Balozi Seif Idd Aahidi Kushirikiana Na Wananchi Kutatua Changamoto
Wawakilishi wawili wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Stara Ali na Bibi Halima Abushiri wakifafanua baadhi ya kero zinazowakibi katika Kituo chao mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Alik Iddi wakati akisikiliza kero na changamoto za wananchi wa Jimbo lake.
Ndugu Charles Bernados wa Kitope akielezea changamoto zinazomkabili baada ya kupata ajali ya moto katika makazi yake mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ikiwa ni utaratibu aliojipangia wa kukutana na wananchi wake.
Ndugu Charles Bernados akionekana mwenye majonzi baada ya kupata ajali ya moto uliopelekea kuungua mkono wake na mali, Fedha na vitu vyake kuteketea kwa moto huo.
Wananchi wa shehia tofauti zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope wamepata fursa ya kukutana na Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi katika utaratibu aliojipanga Mbunge huyo wa kukutana nao ili kusikiliza Kero na changamoto zinazowakabili katika harakati zao za kila siku.
Mkutano wa Mbunge huyo ulifanyika katika Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kijiji cha Kitope ikiwa ni miongoni mwa Ofisi kadhaa zilizojengwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo maalum la kutoa nafasi kwa wananchi kukutana na Waheshimiwa Wabunge wao.
Wananchi wasiopungua ishirini na Tatu walipata fursa hiyo ya kukutana na Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakielezea na kushauri masuala tofauti yakiwemo yale ya Jamii, Binafsi, Maendeleo na hata ya Kiuchumi.
Miongoni mwa masuala hayo muhimu yaliyowasilishwa na Wananchi hao kwa Balozi Seif ni changamoto za Vifaa vya matumizi kwa baadhi ya Majengo ya huduma za Umma pamoja na kutokamilika kwa wakati kwa baadhi ya miradi na majengo hayo.
Wawakilishi wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Stara Ali na Bibi Halima Abushiri wamesema ubovu wa Uzio na ukosefu wa Tanuri la kuchomea Taka taka katika Kituo hicho, imekuwa ni baadhi ya changamoto zinazo wakosesha utulivu wa kutekeleza vyema majukumu yao.
Wamesema upo muhumi wa kuzingatiwa kwa haraka masuala hayo kwa lengo la kuepuka uchimbaji ovyo wa mashimo ya kuhifadhia taka ili kulinda mazingira pamoja na kuepuka kutoa mwanya kwa baadhi ya watu wenye dhamira mbaya ya kutaka kuhujumu Kituo hicho.
Akipata wasaa wa kufafanua pamoja na kuzitafutia mbinu baaadhi ya kero na changamoto zinazowakabili Wananchi hao wa Jimbo la Kitope, Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza Wananchi hao kuwa na azimio Maalum la kuhakikisha wanakamilisha Majengo yao ya Maendeleo.
Balozi Seif amesema si vyema kwa Wananchi kuendelea kuanzisha utitiri wa Miradi ya maendeleo ndani ya maeneo yao wakati uwezo wa kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati unashindikana kutokana na ukosefu wa msukumo wa uwezeshaji.
Akizungumzia Ujenzi wa Majengo ya Umma yanayosimamiwa na Halmashauri za Wilaya Balozi Seif alilaumu baadhi ya Viongozi wa Halmashauri hizo kwa kushindwa kusimamia vyema Miradi ya Majengo hayo.
Balozi Seif amesema upo ushahidi wa majengo mengi ya Wananchi yanayosimamiwa na Halmashauri hizo ambayo hayako katika kiwango kinachostahili Kitaalamu.
Kuhusu Ukosefu wa Huduma ya Umeme katika Kijiji cha Mgambo Balozi Seif amewataka Wananchi hao kuwa na subra, wakati jitihada za Uongozi wa Jimbo hilo zikiendelea kwa kuwasiliana na Uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar katika njia ya kulitafutia Ufumbuzi Tatizo hilo la muda mrefu.
Source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment