Charles
Ekerege, Mkurugenzi Mkuu wa TBS
Machinjio
ya ng'ombe
BISHOP
HILUKA
Dar
es Salaam
MAJUZI nilikutana na dokezo moja kutoka
kwa Profesa Mbele alilolitoa kwenye blogu yake, kuwa ufisadi ndiyo dini
inayoenea kwa kasi nchini Tanzania. Kwangu mimi hii ilikuwa ni habari
kubwa mno. Japo ilikuwa ni kama dokezo tu (fupi mno) la kawaida,
lakini ilinifanya kufikiria kwa kina huku nikilinganisha na hiki kinachoendelea
kutokea nchini mwetu. Kwa kifupi nakubaliana na Profesa Mbele kuhusu hilo.
Profesa
Mbele aliandika hivi: “Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini
inayoenea kwa kasi kuliko zoteTanzania, Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu
ana mtazamo wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni
za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia takwimu,
wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi kuwa dini
yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.
“Kwa
mtazamo wangu, dini inayoenea kwa kasi kuliko zoteTanzania ni ufisadi na
ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo unaendelea kushamiri kiasi kwamba
unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za dini mbalimbali. Hebu
tutafakari hilo.”
Ni
maneno machache lakini yaliyobeba ujumbe mkubwa mno na unaweza kuyaelezea kwa
kurasa zaidi ya elfu moja. Binafsi nadhani kuenea kwa dini (ufisadi) hii
kumesababishwa na nchi hii kuitupa misingi iliyoongozwa na Azimio la Arusha,
kufumbia macho vitendo vya rushwa na kukubali wafanyabiashara ambao wengi wao
historia zao binafsi katika suala zima la uadilifu zinafahamika waziwazi ndani
ya jamii na zimekuwa zinatiliwa shaka sanakupewa nafasi kwenye vyama vya
siasa, hasa chama tawala.
Wafanyabiashara
hawa wakubwa wenye kashfa mbalimbali za kuhujumu Taifa wamekuwa wakijitokeza
kugombania nafasi mbalimbali za kisiasa, wanapokosa huwa wanaamua kupandikiza
watu wao katika uongozi ili kuhakikisha dili zao na biashara zao zinakaa sawa.
Kinyume
na ilivyokuwa katika awamu ya kwanza na kipindi cha kwanza (1985-90) cha awamu
ya pili ya uongozi wa nchi hii, uongozi wa Tanzania kwa sasa si
dhamana tena kamatulivyokuwa tukifundishwa shuleni kwamba 'cheo ni
dhamana'. Uongozi sasa hivi umegeuka kuwa njia ya kumfanya mtu mambo yake
yamnyookee, uongozi umekuwa biashara 'bab kubwa' isiyo na hasara. Zamani
uongozi ulikuwa ni mzigo lakini siku hizi uongozi ni ‘kuula’ kwa maana ya dhiki
kutoweka kabisa.
Kuenea
kwa dini hii ni matokeo ya wimbi la wafanyabiashara kujiingiza kwenye siasa na
kuviteka vyama huku wakipandikiza watu wao kwenye uongozi. Inashangaa hata pale
wataalamu wa fani tofauti wanapoacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa. Hebu
fikiria maprofesa, madaktari, wahandisi, na wataalamu wa fani mbalimbali
wanaacha kazi zao walizosomea na kupigania kwenda kusinzia bungeni au kwenye
mikutano ya halmashauri!
Wafanyabiashara
hawa wana nguvu kubwa sana ndani ya vyama na hata serikalini, ndiyo
maana sasa tunashuhudia wakisamehewa kodi kila mwaka huku ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 aliyoitoa hivi
karibuni ikionesha kwamba katika kipindi hicho misamaha ilifikia shilingi
trilioni 1.2 (asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali).
Kibaya
zaidi, mawaziri na wabunge wetu ni miongoni mwa vigogo wanaojinufaisha na
Sheria ya Msamaha wa Kodi kinyume cha taratibu. Orodha ya majina ya watu
waliosamahewa kodi na Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 inaonesha majina
ya baadhi ya mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali wakiwa
wamenufaika na misamaha hiyo.
Viongozi hawa
wameshiriki katika kuidhinisha shilingi bilioni 31 kununua bidhaa kwa matumizi
ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, shilingi bilioni 8 kutumika bila kufuata
utaratibu maalumu na shilingi milioni 143 kutumiwa na serikali kulipa mishahara
kwa wafanyakazi hewa, watoro na waliostaafu! Yaliyomo kwenye ripoti hiyo
yanasikitisha na kutisha sana.
Matokeo ya
kushamiri kwa dini hii yamesababisha wataalamu wa wanyama, afisa afya na
watendaji wa majinchio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam kuruhusu kuletwa
utumbo na nyama iliyooza na kuuzwa kwa wananchi, kitendo kilichovuka hata
mipaka ya ubinadamu!
Ni nani
atabisha kwamba dini hii haina nguvu na haijaenea nchini? Hata kama nchi
inanuka rushwa na ufisadi, lakini ndiyo iwe kwa kiwango cha namna hii? Kwa hali
ya kawaida, haihitaji kuwa msomi sana kubaini kuwa bidhaa ya kuoza kama ile
italeta madhara makubwa sana kwa watu na pengine hata ndugu wa karibu wa
wahusika.
Hii pia haina
tofauti na ile habari Shirika la Viwango Nchini (TBS) kuruhusu bidhaa feki
zitumike nchini. Tukubali au tukatae, hii ni dini inayoenea kwa kasi kutokana
na kukumbatia rushwa, kuruhusu wafanyabiashara watawale mfumo wa uongozi kwa
kupandikiza watu wao, na kutochukuliwa hatua thabiti kwa wanaobainika kufanya
‘madudu’.
Kushamiri kwa
dini hii kumesababisha pia kuwapo habari kuwa vibali bandia 480 vimetolewa na
kuidhinishwa na kigogo mmoja wa Idara ya uhamiaji mkoani Kilimanjaro. Vibali
hivyo vimeisababishia Serikali hasara ya Sh 231 milioni. Serikali pia ilipata
hasara ya Sh 86 milioni kutokana na vibali vingine bandia 84 vilivyokamatwa
mwaka jana katika kiwanda kimoja wilayani Mwanga, huku kinara mkuu akidaiwa
kuwa uraiani.
Hayo na mengine
mengi yanatufanya tuamini kuwa sasa hii ndiyo dini iliyoshamiri nchini. Ni kipi
kitatufanya tusiamini kuwa dini hii ndiyo inayoenea kwa kasi nchini?
Imewekwa
na Mkereketwa
No comments:
Post a Comment