Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikaguzwa ujenzi wa shule ya ghorofa ya Sekondari Mpendae, alipotembelea ujenzi huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimpongeza mkandarasi wa ujenzi wa shuleya ghorofa ya Sekondari Mpendae bwana Liu Dao Xing kutoka China, alipotembelea ujenzi huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitembelea Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampas ya Tunguu wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi za sekta ya elimu Zanzibar.
Mkandarasi wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari Tunguu kutoka Kampuni ya Electrics Intarenational ya Dar es Salaam Bibi Consolata Ngimbwa akitoa maelezo ya ujenzi huo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipotembelea ujenzi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea taasisi za sekta ya elimu Zanzibar.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeitupia lawama Wizara ya Elimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madai ya kutoishirikisha ipasavyo wakati inapofanya mabadiliko hasa yale yanayohusiana na mitihani ya Taifa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Juma Shamuhuna ametoa malalamiko hayo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko makao makuu ya wizara hiyo Mazizini, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika sekta ya elimu.
Mhe. Shamuhuna amefahamisha kuwa Wizara ya Elimu Tanzania kupitia Baraza la Mitihani la Taifa, mara nyingi imekuwa ikafanya maamuzi bila ya kuishirikisha Wizara ya Elimu Zanzibar, jambo ambalo linawapa ugumu wa kuetekeleza mipango yao ikiwa ni pamoja na kuwaandaa wanafunzi kuweza kuyafahamu mabadiliko yanayofanywa na baraza la mitihani.
Ametoa mfano wa maamuzi yaliyofanywa hivi karibuni na baraza la mitihani ya kuwazuia baadhi ya wanafunzi kutofanya mitihani yao ya kidato cha sita hapo Februari mwakani kwa madai ya kutotimiza masharti ya kufanya mtihani huo, kwamba Wizara yake haikuarifiwa mapema juu ya masharti mapya ya sifa za kufanya mtihani wa kidato cha sita.
Amesema Wizara hiyo imekuwa ikikwepa kuiarifu Wizara yake juu ya mabadiliko yanayofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa, na badala yake imekuwa ikiziarifu Skuli binafsi, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Amesema hali hiyo imekuwa ikichangia kutoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wa Zanzibar kutokana na kutoarifiwa mapema juu ya mabadiliko yanayofanywa ikiwa ni pamoja na kubadilika kwa ratiba za mitihani pamoja na muongozo wa kufundishia “Syllabus” kwa baadhi ya masomo.
Akizungumzia suala hilo Makamu wa Kwanza wa Rais amezishauri Wizara hizo kukaa pamoja na kujadiliana juu ya hatua bora za kuchukuliwa katika kuondosha tofauti hizo, na kuelezea haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya karibu baina ya Wizara hizo mbili.
Baada ya kupokea taarifa ya Wizara hiyo iliyowasilishwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Abdalla Mzee, Maalim Seif alihoji juu ya uhaba wa madarasa ya kusomea pamoja na vikalio katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.
Pia ameelezea haja ya kurejeshwa kwa huduma za dakhalia ili kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali, hoja ambayo imeungwa mkono na uongozi wa Wizara hiyo kwamba wamelifikiria kwa muda mrefu suala hilo lakini bado wanakabiliwa na ufinyu wa bajeti.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Mwanaidi Saleh amesema Wizara hiyo ina dhamira ya kurejesha huduma hiyo kwa wanafunzi wakati wowote hali ya bajeti itakaporuhusu.
Katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Tunguu, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Idrisa Ahmada Rai, amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais juu ya mipango ya chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukifanya kuwa kituo bora zaidi cha elimu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Profesa Rai amesema miongoni mwa dhamira kuu za chuo hicho ni kutoa wahitimu wa ngazi mbali mbali ambao wataweza kukabiliana na changamoto za karne ya 21 ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameupongeza uongozi wa Chuo kicho kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa pamoja na mipango imara ya kukiendeleza.
Hata hivyo ameutaka uongozi wa SUZA kuweka vipaumbele katika utekelezaji wa malengo yake ili kuweza kukamilisha malengo hayo kwa wakati muafaka.
Katika ziara hiyo Maalim Seif pia alitembelea ujenzi wa skuli ya ghorofa ya Sekondari Mpendae pamoja na ujenzi wa skuli ya sekondari Tunguu, ambapo amewataka wakandarasi wa ujenzi huo kukamilisha kazi zao kwa wakati.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais amefanya mazungumzo na ujumbe wa serikali ya Uturuki ukiongozwa na Waziri wa Chakula, Kilimo na Mifugo wa nchi hiyo Bwana Mehmet Mehdi Eker.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea haja ya kukuza mashirikiano katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi zikiwemo biashara na utalii.
Bwana Aker amesema Uturuki imepata mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita baada ya kufanya mabadiliko ya sera yake ya kilimo, jambo ambalo limeongeza uzalishaji hasa katika kilimo cha mpunga.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ameiomba Uturuki kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Zanzibar katika kilimo cha umwagiliaji ikizingatiwa kuwa nchi hizo zina uhusiano wa muda mrefu
source: Hassan Hamad-Zanzibar
No comments:
Post a Comment