Mbunge wa Monduli Edward LOwassa Mwananchi
Ni kuhusu elimu bure hadi sekondari, asema iwe moja ya ajenda za ccm 2015
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa ni fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza weledi na uelewa wa mambo mengi katika jamii.
“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari kuwa kama elimu ya msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika mgogoro na CCM kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure inawezekana hadi ngazi ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa wakisema kuwa suala hilo haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni kuwahadaa wananchi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku akisema chama chake kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa elimu bure.
Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kupata ushindi, Rais Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha wapigakura kuwa kwamba ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja Kampeni wa CCM na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na kwa upande wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Novemba 10, 2010 katika Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za jamii bure” na kwamba lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika moja ya mikutano yake alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya elimu bure hadi sekondari kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.
"'Ni lazima tukubali na tujadili suala hilo kwa manufaa ya nchi kwa kila Mtanzania kukubali ushauri huo wa elimu ya sekondari kuwa ya bure,” alisema Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM) na kuongeza:
“Tukishakuwa na mjadala wa elimu yetu kuwa bure hadi ngazi ya sekondari, tena basi iwe ni elimu bora, jambo hili linapaswa kuwa moja ya ajenda kuu za CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.”
Alisema Serikali inapaswa kugharimia elimu ya sekondari bila ya woga na kwamba anaunga mkono wito uliotolewa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete akiwaagiza watendaji serikalini kusimamia ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata.
Alisema mafanikio katika ujenzi wa shule za kata nchini yanatokana na mpango ambao yeye ni mwasisi wake alipokuwa Waziri Mkuu na kwamba ali aliusimamia kikamilifu kuhakikisha unafanikiwa.
Azungumzia tuhuma
Katika hatua nyingine, Lowassa alizungumzia tuhuma zinazoelekezwa kwake kwamba ana utajiri wa kupindukia kwamba siyo za kweli na zinalenga kumpaka matope.
Alisema wale wanaomtuhumu kutokana na yeye kushiriki katika uchangiaji wa shughuli za kijamii hawamtendei haki kwani kuchangia siyo kosa.
Lowassa alisema anachokifanya yeye katika shughuli anayoalikwa huwataarifu marafiki zake kote nchini na kwenda katika eneo husika na kuchangia na yeye hana utajiri huo kama inavyodaiwa.
Alisema, ataendelea kuchangia bila ya wasiwasi yeye na marafiki zake na hatishwi na tuhuma hizo kwani siyo za kweli na aliziita kuwa ni ‘uongo wa kupindukia’.
Naye Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Thomas Laizer aliwataka waumini wa kanisa hilo kote nchini na waumini wa makanisa mengine kuwapuuza baadhi ya watu wenye kutaka kuleta vurugu nchini.
Askofu Laizer alisema vurugu za kuchoma makanisa zilizofanyika Mbagala na maeneo mengi zinapaswa zikomeshwe, lakini akatoa wito kwa waumini Waksrito walioguswa kutokuwa na mawazo ya ulipizaji wa kisasi.
Alisema, nchini kuna Waislamu wengi wasiounga mkono vitendo vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya waumini wa dini hiyo, hivyo makanisa yaombee amani ya nchi, ili Watanzania waendelee kuishi kwa utulivu.
“Kila mtu mwenye dini afanye maombi kuiombea nchi amani, yapo makanisa mengi yamechomwa moto na siyo kama waumini wa dini ya Kikristo ni waoga la hasha, bali mafundisho yetu yanakataza ulipizaji wa kisasi, kisasi ni kwa ajili ya Mungu,” alisema Askofu Laizer.
Katika harambee hiyo kiasi cha Sh133. 89 milioni kilichangwa, na kati ya hizo Sh87. 54 ni fedha taslimu na Sh45.85 ni ahadi. Fedha hizo ni zaidi ya malengo yaliyokuwa yamekusudiwa ya kuchangisha Sh120 milioni.
Hadi sasa ujenzi wa kanisa hilo umeshagharimu Sh186 milioni na hadi litakapokamilika linatarijiwa kuwa limegharimu kiasi cha Sh600 milioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment