Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akionnyesha Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, baada ya kuizindua rasmi huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanziba Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Mariam Khan baada ya kuzindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja
Waziri wa Afya Juma Duni Haji akiungana na
kikundi cha Sanaa Zanzibar kutoa burudani ya ngoma ya Msewe wakati wa uzinduzi
wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa
Kaskazini Unguja.(Picha na Salmin Said, OMKR)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa
jamii inahitaji kuelimishwa zaidi juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango kwa
maendeleo ya nchi na kutunza afya ya jamii hasa kwa akina mama na watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya
Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya
Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein.
Amesema jamii bado haijatoa umuhimu unaostahiki
katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hali inayopelekea kuwepo kwa
ongezeko kubwa la watu ambalo huathiri harakati za maendeleo na afya ya jamii.
“Taarifa zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa
inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3 milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya
asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba
imefikia watu 496 mwaka 2011”, ilieleza sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein
iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amefahamisha kuwa bado vifo vya mama wajawazito
viko juu duniani lakini vimepungua kwa upande wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa
kina mama wenye umri mdogo na wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.
“Kwa Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo
ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito 100,000 na kupungua kidogo hadi
kufikia vifo 454 mwaka 2010. Hata hivyo kwa Zanzibar vifo vya akina mama
vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 281 mwaka 2011, kwa kila kina mama
100,000 kwa takwimu za hospitali”, alifafanua.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za
serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa
chanjo za pepopunda na shurua, sambamba na kuimarisha huduma za afya ya uzazi
katika hospitali mbali mbali.
Kwa upande wao wawakilishi wa Umoja wa Mataifa
wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa huduma ya
uzazi na kuamua kutoa huduma hiyo bila ya malipo.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu
(UNFPA) Tanzania bibiMariam Khan amesema bado suala la uzazi wa
mpango linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wanajamii kuona
ugumu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango.
Amefahamisha kuwa uzazi wa mpango ni muhimu
katika kusaidia kukuza kipato cha wanafamilia, sambamba na kuwaendeleza watoto
katika makuzi bora, na wito kwa jamii kutoa fursa zinazostahiki kwa akina mama
na watoto ili kusaidia harakati za maendeleo kwa jamii.
Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema
wameamua kufanya uzinduzi huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kutoa uelewa
zaidi kwa wakaazi wa Mkoa huo ambao ni miongoni mwa mikoa inayofanya vibaya
katika suala la uzazi wa mpango.
Amesema akinamama na watoto wanahitaji kulindwa
kiafya, na kuwataka wazazi kushirikiana katika suala la malezi na makuzi ya
watoto.
Mapema akitoa muhtasari wa ripoti hiyo, Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Khamis Mussa amesema
kimsingi ripoti hiyo imeelezea juu ya changamoto, faida na haki za binadamu
katika uzazi wa mpango.
Amesema uzazi wa mpango ni miongoni kwa haki za
binadamu lakini imeelekezwa zaidi kwenye haki za kifamilia, ili wanafamilia
waweze kupanga juu ya idadi na umri wa kupishana kwa watoto, ili kuepuka mimba
zisizotarajiwa.
“Inakisiwa kuwa kiasi cha mimba milioni 80
zinapatikana bila ya kutarajiwa duniani, huku nusu ya mimba hizo zikitolewa,
jambo ambalo ni hatari nyengine katika uzazi”. Alidokeza Katibu Mkuu huyo.
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment