WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, April 6, 2014

Matumaini Katiba Mpya arijojo

Ukawaa 72f6e
Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza  kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
"Kweli matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine, ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya," alieleza Balozi Sefue.(Hudugu Ng'amilo)
Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15 Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.
"Lakini walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana," alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
"Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo watoto wadogo," alieleza Dk. Slaa.
Kauli ya LHRC
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi ya muda iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk. Bisimba alisema kwa hali ilivyo, hawana hakika ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi, kwa kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.
"Mambo ya nchi hii tunayafahamu, inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa," alieleza Dk. Bisimba.
Alisema hilo waliliona mapema, wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine, ili wananchi waelimishwe lakini hawakusikilizwa.
Alisema kuwa katika mazingira hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.
"Wakichezea Rasimu wajue wanachezea maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo kusababishia taifa hasara isiyomithilika," alieleza Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alisema mchakato huo umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana, lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa awali.
Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
"Hata hivyo tunachotakiwa kuzungumzia ni ubora wa kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza nchi kwa miaka 50 ijayo," alisema Kairuki.

CHANZO MWANANCHI

Msekwa: Sitta ana lake jambo

msekwaclip 19e78

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, 'mzungumzaji huyo ana lake jambo'.(Hudugu Ng'amilo)

Sitta akizungumza  juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi 'us' kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno 'Msekwa' kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.
Msekwa akizungumza  jana alisema: "Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo."
Aliongeza: "Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?"
Maoni mengine
Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga hoja iliyopo mezani.
Alisema kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.
"Tusianze kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe kuhusu Muungano," alisema Mwakagenda.
Sakata lilivyoanza
Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.
Hali hiyo ilitokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo katika hati hiyo ni ya kwake.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.
Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.

CHANZO MWANANCHI

Massauni: Zanzibar haijavunja Muungano

zanzibar 781ab
Bunge la Katiba limeanza kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba katika sura ya kwanza na sura ya sita ambayo kwa kiasi kikubwa inahusu Muundo wa Muungano.
Sura hizi mbili, ndizo ambazo zinaelezwa kuwa ni roho ya mjadala wa Katiba katika Bunge hilo Maalumu kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imependekeza Muundo wa Muungano wa serikali tatu katika sura hizo na ibara nyingi katika rasimu inayojadiliwa, zinajengwa kwa muundo huo wa Muungano.(Hudugu Ng'amilo)
Wakati akiwasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba bungeni Jaji, Joseph Warioba alitoa sababu nyingi za tume kufikia kukubali mapendekezo ya wananchi kuhusu serikali tatu.
Miongoni mwa sababu kubwa ni pamoja na sasa Muungano kubadilika kuwa ni wa serikali mbili na nchi mbili, Muungano ambao siyo ule ulioachwa na waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid Karume wa serikali mbili nchi moja.
Nchi mbili ndani ya Muungano, zimetokana na Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ambayo yalifanyika mwaka 2010.
Katika mabadiliko hayo yaliyopo katika sehemu ya kwanza tu ya Katiba ya Zanzibar yanasema Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambavyo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.
Zanzibar ni sehemu ya Muungano
Namba mbili katika katiba hiyo sehemu ya kwanza, inaeleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sehemu ya pili(a) inaeleza kuwa , kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyototungwa na Baraza la Wawakilishi.
Katiba ya Zanzibar pia imebadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema Sheria za Muungano zinazotungwa na Bunge la Jamhuri, zitume sehemu zote, lakini kwa sasa Zanzibar ili Sheria ya Muungano itumike ni lazima ipelekwe Baraza la Wawakilishi.
"Maana yake ni kuwa, Katiba ya Zanzibar ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano," anasema Jaji Warioba.
Kutokana na utata huu, Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad Yusuph Masauni alifanya mahojiano na gazeti hili na kueleza ifuatavyo;Swali: mababadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, yanatajwa kuwa moja ya mambo ambayo yamechangia sana mapendekezo ya Serikali tatu, je nini maoni yako?
Jibu: Ni kweli kuwa yamefanyika mabadiliko hayo, lakini kwa ufahamu wangu mimi nadhani Zanzibar hawajavunja Katiba, kwani kusema tu Zanzibar pia Katiba ya Zanzibar kumpa Mamlaka Rais kuigawa katika mikoa na wilaya siyo kosa.
Swali: lakini jambo hili linatajwa kuwa nyeti kwani kwa kiasi kikubwa licha ya matatizo mengine, inaonekana ndilo limebariki uwepo wa serikali tatu.
Jibu: Hapana. Kwanza naomba ieleweke Suala la Tawala za mikoa siyo la Muungano hivyo, haimzuii Rais wa Zanzibar kugawa mikoa na wilaya kwani jambo hili si la Muungano.
Swali: Unadhani ni kwa nini Zanzibar imefikia kufanya mabadiliko haya makubwa ya Katiba yake?
Jibu: Mimi sioni kama kuna tatizo, lakini kwa kuwa sasa tunatengeneza Katiba ya Muungano ni vyema tukafanya marekebisho kama tunataka kulifanya suala la tawala wa mikoa liwe la Muungano.
Swali: Masauni wewe ni mbunge wa Jamhuri wa Jimbo la Kikwajuni Zanzibar. Hivi sasa kuna mjadala mzito juu ya Muundo wa Serikali nini maoni yako?
Jibu: Mimi naunga mkono msimamo wa chama changu na wananchi wa jimbo langu kuendelea na muundo wa serikali mbili.
Swali: Lakini muundo huu unaonekana kulalamikiwa na Wazanzibari wengi kutokana na hoja kuwa Tanganyika imevaa koti ya Muungano na fedha nyingi zinaendesha Maendeleo ya Tanganyika badala ya Zanzibar.
Jibu: Ni kweli kuna madai hayo, lakini naamini changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi kama ambavyo aliahidi Rais Jakaya Kikwete alipokuja kuzindua bunge.
Swali: Lakini hata baada ya bunge kuzinduliwa na kutolewa ahadi hizo na Rais Wazanzibari na hata wanaounga mkono mfumo wa Serikali tatu, wanasema hata katika bunge hilo bado kunaonyesha Zanzibar kumezwa. Nini Maoni yako?
Jibu: Hayo ni madai ya wanasiasa wachache ambao wana malengo ya kushika dola kama mfumo wa Serikali tatu, ukipita lakini mimi binafsi naamini Zanzibar haijamezwa bungeni kwanza katika kamati zote kama Mzanzibari siyo mwenyekiti basi ni makamu.Swali: Je, wewe binafsi kwa mtazamo wako unaona ni Muundo wa Serikali ngapi unafaa na je, wananchi wa jimbo lako watakuelewa kwa kutetea msimamo wa chama chako?
Jibu: Mimi naunga mkono serikali mbili na hakika nikirudi na serikali tatu wananchi wangu hawatakubali sio kwa sababu jimbo langu wana ccm ni wengi lakini wana hoja.
Swali: Baraza la Wawakilishi limetajwa pia kupendekeza muundo wa serikali tatu, hasa kutokana na hoja yao, kutaka Zanzibar yenye Mamlaka, Tanganyika yenye Mamlaka na kujulikana Mamlaka ya Muungano.
Jibu:Binafsi siwezi kuzungumzia maoni ya wawakilishi lakini nadhani tatizo ni tafsiri tu zinachanganya watu.
Swali: Unadhani sasa Bunge hili la Katiba linaweza kusaidia kuondoa matatizo ya Zanzibar na hata Tanganyika katika mfumo wa Muungano uliopo?
Jibu: Ndio kwani Bunge hili lina jukumu kubwa la kutunga sheria ambazo ndizo zitakuwa kuu kwa pande zote na kuondoa kero za muda mrefu kwa kila upande.
Swali: Nini hofu yako katika Muundo wa serikali tatu?
Jibu: Hakuhitaji mtu kuwa ya PhD kujua kuwa serikali tatu zitaua muungano wetu, hofu yangu mimi bila Serikali mbili muungano unakwenda kufa.
Swali: Nini maoni yako ya jumla kuhusu Bunge Maalumu la Katiba?
Jibu: Mimi wito wangu kwa wajumbe,tutengeneze Katiba hii kwa maslahi ya wananchi na sio masilahi yetu. Hakuna wananchi ambao wanataka vurugu zitokee katika Bunge hili hata baada ya kupitishwa mapendekezo ya Katiba.

Mussa Juma ni mwandishi wa mwananchi.0754296503.

UCHAGUZI JIMBO LA CHALINZE ,CCM YAZIDI KUONGOZA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya mrisho Kikwete akisoma karatasi ya kupigia kura kabla ya kupia kura kumchagua Mbunge wa Jimbo la Chalinze kwenye kituo cha kupigia kura cha Zahanati Msoga.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye chumba cha kupigia kura wakati wa kupiga kura za kumchagua Mbunge mpya wa Jimbo la Chalinze.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipiga kura yake ya kumchagua Mbunge mpya wa Jimbo la Chalinze.
 Mama Salma Kikwete akiweka kura yake kwenye sanduku la kupigia kura kwenye kituo cha Zahanati Msoga.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha AFP Ndugu Ramadhani Mgaya akizungumza na waandishi wa habarai nje ya kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata namba 1na kusema kuwa Chama chake kitakubali matokea yeyote na pia kama watashindwa watajipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2015.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze Ndugu Mathayo Torongey akizungumza na baadhi ya mawakala alipotembelea kituo cha Ofisi Mtendaji Kata namba 1, Bwilingu.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze Ndugu Ridhiwani Kikwete akihakiki taarifa zake kabla ya kupiga kura kwenye kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata namba 3 Bwilingu, Chalinze.
Aziza mtoto wa mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ndugu Ridhiwani Kikwete akimsaidia Baba yake kuweka kura kwenye sanduku la kura ,Ridhiwani alipigia kura yake kwenye kata ya Bwilingu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Jimbo la Chalinze Ndugu Samuel Salianga akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata Bwilingu na kutoa tathmini ya jinsi zoezi linavyoendelea na kufafanua mambo mbali mbali yanayohusu uhalali wa wagombea kupiga kura popote ndani ya jimbo la uchaguzi.
wananchi  wa  jimbo la Chalinze   wamemaliza  kupiga  kura  hivi  punde  na  tayari  baadhi ya  vituo  matokeo  yameanza  kujulikana  huku  katika matokeo hayo ambayo  si rasmi mgombea  wa CCM Ridhiwani  Jakaya  Kikwete  anaendelea  kuongoza huku  vyama  vingine  vikimfuata kwa mbali  zaidi .
Hata  hivyo  zoezi   hilo  limefanyika katika  hali ya amani na utulivu na hadi  sasa  wananchi  wameendelea  kusubiri  matokeo  hayo kwa hamu  kubwa na baadhi ya  vituo  ambavyo  matokeo  yameanza  kujulikana  wafuasi wa CCM  wameanza  kushangilia .
Mbali ya  wafuasi wa CCM  kuonyesha  kuanza kushangilia  bado  wafuasi  wa  vyama  vikuu kama Chadema  na CUF  wameendelea  kujipa matumaini makubwa ya  kushida  katika  uchaguzi  huo na  kuwa  mwisho  wa zoezi la kuhesabu kura ndipo watakapo jua  mbichi na  mbivu  katika mchakato  huo 

 Tayari  Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha AFP Bw Ramadhani Mgaya ametangaza  msimamo  wa  chama  chake   baada ya matokeo hayo  kutangazwa kwa kudai kuwa atakuwa  tayari  kukubali matokeo hata kama atashindwa  katika  uchaguzi huo .

Mgaya  ambae amekuwa  mwanasiasa wa kwanza  wa  vyama  vya  upinzani  kuueleza umma kuwa  yupo  tayari  kwa  matokeo  hayo na  kutangaza  kujipanga kwa mwakani 2015  .
Wakati  mgombea  huyo wa AFP akieleza  hayo kwa upande wa  mgombea wa CCM Ridhiwan Kikwete  yeye  leo amefanya  kituko  cha karne  baada ya  kujipigia  kura  katika zoezi hilo na kisha  karatasi hiyo ya  kupigia  kura  kumpa mtoto  wake  mwenye  miaka  chini ya minne kuitumbukiza katika kisanduku  cha kuhifadhia kura 
uchaguzi  huo  unafanyika  kufuatia  kifo cha  aliyekuwa  mbunge wa jimbo  hilo kupitia  CCM Marehemu  Said Bwanamdogo aliyefariki  dunia mwanzoni mwa mwaka  huu .

Chanzo:Fransis G

Wednesday, April 2, 2014

BUNGE LA KATIBA NA FALSAFA YA MPE KAISARI YALIO YA KAISARI:



  • TIMIZA WAJIBU WAKO KWA JAMII YA TANZANIA KWA MAISHA YAO BORA na KWA VIZAZI VIJAVYO- falsafa ya kaisari;


Dhana ya uongozi wa namna yeyote ile unafaa uanzie nyumbani kwa kila mtu  uongozi ni uwezo wa kuweza kuyakabili kwanza yako mwenyewe na kufanya maamuzi sahihi bila kushawishiwa na mtu mwingine yeyote yule.

kwa kufanya hivyo utakuwa umefanikiwa kuyatawala maisha yako kulingana utaratibu ambao wewe mwenyewe umejiwekea kuanzia ndani ya familia yako;  ukifanikiwa hili unakuwa umefaulu katika mtihani huu wa kwanza wa uongozi ndipo jamii inapoanza kukuona kuwa hata ukipata nafasi ya  kuwaongoza wao pia utaweza kufanya maamuzi sahihi. 

 Kwa maneno mengine ni uwezo au njia ya kuweza kuwashawishi watu ili waweze kufanya kitu au kufikia lengo fulani la kikundi kwa ridhaa yao wenyewe. ili uongozi uwe bora ni lazima kuwe na kiongozi anayeongoza kundi fulani la watu au jamii husika.

Katika kila jamii kuna umuhimu wa kuwa na kiongozi kunatokana na ukweli kwamba watu wanapaswa kuwa na namna ya kuunganisha nguvu zao ili kufikia malengo yao. Katika  kila jamii, ni lazima kuwepo na mikakati ya kuunganisha nguvu, vipaji, uwezo na stadi mbalimbali za wana jamii. 

Wajibu wa msingi wa kiongozi yoyote ni kusaidia kuunganisha uwezo wa watu, kuratibu, kusimamia shughuli za watu, na kila inapobidi aonyeshe njia itakayosaidia kufikia lengo. Hii ndio dhana ya Bunge letu la Katiba ambalo limejengwa na watu wenye sifa na uzoefu tofauti tofauti ili watuletee katiba iliyo bora ambayo itaweza kudumu kwa vizazi;

Kwa dhana ya Plato uongozi ni dhana  au taaluma inayompa muhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaoongozwa kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao.

Uongozi bora una mchango mkubwa sana katika uimara wa jamii. Lakini tufahamu kuwa Ubora wa kiongozi unachangiwa na vitu vingi lakini tusisahau kuwa vile vile uongozi au kiongozi bora hutoka kwa Mungu. hivyo ndugu zetu wajumbe wa Bunge maalum la Katiba mjue kuwa mna dhamana nzito kwani mkiwatendea watanzania ndivyo sivyo adhabu yenu itatoka pande mbili kwa Mungu na kwa jamii iliyowachagua.

Leo hii wajumbe wa Bunge maalum la katiba ninyi ni viongozi muhimu sana ambao mtaingia katika vitabu vya kumbukumbu ya Taifa hili kuhusu katiba bora au mbaya kwa Taifa letu.  

swali la kuwauliza wajumbe wa bunge hili je wanajitahidi kumpa Kaisari yaliyo ya Kaisari au kuwatumikia wananchi waliowaweka katika nafasi hizo ambazo wanajivunia leo?

Je wajumbe  hawa wa bunge maalum kama viongozi muhimu wa Taifa hili leo hii  wanafahamu ukubwa na umuhimu wa maamuzi yao kwa jamii ya Tanzania?

Je Wajumbe wetu wa Bunge Maalum wanamalengo ya kufikia hatua ya juu kabisa ya ubora wa kutupatia Katiba Bora.? Inatakiwa wakumbuke kuwa Ni wajibu wa kiongozi kuwaongoza wana taasisi ili wafikie malengo yao. Kwa hiyo, kiongozi ni lazima aweze kubuni mikakati na mbinu zitakazoiwezesha taasisi anayoingoza kufikia malengo yake.

Je viongozi wetu wa bunge maalum wametawaliwa na maadili gani katika utendaji wa kazi yao hii Muhimu? Ili wakuliane katika hoja ni lazima wazingatia maadili ya msingi ya kufanikisha muafaka wa kitaifa kwa kujiepusha na unafiki kuficha hisia zao na kuwa kweli waaminifu katika hoja za msingi.

Je wajumbe wetu wa Bunge la katiba wamekuwa mifano miongoni mwao? Njia pekee ya kuonyesha ufano bora ni uwezo wa kuvumiliana katika hoja hata kama hoja hiyo huitaki tafuta jibu lililo bora, na sio kukataa hoja kwa kuzomea au kwa matusi huu sio msingi mzuri kwa kufikisha hoja au kufifisha hoja; 

kwa upande mwingine wajumbe wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutimiza wajibu badala ya kujali maslahi yao binafsi yatokanayo na itikadi au faida ambayo wanafikiria wao tu watanufaika nayo;

  • Je wajumbe wa bunge maalum wanajifahamu mwenyewe au wanaburuzwa buruzwa tu kufuatia itikadi wananzofuata?

  • wanafahamu wananchi wanatamani nini au katiba iwe vipi?

  • wanajua namna katiba hii itaweza kustawisha maisha ya wananchi wao na kuendelea kudumisha amani iliyopo katika pande zote mbili za jamuhuri ya Muungano?

Hebu tujikumbushe Busara za Baba wetu wa Taifa  Mwalimu Nyerere alipozungumzia dhana ya uongozi, Mwalimu Nyerere alisema, “uongozi ni kuonyesha njia.” Kwa maana hiyo, viongozi shurti wafahamu vema matokeo ya uongozi wao. Wasome imani za wanaowaongoza na nyakati zilizopo ili kutambua matumaini ya umma kimaisha.

TATIZO LA WAJUMBE WA BUNGE  MAALUM LA KATIBA NI NINI ?

  • Wanaelekea zaidi kwenye propaganda za kisiasa zilizojaa kuchafuana huku wakiacha mijadala ya maana bila kuipa kipaumbele. Wamesahau kuwa  la msingi hapa ni kuwa kiongozi yeyote anayekuwa tayari kuongoza na anapochaguliwa  kuongoza popote, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri. Atumie stadi za uongozi mwema kuonyesha njia.

  •  Inaelekea wajumbe wetu wa bunge bunge maalum wamejikita zaidi katika  kufikiria zaidi maslahi binafsi.  Wanaepuka kutumia stadi za uongozi kusimamia haki za waliowa wafikisha hapo hasa wanyonge. na. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.

Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha miongoni mwao  akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kupitia siasa safi kila kitu cha kunufaisha wananchi hupatikana. Bali ni muhimu viongozi wanaotarajiwa kufanikisha ustawi wa wanadamu, wapatikane kwa njia ya haki. Watokane na ridhaa ya watu wenyewe wanaotaka kuongozwa.

Hitimisho

Bunge maalum la Katiba lisitawaliwe na  malumbano ya mara kwa mara na matumizi ya lugha za kejeli na matusi; kwa kuendekeza tabia hiyo wananchi wanawaona wajumbe hawa wa bunge maalum wako zaidi kim kimasilahi na kiitikadi na kuto kubadilisha misamamo yao hata pale ukweli unapokuwa wazi.

Tunaendelea kuona kuwa wajumbe wengi waliochangia hoja wanafikiri malumbano yasiyo na msingi kwa Taifa letu leo hii na katika kipindi hiki muhimu sana. Itakuwa ni jambo nzuri kama wajumbe watajua matumizi ya muda ili kuepusha  mabaya ya rasilimali. Wanatakiwa kuweka mbele uzalendo wa Taifa hili na sio maslahi binafsi au ya kiitikadi.

MWENYEZI MUNGU IBARIKA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA UTUPATIE KATIBA ILIYO BORA KABISA KWA VIZAZI VYETU VIJAVYO.