Mzee Makamba Atikisa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana kimenusuru Rais Jakaya Kikwete kupigiwa kura za maruhani, baada ya kubadili taratibu za uchaguzi, huku Katibu Mkuu wake wa zamani, Yusuph Makamba akiwapiga vijembe waliokuwa wamepanga mbinu hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa CCM, Spika wa Bunge, Anne Makinda, muda mfupi kabla wajumbe hawajaanza kupiga kura alitangaza utaratibu mpya kwamba kila mkoa utapiga kura katika sanduku lake.
“Kila mkoa utakuwa na sanduku lake la kupigia kura,” alisema Makinda na bila kufafanua, hali iliyowafanya baadhi ya wajumbe kushangaa uratatibu huo kwani kwa kawaida chaguzi za kumpata mwenyekiti na makamu wake hufanyika kwa wajumbe kupiga kura kwa ujumla, bila kufuata utaratibu wa mikoa.
Uamuzi huo ulikuja wakati kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya wajumbe, walikuwa wamepanga kumpigia kura za maruhani, mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.
Dalili kuwa CCM kiligundua njama za hujuma hiyo, zilionekana mapema wakati Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba alipokuwa akimwombea kura Rais Kikwete.
Makamba na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai waliteuliwa na NEC ya CCM kumwombea kura Rais Kikwete kwa wajumbe wa mkutano huo.
Makamba aliwataka wajumbe wote kumpigia kura za ndiyo Rais Kikwete kwani wakipiga kura za maruhani wanataka mwenyekiti awe nani.
“Mpigie kura za ndiyo mwenyekiti wetu Kikwete, wale ambao mnataka kupiga kura za maruhani mnataka mwenyekiti awe nani?” alihoji Makamba, huku wajumbe wakimshagilia. Viongozi waliotarajiwa kuchaguliwa ni Mwenyekiti wa CCM na makamu wake wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Waliopendekezwa na Halmashauri Kuu kuwania nafasi hizo ni Rais Kikwete kwa nafasi ya mwenyekiti, wakati Philip Mangula na Dk Ali Mohamed Shein walipendekezwa kwa nafasi za umakamu wa Bara na Visiwani sawia. Hadi tunakwenda mitamboni, matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa bado yanasubiriwa.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa CCM, katika uchaguzi huu kuziba mwanya wa kufanyika hujuma, baada ya Jumapili kubadilisha ghafla ratiba yake ya uchaguzi na kuanza na uchaguzi wa wajumbe wa Nec, badala ya uchaguzi huo kufanyika jana.
Hali hiyo iliwafanya wagombea na wapambe wao kushindwa kupata muda mrefu wa kufanya kampeni ikiwamo kutoa rushwa.
Makamba atikisa
Akitumia aya zilizopo katika vitabu vitakatibu vya Biblia na Koran, Makamba aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Rais Kikwete ana wito wa Mungu.
“Tembo hashindwi kubeba mikonga yake miwili, sasa wanaosema kuwa tupige kura za maruhani wanataka awe nani, nasema washindwe kabisa kwa jina la Yesu,” alisema Makamba huku akishangiliwa kwa nguvu na wajumbe wa mkutano na baadhi yao waliinuka kwenda kumtuza fedha.
Wakati anatuzwa alikatisha hotuba yake kwa muda, hali ambayo iliwafanya wajumbe kulipuka kwa kicheko akiwamo Rais Kikwete, huku yeye mwenyewe akisema, “Ninakula sehemu yangu kama watu wa dini wanavyokula sehemu yao.”
Mbali na hilo, aliwakumbusha machungu baadhi ya wanaCCM waliogombea nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kwa kusema wako mbali na watu na ndiyo baadhi yao waliadhibiwa kwa kunyimwa kura.
Makamba alisema kuwa Rais Kikwete yupo karibu na watu na kwamba muda wote amekuwa akitekeleza Ilani ya chama hicho, hivyo apewe nafasi nyingine ya kukiongoza chama hicho.
“Wengine wanapiga kelele kuwa tupunguze kura za mwenyekiti, lakini wanasahau kuwa wao wana kazi moja, lakini kazi hizo zinawashinda, sasa kelele ya nini ndugu zangu, mpeni Jakaya mtu wa watu,” alisema.
Alisema CCM imesajili wachezaji wazuri ambao ni watendaji waliopatikana katika chaguzi mbalimbali za chama hicho na kwamba sasa wanatafuta kocha wa timu ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.
Makamba aliwasuta baadhi ya viongozi wa mikoa akisema kama asingekuwa Rais Kikwete kuwakumbuka hivi sasa hawangepata uongozi, hivyo wanapaswa kuonyesha shukrani kwa kuisaidia CCM kutekeleza Ilani yake.
Aliongeza kuwa wako watu ambao wamekuwa wakijitafutia umaarufu mkubwa ikiwamo kutaka uongozi wa nafasi ya urais, lakini hawajipimi kama wanakubalika au la.
Alisema watu wana namna hiyo wanaweza kufika mahali wakajikuta wanapigiwa kura na watu wachache sana ikiwamo kura zao na wake zao kutokana na kuamua kufanya mambo bila ya kufanya tathmni.
Makamba alisema kiongozi ili upendwe na wananchi lazima ufanye kazi nzuri, kama aliyoifanya Rais Kikwete katika uongozi wake katika CCM.
Akiwa ameliteka jukwaa la wajumbe huku akishangiliwa kwa nguvu huku akiendelea kutuzwa, Makamba aliwatolea mfano baadhi ya wenyeviti na kueleza namna wengine walivyolia wakati wakitafuta nafasi hizo.
“Mfano ndugu yangu Kaborou (Walid, Mwenyekiti wa CCM) kule Kigoma ulikuwa ukinitukana, lakini leo upo hapa, Shekifu (Henry, Mwenyekiti Mkoa wa Tanga) kule Tanga ulihangaika sana, Madabida (Ramadhan, Mwenyekiti wa Mkoa Dar es Salaam) ulikuwa ukihaha kweli, lakini wewe Msukuma Mgeja, (Hamis, Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga) ulilia machozi kabisa, kwa nini leo mwenzenu anapotafuta nafasi hiyo mnakuwa na nongwa,” alisema.
Hata hivyo, hakufafanua jinsi viongozi hao wanavyohusika katika mchakato wa uchaguzi huo.
Kabla ya kuingia CCM, Kaborou alikuwa Mbunge wa Chadema wa Kigoma Mjini, huku Mgeja, Shekifu na Madabida walikabiliwa na upinzani mkubwa wakati wa uchaguzi wa nafasi zao.
Mstaafu huyo alitumia nafasi hiyo kuwatupia kombora baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete kuwa wamelewa madaraka kiasi kwamba hata wakipigiwa simu huwa hawapokei na badala yake huwapa wake zao simu hizo, tofauti na Kikwete ambaye kupokea simu wakati wowote.
Hata hivyo, Makamba mbali ya kumnadi Kikwete alitumia jukwaa hilo kutoa dukuduku lake kuwa kilichomgarimu wakati akiwa ndani ya chama hicho ni kutokana na kusema ukweli.
Alisema kuwa amekuwa akisimamia katika ukweli na haki wakati wote jambo ambalo halikukubalika na watu wengi ndani ya chama.
SOURCE: mwananchi
No comments:
Post a Comment