CCM na njia ya Kinana
Na Maggid Mjengwa,
MWANAFALSAFA Benjamin Disraeli anasema; “ Mamlaka zote msingi wake ni imani, tunawajibika katika kuyatekeleza yaliyo kwenye mamlaka zetu, na kwamba, mamlaka yatatokana na watu, kwa ajili ya watu, na chemchem zote za fikra ziachwe hai”- Benjamin Disraeli. Kwa kukiangalia anachosema Diseaeli tunaona, kuwa kazi ya Chama ya cha siasa haipaswi kuwa ni kuudhibiti umma katika kuhoji yanayofanywa na Serikali, badala yake, Chama kinapaswa kuwa upande wa umma. Ni katika kuyaelewa mahitaji ya umma. Na kwa vile Serikali inapaswa kuwa mtekelezaji wa yale yaliyoamuliwa kwa niaba ya umama, basi, kazi kubwa ya chama cha siasa ni kuisimamia Serikali katika kuutekeleza wajibu wake huo.
Tumeona, katika muda mfupi, Abdulahaman Kinana , Kama Katibu Mkuu wa Chama kinachoongoza, CCM, amelitambua jukumu lake kama Katibu Mkuu . Hivyo, amelitambua jukumu la Chama chake. Kuwa wajibu wake wa kwanza ni kuisimamia Serikali. Katika mawimbi mazito iliyoyapitia katika miaka ya karibuni, Wana- CCM wanapaswa kumshukuru Mwenyekiti wao wa Taifa, Jakaya Kikwete, kwa kufikiria kumweka Kinana kwenye nafasi hiyo ya kiutendaji katika wakati muafaka. Tunayemfuatilia tunajua, kuwa Abdulahaman Kinana ni mchapakazi. Na katika anayoyafanya, hana dhamira ya madaraka ya juu kabisa, bali, kukisaidia chama chake, na taifa. Maana, inavyoonekana sasa, Abdulahaman Kinana amekisaidia chama chake kuitafuta njia mpya ya kisiasa. Njia ya kisiasa anayokwenda nayo Kinana kwa sasa ni ya ‘ Kati- Kushoto’.
Hii ina maana, Kinana anakipeleka chama chake kwenye kupata miafaka ya kisiasa ya ndani ya chama, na wakati huo huo kutafuta kukubalika nje kwenye umma. Hii ni kwa kuegemea kushoto zaidi. Kushoto ya kiitikadi ndiko waliko wengi. Na njia ya Kinana ndiyo inayopaswa kufuatwa na wenzake ndani ya CCM. ni njia iliyoonyoka na yenye tija kwa umma na hatimaye, ni njia inayoweza kukinufaisha chama chake. Maana, katika siasa, njia nyingine hazina tija kwa umma wala chama chenye kuchagua njia hiyo. Ona ngojera zile za CCM za ‘ kuvua magamba’. Ama hakika, mradi wa kisiasa wa ‘ kuvua magamba’ ni moja ya miradi ya hasara kubwa Chama Cha Mapinduzi imepata kuifanya. Ni mradi uliokigharimu zaidi chama hicho kisiasa kuliko kukiletea tija. Na yumkini, makovu ya mradi huo yatabaki kwa muda mrefu ndani ya chama hicho. Maana, mradi wa kujivua magamba haukulenga kwenye kubadili mfumo uliosababisha tatizo, bali , ulichukua sura ya mbio za Urais wa 2015, na hivyo, ukabeba sura ya kuwindana kisiasa ( Political Witch Hunting) zaidi miongoni mwa wana-CCM wenyewe kuliko kukijenga na kukiimarisha chama chao.
Leo Kinana na wenzake wanazunguka mikoani wakijenga hoja zaidi za kisiasa zenye kuwagusa wananchi. Mathalan, Kinana na wenzake wameonyesha wanavyofanya kazi ya kuisimamia Serikali kwa kuwabana watendaji wa Serikali hadharani. Kufanya hivyo ni moja ya kutekeleza wajibu wa chama cha siasa kinachoongoza nchi; kuisimamia Serikali. Maana, juma la jana niliweka bayana hapa, juu ya tatizo nililoliona, kuwa linaikabili CCM kama Chama cha Siasa, kuwa CCM imeusahau umma uliochoshwa na malumbano ya kisiasa yasiyoisha, malumbano ambayo msingi wake ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Chama. Vita ya kuwania nafasi za juu za uongozi. Umma ambao kwao wao lililo la msingi, kama alivyosema Askofu Desmond Tutu, ni kuhakikishwa wanapata huduma muhimu za msingi, kama vile ajira, elimu, maji ya bomba, makazi bora, huduma za afya na mengineyo. Umma unahitaji kutoka kwa wanasiasa, kauli zenye kuwatia matumaini ya baadaye. Kauli zenye kuashiria kwamba mwenye kuzitoa, amedhamiria kutatua matatizo yao ya kimsingi.
Umma unahitaji kutoka kwa wanasiasa, kauli zenye kuwatia matumaini ya baadaye. Kauli zenye kuashiria kwamba mwenye kuzitoa, amedhamiria kutatua matatizo yao ya kimsingi. Nikaweka wazi, kuwa hata kwa maslahi ya nchi yetu, ni heri kuwa na CCM yenye makundi yenye kuwania urais 2015 kuliko CCM yenye magenge yenye kuendesha biashara ya ‘siasa za rejareja na au ‘siasa za mafungu’ (retail politics). Ni kwenye ‘siasa za mafungu’ ndipo utawakuta wana-CCM wenye kudhani wao ni wasafi, na wenzao ni wachafu. Wakati, kimsingi, jamii nzima kwa sasa ni kama imeoza kimaadili.
Leo utawakuta wala rushwa CCM, na hata kwenye vyama vya upinzani. Utawakuta makanisani, misikitini na hata kwenye sekta ya michezo. Kinachohitajika ni mkakati wa kitaifa utakaohakikisha kwamba huko tuendako, tunapunguza idadi ya viongozi wa kisiasa, kijamii na hata kimichezo watakaoingia kwa nguvu za fedha, hivyo basi, nguvu ya rushwa. Kama alivyopata kutamka Mwalimu kwenye Kitabu Chake; Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, rushwa ni kama kansa kwenye jamii yetu. Kwa hiyo, ni tatizo la kimfumo zaidi kuliko la baadhi kwenye jamii. Itaendelea juma lijalo…
No comments:
Post a Comment