Asema wamepokea malalamiko mengi mno
Watawafanya kama wale 31 wa mwaka 2000
Watawafanya kama wale 31 wa mwaka 2000
Amesema chama kimekwisha kupokea malalamiko mengi ya wanachama wake kuhusu rushwa ilivyotawala kwenye uchaguzi na kwamba kwa sasa wanayachambua.
Akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mangula alisema chama hicho hakitamwonea huruma mshindi yeyote aliyepata nafasi ya uongozi kwa njia ya rushwa katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni.
“Tumepokea malalamiko mengi sana. Hivi sasa yanaendelea kuchambuliwa; uchambuzi ukimalizika tutatuma timu ya kwenda kuona hali halisi ambayo italeta ripoti kwenye kamati ndogo ya maadili ambayo mimi ni Mwenyekiti wake,” alisema.
Alisema suala la rushwa ndani ya chama hicho halihitaji hata nguvu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), bali ni ‘political management’ (utawala wa kisiasa) kumaliza tatizo hilo, kwa kuwa siyo jinai.
Mangula alisema: “Kwa hiyo timu yetu itakwenda kuangalia haya malalamiko ni ya kweli? Nani alifanya nini. Hatupeleki timu moja, baada kukabidhiwa na kamati yangu kupitia ripoti, tunaipelekea Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-Nec), ambayo itafanya maamuzi.”
Alisema ikithibitika kuna mtu alishinda kwa rushwa, matokeo yatatenguliwa na uchaguzi kurudiwa hata kama ni washindi wa nafasi za ujumbe wa Nec.
“Kama mtu anajijua aliingia kwa rushwa atanyang’anywa ushindi, yaani matokeo yatafutwa na uchaguzi utarudiwa. Na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni zetu za uchaguzi,” alisema.
Kuhusu taarifa za kuwapo kwa rushwa ndani ya CCM kwa muda mrefu na uwezo wake wa kuiondoa, Mangula alisema atafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na pia atashughulikia malalamiko yatakayolewa kwa sababu lazima kuwapo kwa malalamiko rasmi.
Kuhusu rushwa ya mtandao ambayo inadaiwa kuibuka ndani ya CCM, Mangula alisema haifahamu kwa kuwa wakati tuhuma hizo zinaibuka, alikuwa shambani kijijini kwake akilima.
Mangula alisema chama hicho kitatekeleza uamuzi huo kama ambavyo kiliwahi kutengua matokeo ya uchaguzi mwaka 2000, walipoengua wagombea 32 waliokuwa wameongoza kwenye kura za maoni.
Alisema mwaka huo, CCM kilitengua pia matokeo ya majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Morogoro Mjini, Singida Mjini na Bukombe.
Alisema kazi hiyo itafanyika ndani ya miezi sita kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la mwaka 2012 kifungu cha 33 (2) na (4), cha miiiko ya kuzingatiwa wakati wa uteuzi na uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, kifungu cha 33 (2), kinaeleza kwamba ni mwiko kwa mgombea au kiongozi yeyote kutoa au kupokea rushwa na kwamba ikithibitika ametumia rushwa kupata nafasi husika atapokonywa ushindi.
Kadhalika, kifungu hicho kinaeleza kwamba mtu huyo atazuiwa kugombea uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM au atapewa adhabu kubwa nyingine zaidi ya hiyo kama itakavyoamuliwa na kamati hiyo.
KUUNDA MITANDAO
Kifungu cha 33 (4) kinaeleza zaidi kwamba ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume cha ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa.
Hata hivyo, Mangula hakutaja kiasi cha malalamiko ambayo yamepokelewa na chama wala hatua ya uchambuzi ilikofikia.
Msimamo huo wa Mangula umekuja siku chache tangu kumalizika kwa chaguzi za ndani za CCM ambazo zililalamikiwa na baadhi ya makada kwamba baadhi ya walioshinda walitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua kura.
Miongoni mwa chaguzi zilizolalamikiwa ni katika baadhi ya wilaya na mikoa, lakini zaidi zile za jumuiya za chama hicho; Umoja wa Wanawake (UWT), Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.
Itakumbukwa kuwa ni kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, alisema waziwazi wakati akifunga mikutano ya UWT na Wazazi na wakati wa kufungua ule wa UVCCM kwamba vitendo hivyo vitakipeleka chama hicho kubaya ikiwa havitakomeshwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment