Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mpango wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwamo mawaziri kuanza ziara mikoani, hauwezi kukisaidia chama hicho kujiimarisha kisiasa wala kuathiri kasi ya Chadema ya kujipanua nchi nzima.
Chama hicho kimesema CCM hawatafanikiwa kwa kuwa zimejitokeza tuhuma nzito ambazo hazijajibiwa na serikali ya CCM kwa Watanzania na hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani na serikali ya chama hicho.
Kauli hiyo ya Chadema imekuja siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kueleza kuwa Sekretarieti mpya ya Chama hicho inatarajia kuongozana na mawaziri kufanya ziara ya kichama mikoani kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo.
Nnauye alisema juzi kuwa katika ziara hiyo ambayo itaanza leo katika mikoa ya Mtwara, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, atakuwa akiambatana na baadhi ya mawaziri kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu mwaka 2010.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema ziara hiyo haiwezi kukisaidia CCM kwa sababu hata mwaka 2007 mawaziri walifanya ziara mikoani kuelezea utekelezaji wa bajeti ya kipindi hicho na bado hawakufanikiwa.
“CCM leo ndiyo wameamka, sisi Chadema kama ni kufanya ziara kila siku tupo mikoani, tunakumbuka mwaka 2007 mawaziri walifanya ziara kama hiyo wakatumia fedha za walipa kodi Shilingi bilioni 2.5 na bado hawakufanikiwa, hawawezi kujibu hoja,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa ambaye wakati akizungumza na NIPASHE jana alikuwa njiani akielekea mkoani Kagera kwa ziara ya kichama, alisema CCM hawawezi kuwa na majibu ya kuwatosheleza Watanzania kutokana na kashfa na tuhuma kadhaa ambazo zimejitokeza kipindi hiki ambazo serikali yake imeshindwa kujibu na hivyo kuzua maswali mengi kutoka kwa wananchi.
Alitolea mfano mwaka 2007 wakati Chadema kilipowataja kwa majina baadhi ya viongozi wa serikali na CCM kwa tuhuma za ufisadi, lakini hadi sasa hawajachukuliwa hatua za kisheria licha ya kuwapo kwa ushahidi wa kutosha ambao ungesaidia kuwatia hatiani.
Dk. Slaa alisema kashfa nyingine za hivi karibuni ambazo bado serikali ya CCM haijazijibu ni utoroshwaji wa meno ya tembo yenye thamani ya Sh. bilioni 2.24 ambayo yalikamatwa na maofisa wa bandari ya Hong Kong.
Aliongeza kuwa kashfa nyingine ambazo Watanzania wanataka majibu ni usafirishaji wa wanyama hai akiwamo twiga kwenda nje ya nchi.
Dk. Slaa alisema CCM lazima itambue kuwa kikatiba kazi ya wapinzani ni kusema na serikaki kazi yake kubwa iwe ni kujibu hoja kwa vitendo kwa kutekeleza mambo yanayokuwa yanalalamikiwa.
“Wapinzani kazi yao ni kusema au kuisema serikali iliyopo madarakani, na serikali kwa upande wake inatakiwa kutekeleza mambo yanayolalamikiwa na nchi inaendelea kusonga mbele, lakini inashangaza unapoona serikali nayo inafanya propaganda za kisiasa, hii ni hatari,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kama serikali itaendelea kuzungumzia propaganda za kisiasa kwa kujibu kwa maneno wapinzani badala ya kutenda kwa vitendo, nchi itaendelea kurudi nyuma kimaendeleo na wananchi wataendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
“Watanzania wanataka kujua lini CCM na serikali yake watachukua hatua za dhati kukabiliana na ufisadi, CCM wasifikiri ajenda ya ufisadi itaishia hewani…hapana itakuwa ya kudumu hadi tutakapoona hatua zimechukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema.
Juzi Nape alisema kuwa Sekretarieti mpya ya CCM imeapa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kufuatilia mienendo ya watendaji wakuu wa Serikali wakiwamo mawaziri.
Alisema mpango huo ambao una lengo la kuongeza ufanisi wa Serikali, utawabana pia wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wanaosimamia utekelezaji wa Ilani hiyo.
Wakati wa mkutano wa nane wa CCM uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, alisema vyama vya upinzani vimekuwa hodari wa kutunga mambo ya uongo na kuyaeneza kwa wananchi, lakini kama mambo hayo yakiachwa na wana-CCM bila kujibiwa kwa kueleza ukweli, wananchi wataamini uongo huo na kuona ni ukweli.
Alisema tatizo lililopo ni kwa viongozi na wanachama wa CCM kutokuwa na tabia ya kuitisha mikutano ya hadhara kama vinavyofanya vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikitumia mikutano hiyo kueleza propaganda za uongo kwa wananchi.
Alisema baada ya CCM kukamilisha chaguzi zake, sasa kilichobaki ni kuchapa kazi na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili CCM iendelee kushika dola.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment