Utamaduni wa kujisomea huanza tangu
utotoni
kama anavyoonekana mtoto Magdalena
Hiluka
BISHOP HILUKA
Dar es Salaam
KUSOMA vitabu ni jambo zuri na
muhimu sana katika maisha ya binadamu kwani mambo mengi muhimu katika
dunia hii yapo katika maandishi, iwe kwenye vitabu au mitandao ya jamii,
yakiwemo maneno ya Mungu kwa wale wenye imani za kiroho. Yote haya utayakuta
katika maandishi, ndani ya vitabu. Kama huna utamaduni wa kujisomea
vitabu au kuperuzi katika mitandao ya intaneti, basi usitegemee kupata habari
nzuri, kuelimika zaidi na kujua mengi yanayotokea duniani.
Wiki chache zilizopita katika
kuperuzi kwangu baadhi ya machapisho nikiwa na lengo la kujaribu kuongeza
maarifa, nilikutana na makala moja kuhusu usomaji wa vitabu ambao Watanzania
tumeuacha siku hizi, ingawa jambo hili limekuwa likiandikwa sana lakini
nikiri tu kuwa makala hii ilinivutia sana, ndiyo maana leo nimeamua kuja
na hoja hii.
Makala hii iliandikwa na mmoja wa
waandishi wa vitabu wakongwe, Profesa Joseph Mbele, Mtanzania anayeishi Northfield,Minnesota,
nchini Marekani. Profesa huyo aliandika akihimiza wazazi kupenda kuwasomea
watoto wao vitabu ili kuwavutia kupenda kusoma, akifananisha na enzi zile za
mababu na mabibi zetu, ambapo ilikuwa ni kawaida kwa wazee hao kukaa na watoto
au wajukuu jioni na kuwasimulia hadithi.
Utamaduni huu ulikuwa ni sehemu ya
maisha, na ingawa watoto walichukulia kama kitu cha kawaida lakini
ilikuwa ni sehemu ya elimu waliyopewa hao watoto. Hapakuwa na shule tulizonazo
leo, wala vitabu, lakini wazee walikuwa walimu bora, waliotumia mbinu
mbalimbali, kama hizi hadithi, katika kuwaelimisha watoto.
Lakini siku hizi, japo tuna vitabu
na shule karibu kila mtaa, lakini tunashindwa kutumia fursa ya kutumia vitabu
kuendeleza elimu ya watoto! Sijui tatizo ni nini?
Hivi tatizo ni nini hata pale
tunapokosa uwezo wa kuwasimulia hadithi kwa mtindo wa mababu na mabibi zetu,
tunayo fursa ya kuwasomea vitabu, lakini tunashindwa kuitumia na kujikuta
tukiuendeleza ule msamiati ambao binafsi umekuwa ukiniudhisana, wa “Watanzania
hatuna utamaduni wa kusoma vitabu”.
Katika nchi za wenzetu, kama nchi
aliyoitolea mfano Profesa Mbele ya Marekani, wamekuwa wanaendeleza utamaduni
huu kwa kuwasomea watoto hadithi za vitabuni. Watoto wa Kimarekani wanategemea
mzazi awasomee vitabu. Ni kawaida kwa mzazi kumsomea mtoto kitabu kabla
hajalala.
Wamarekani wanajali sana utamaduni
wa kusoma vitabu. Utawaona wazee, watu wazima, wake kwa waume, vijana, na
watoto katika maduka ya vitabu. Utawaona wazazi wakiwa wanakuja na watoto wao.
Utawasikia wakiongea na watoto kuhusu vitabu, wakiwasomea watoto vitabu,
wakijibu maswali ya watoto, na kadhalika.
Hali hii ni tofauti sana na iliyopo hapa nchini mwetu Tanzania.
Leo ni Ijumaa. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo
anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake
kwenye duka la vitabu?
Imewekwa na Mkereketwa
No comments:
Post a Comment