Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar
Dkt Ali Mohammed Shein ameendelea kukemea vikali vikundi vya watu
vilivyojificha chini ya mwamvuli wa kidini kufanya vurugu na kutishia amani
kwamba havitavumiliwa.
Amesema haiwezekani
kuwaruhusu watu wachache kuwafanyia vurugu wengi wakati kila mtu ana haki ya
kuheshimiwa na kuishi kwa salama katika jamii.
Akizungumza kwenye Mkutano
wa hadhara Kibanda maiti mjini Zanzibar, Dk Sheinamesema wananchi wa Tanzania
wana uhuru wa kuamini dini waitakayo bila ya kubughudhiwa wala
kuingiliwa katika ibada zao lakini panapoingia fujo na vurugu Serikali haiwezi
kukaa kimya.
Amesema hakuna mtu
anayekatazwa kuabudu lakini kufanyafujo na kuharibu mali za watu
hakustahamiliki na kuongeza kuwa vikosi vya ulinzi vitaendelea na kazi yao kwa
mujibu wa sheria kuona vurugu na fujo hazitokei tena.
Dkt. Shein ameongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuilinda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa na kuheshimu maridhianao ya kisiasa yaliyopo ili kuleta maendeleo kwa
Wananchi wote.
Amesema Serikali ambayo
anaiongoza itaendelea kuwalinda na kuwaletea maendeleo wananchi wote bila
kujali tofauti zao kama ambavyo sheria za nchi zinavyoelekeza.
Ameongeza kuwa yeye ni
Kiongozi Jasiri ambaye haongozi kwa kubahatisha bali hutumia Katiba ya nchi
sambamba na kanuni nyingine zinazosaidia kuendesha nchi na kuwaletea wananchi
maendeleo.
Kuhusu kuimarisha chama
cha CCM Makamu Mwenekiti huyo amewataka wanaCCM kushikamana katika kuimarisha
chama chao ikiwa ni pamoja na kuziimarisha Maskani za Chama hicho ambazo ndio
nguzo imara za ushindi wa Chama.
Aidha amewataka WanaCCM
kutembea kifua mbele kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake
na kwamba uwezekano wa CCM kuendelea kuongoza dola mwaka 2015 ni mkubwa.
Akizungumzia kuhusu
Muungano Dkt. Shein amesema ulitokana na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwaka
1964 hivyo akiwa Rais ataendelea kuulinda chini ya Mfumo uliopo wa Serikali
mbili.
Aidha amewataka wanaCCM
katika mchakato uliopo wa Katiba mpya kutoogopa kutoa maoni yao kwa Tume ya
Katiba ambapo pia aliwakumbusha WanaCCM kuwa Sera ya Chama katika muungano ni
Serikali mbili.
Awali Akitoa salamu zake
Katibu Mkuu wa CCM Abrahman Omar Kinana amemuhakikishia Dkt Shein ushirikinao
wa kutosha wa kukiimarisha Chama hicho nakwamba chini ya uongozi wake CCM Bara
na Zanzibar itakuwa inafanya kazi kwa mashirikiano makubwa.
Mapema WanaCCM wa mikoa
minne kichama ya Unguja walitoa salamu zao za pongezi na kumuomba Makamu
Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar kutowafumbia macho watu ambao wanahatarisha
amani na utulivu uliopo nchini.
Mkutano huo wa CCM wa
kuwashukuru wanachama umekuja kufuatia ushindi wa asilimia 100 ambao Rais Shein
aliupata kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mweyekiti wa Chama hicho kwa upande wa
Zanzibar.
IMETOLEWA NA IDARA YA
HABARI MAELEZO ZANZIBAR 17/11/2012
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment