wananchi kumetokana na matatizo ya kiuchumi licha ya taasisi za fedha za kimataifa kusema kwamba Tanzania inafanya vizuri katika eneo hilo.
“Wananchi wanasema bado uchumi wetu ni tatizo kwa sababu wanadai kuwa maisha bado ni magumu na duni na  hakuna kitu kinachobadilika,” alisema Profesa Wangwe.

 CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment