Waliokulia maeneo ya wafugaji wanalielewa hili vizuri sana. Inapoonekana ng’ombe wamekondeana watu huuliza; hawa ni ng’ombe wa nani? Msemo huu una maana kubwa katika dhana nzima ya uongozi.
Unaposhindwa kuongoza usisingizie unaowaongoza, maana, kiongozi ana wajibu wa kuonyesha njia. Ni njia ya kufuatwa na wengine.
Ona pichani watoto hao wakibeba kuni na kutembea mwendo mrefu. Ni Pawaga , iringa. Na wakifika nyumbani kuna shughuli ya kuchota maji. Inahusu kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii; ni pamoja na maji pia. Watu wetu wanatahabika, na zaidi maeneo ya vijijini. Ni aibu yetu.
Kuna wakati nikiwa kijijini kwetu Nyeregete nilifuatwa na mama mmoja . Aliniomba nimsomee kadi yake ya hospitali. Hakujua kusoma na kuandika. Alikuwa akiugua UKIMWI, alitumia dawa za kurefusha maisha. Masikini, hakujua ni lini tarehe aliyopangiwa kwenda kuchukua vidonge vyake.
Nikamwambia, kuwa ni tarehe hiyo aliyonionyesha kadi yake kwa mwezi mmoja uliopita ndipo alitakiwa akachukue vidonge vyake. Nilimwangalia alivyoinamisha kichwa chini kwa huzuni. Hakufahamu hilo, nami napatwa na huzuni. Si tu nami nilihuzunika, bali, niliona aibu pia. Nilifahamu, kuwa si kosa lake.
Wako Watanzania wengine kama yeye. Hawajui kusoma wala kuandika. Niliona aibu kwa vile, kama taifa, tunashindwa kuelewa , kuwa takribani asilimia 39 ya Watanzania hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Na kama taifa, hatuna mikakati thabiti ya kupambana na adui ujinga. Ni aibu yetu.
Na hilo ni Neno Fupi la Usiku Huu.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment