Mwalimu
Nyerere akichanganya mchanga kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa
taifa jipya la Tanzania, Aprili 26, 1964
BISHOP
J. HILUKA
Dar
es Salaam
MUUNGANO
wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya
la Tanzania ulizaliwa Aprili 26, 1964 na hivyo Alhamisi ya Aprili 26
mwaka huu muungano wetu umetimiza miaka 48. Nilishuhudia sherehe za Muungano
kupitia televisheni, na hali imeendelea kubainisha kuwa tunalazimisha
kusherehekea huku kukiwa na manung’uniko kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya
viongozi wa kisiasa wakionekana ama kuupinga mfumo wa Muungano au kutoutaka
kabisa Muungano huu.
Wazanzibar
wanalalamika wamemezwa na Tanzania Bara, Watanzania Bara (Watanganyika)
wanalalamika kuwa wameipoteza Tanganyika yao na wananyonywa
kupitia mwamvuli wa Muungano wa Tanzania, lakini wachache katika serikali
yetu wameapa kuwa wataulinda muungano huu kwa nguvu zote!
Ni
ajabu sana kuwa kila upande unalalamika! Inashangaza sanakatika
vuta nikuvute hii eti kuna kundi linasema litaulinda Muungano kwa nguvu zote!
Katika kuulinda huu Muungano kumekuwepo tafsiri ambayo inahitaji ufafanuzi;
kuulinda kwa nguvu zote maana yake nini?
Wafuatiliaji
wa masuala ya siasa wanaiona kauli ya kuulinda ni kuzuia watu wasiujadili.
Kutoruhusu uvunjike. Huku wengine (nikiwemo mimi) tukijiuliza, ya nini kuwa na
muungano bila kuujadili? Inafaa nini kuishi kwa mazoea? Na kwa faida ya nani?
Huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema kuwa jambo pekee
wanalopaswa wananchi kujadili kuhusu Muungano ni kuuboresha! Inawezekanaje watu
waboreshe kitu ambacho hawajakubaliana umuhimu wake?
Rais
amesahau kuwa Watanzania walio wengi leo hii ni vijana waliozaliwa baada ya
Muungano. Ingawa wamesoma habari za Muungano katika vitabu vya historia lakini
hawauelewi vyema, ndiyo maana hata shamrashamra za serikali na wananchi juu ya
Muungano zimeshuka siku hizi. Tunachoshuhudia ni wananfunzi kulazimishwa kwenda
kwenye sherehe hizi bila ridhaa yao.
Kama vijana
hawaujui vyema Muungano wetu, kwa nini sasa wanataka kunyimwa fursa ya
kuujadili? Fursa imejitokeza lakini viongozi wanatuzuia? Hivi kweli wanautakia
mema Muungano huu?
Hapa
sijui kama kweli kuna nia ya dhati ya kuuboresha. Kutoujadili?
Kutorusu uvunjike? Hivi tunayafanya haya kwa faida ya nani? Wananchi ambao
ndiyo wenye nchi yao wanataka kuandika upya historia yao tena
kwa nyakati zao
lakini
viongozi wanataka kuwaenzi waasisi kinafiki! Nani mwenye nchi? Wananchi au
viongozi?
Siandiki
haya kwa kuwa labda siutaki Muungano, hasha! Nautakia mema ndiyo maana napenda
tukae mezani kuujadili, tuangalie kasoro zote zilizopo na kuzirekebisha ili
hatimaye tuingie kwenye Muungano uliopata ridhaa za wananchi wa pande zote. Ni
kufilisika kimawazo kudhani kwamba anayehoji Muungano ana nia ya kuuvunja.
Badala yake, ni kuchochea mjadala mpana na wa kina kuhusu umuhimu wa Muungano.
Hatutakuwa na muungano imara kama viongozi wataendelea kutulazimisha
bila kusikiliza hoja na manung’uniko yetu.
Hata
hivyo, kuvunjika kwa muungano si jambo la ajabu, kamahatutaruhusu mijadala
ya wazi tunaweza kuishia walikoishia wengine. Tusidhani kuwa sisi tuna akili
zaidi au tumebarikiwa zaidi ya wengine. Tuna kipi cha ajabu? Kumbukumbu zangu
zinanieleza kuwa mojawapo ya waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia
iliyotengana na Eritrea, muungano wa Senegambia ulishindikana kwa kuwa wananchi
hawakushiriki na hatimaye walitengana na kubaki nchi mbili za Senegal na
Gambia, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo sasa ni nchi mbili za Rwanda na
Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.
Inashangaza sana kuona
kuwa kundi dogo linataka kubinafsisha mawazo ya walio wengi, vijana na wasomi
wa taifa hili wanashindwa kuhoji mambo kwa mapana yake. Tunapaswa tujiulize,
hivi kwa nini tuliungana? Huu si wakati tena wa kuleta sababu dhaifu eti
tunaleta umoja au eti kwa vile sisi ni ndugu. Mbona hatuungani na Wakenya
wakati nchi zote hizi zina undugu?
Kwa
nini hatupewi nafasi ya kuhoji nini sababu hasa ya muungano huu? Wenye majibu
wote kwa sasa hawapo na yaliyobaki ni majibu ya kufikirika tu, nafasi ya uongo
ni kubwa. Bila majibu haya, ni vigumu ni bora watu wakajadili na wakaja na aina
ya muungano wanaoutaka.
Hali
ya mashaka inaugubika Muungano huu, inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa
kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano
kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar,
Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano;
Bara na Visiwani.
Habari
zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na
watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki
yoyote ya mustakabali wa nchi yao.
Ndiyo
maana nafikiri kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano
ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa
tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo
siku mauti itatuumbua.
Ukiuangalia
Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzurisana wa maelewano kwa
watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa
hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao
tunaweza kushindwa kuuzima na hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.
Kwa
kuwa tupo katika kipindi cha kuandika Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka
kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe
mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.
Hofu
za viongozi wetu zinatoka wapi? Mbona Watanzania wengi kutoka pande zote
zinazohusika na Muungano, wanaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano
kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.
Kero
hizi ni pamoja na mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa
serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo
wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa
kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka
kuuboresha Muungano. Muundo wa Muungano, hatakama chama tawala kimekuwa
kikidai kuwa sera yake ni ya serikali mbili, linatakiwa liwe jambo
litakaloamliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.
Ukiangalia
kwa makini utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa
na ulikuwa wa mambo 11 kamaambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo
wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya
kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa
kinyemela.
Hata
hili la ushirikiano wa kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya
mambo ya Muungano na ndiyo maana Zanzibarwaliamua kujiunga na Jumuiya ya
Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali
iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.
Kero
nyingine ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa
Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka
upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili
limeondolewa bila ya kura ya maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote
Miaka
ya hivi karibuni zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibarkutaka masuala
ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya
Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia ikilalamikiwa. Haya yanahitaji
muungano kuhojiwa kwa uwazi ili majibu ytaolewe. Kama kutakosekana
majibu ya maana, itakuwa ni kazi bure kutumia maneno makali kwani wananchi
wataukataa.
No comments:
Post a Comment