WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, April 2, 2014

Maoni kuhusu Muungano v Shirikisho



Zitto Kabwe, Mjumbe, BMK
Iwapo Tanzania ni Shirikisho (Federation) au ni Muungano (Union) ni jambo ambalo limekuwa likuzua utata kwa miaka mingi. Hivi sasa katika vikao vya Kamati za Bunge maalumu la Katiba jambo hili limezua mjadala mkubwa ambapo baadhi ya Wajumbe wanapendekeza kuwa neno Shirikisho litoke kwenye sura ya kwanza ya Rasimu ya Katiba na wengine wakipendekeza libakie au hata kuweka wazi kabisa kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar. Maoni haya yanatokana na misimamo ya wajumbe kuhusu muundo wa Muundo wa Muungano kwa maana ya idadi ya Serikali. Ni vema dhana hizi kueleweka vizuri ili watumiaji waweze kuzitumia kwa usahihi. Kwa ufupi tutazame maana ya kila dhana na mifano mbalimbali duniani. Tutatazama dhana tatu kuu - Muungano (Union), Shirikisho (Federation) na Jumuiya (Confederation/Community).
Muungano (Union)
Katika aina hii ya Nchi kuungana huundwa Taifa moja, Dola moja ndani ya Nchi moja. Katika muundo huu Serikali za Washirika wa Muungano huachia sehemu kubwa ya madaraka yao kwa Serikali ya Muungano. Mara nyingi muundo huu hupelekea kuwapo kwa Serikali moja yenye nguvu ya Muungano na kama Washirika wanabakia na Serikali zao, basi hubakia na mambo machache sana. Faida ya Muundo huu ni kwenye uimara wake na sio rahisi kuvunjika. Hasara za muundo huu ni athari ya moja ya nchi, hasa kama ni ndogo, kumezwa na Mshirika mkubwa. Hapa Afrika Nchi ya Afrika ya Kusini (Republic of South Africa) inafuata muundo huu wa Muugano ambapo Serikali ya Muungano ina nguvu na mamlaka mengi kuliko Serikali za Majimbo yanayounda Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Huko Asia mfano mzuri ni Nchi ya India ambapo japo muundo wake unatoa nguvu kubwa kwa Majimbo kujitawala, Serikali ya Muungano (Union Government) ina nguvu kubwa zinazoondoa sifa ya kuitwa Shirikisho. Sio lazima 'Union' kuwa na Serikali moja (Unitary State) isipokuwa mazingira ya nchi husika ndio yanaweza kuamua. Mfano mzuri hapa ni ule wa Afrika ya Kusini ambayo ni 'unitary state' yenye Serikali 10, tisa za Majimbo na Moja ya Muungano.
Shirikisho (Federation)
Katika muundo huu Serikali za Washirika hukasimu sehemu ndogo ya madaraka yake kwa Serikali ya Muungano. Mambo ya kidola (sovereign functions) hufanywa na Serikali ya Shirikisho na Serikali za Washirika kubakia na mambo yake yenyewe. Kwa mujibu wa Sheria za kimataifa nchi yenye mfumo wa Shirikisho kuwa ni nchi moja katika sura ya kimataifa ingawa inawezaonekana ni nchi zaidi ya moja ndani ya Shirikisho husika. Faida kubwa ya muundo huu ni kuondoa hofu ya mkubwa kummeza mdogo na ule uhuru wa kujiamulia mambo mengi. Hasara ya muundo huu ni kujengwa kwa utaifa au hisia za utaifa za Washirika ambazo hatimaye hupelekea Shirikisho kuvunjika. Hapa Afrika mfano mzuri wa Shirikisho ni nchi ya Ethiopia ambapo Majimbo yake yanao uwezo hata wa kujitoa katika Shirikisho kikatiba. Eritrea ilitumia fursa hii na kujitoa kuwa sehemu ya Ethiopia mara baada ya mapinduzi yaliyomtoa Mengistu Haile Mariam. Ujerumani pia ni Shirikisho (Federal Republic of Germany au kwa kijerumani BundesRepublik Deutschland)
Jumuiya (Confederation/Community)
Katika muundo huu kila Mshirika anakuwa na uhuru wa mambo yake yote isipokuwa tu kunakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja. Aina hii ya Muundo ndio unapaswa kwa kinachoitwa Muungano wa Mkataba. Faida kubwa ya muundo huu ni kwamba hakuna kubanana na pale kunapotokea hofu Mshirika hujitoa. Hasara yake imo kwenye faida yake.Mfano mzuri ni Switzerland na Jumuiya ya Ulaya. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki pia inaitwa kuitwa ni Muungano wa Mkataba.
Muundo gani Tanzania?
Tanzania kuwa Shirikisho au Muungano ni mjadala ambao utaendelea kuwapo licha ya kuamua kuchagua muundo mmoja wapo. Wakati wa kuandika Katiba ya India mwaka 1947 ubishani huu ulikuwa mkubwa sana pia. Katiba ya India imegawanya mamlaka katika sehemu tatu - Mambo ya Muungano, Mambo ya Washirika na Mambo ya pamoja (concurrent). Wajumbe wa Bunge la Katiba la India wanaotaka Shirikisho walipinga muundo huo na kukataa 'Washirika kuwa ombaomba kwa Serikali ya Muungano'. Hata hivyo ubishi huo ulimalizwa na Mwanasheria mahiri wa India bwana B M Ambedkar kwa kusema 'tunataka Serikali imara ya Muungano na yenye nguvu iwezekanvyo' na alifunga mjadala kwa kusema 'Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la Washirika'. Hivi ndivyo ilivyo India ambapo pamoja kwamba ni Shirikisho lakini ni 'Unitary'. Vile vile Jamhuri ya Afrika ya Kusini ina muundo sawa sawa na nchi ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani lakini wakati Ujerumani ni Shirikisho, Afrika Kusini ni Muungano (Unitary).
Watanzania hatupaswi kuiga isipokuwa kujifunza kwa nchi nyingine. Hivyo muundo gani unafaa ni uamuzi wetu wenyewe. Hata hivyo uamuzi huo ni lazima ujibu vigezo fulani fulani. Vigezo vikubwa ni viwili; Je, Muundo tunaoutaka utajibu kero (malalamiko) za Muungano wa sasa? Je, Muundo tunaoutaka utajibu hofu za Muungano kuvunjika. Muundo utakaojibu hofu hizo ndio utakaotufaa. Tanzania inaweza kuwa na Muundo wa Muungano wenye Serikali tatu ama Muundo wa Shirikisho wenye Serikali mbili, ama kinyume chake. Idadi ya Serikali haina uhusiano wowote na ama tunaitwa Shirikisho au Muungano. Mifano miwili hapo juu ituongoze, India ni Muungano unaitwa Shirikisho na Afrika Kusini ni Shirikisho linaloitwa Muungano. Tanzania inaweza kuwa vyovyote vile ili mradi tu kunakuwa na Mamlaka ya kutosha katika masuala ya Muungano ili kuiweka Nchi pamoja na kuwa na Taifa imara mbele ya mataifa ya ulimwengu.
Muungano wa Serikali 3 na sio Shirikisho la Serikali 3 ndio mapendekezo yangu. Muungano (Union) wa Washirika ni bora, imara na endelevu zaidi kwa mazingira ya Afrika kuliko Shirikisho (Federation) la Washirika.
Mapendekezo yangu mahususi yaliyowasilishwa kwenye kamati namba 12 ni kama ilivyo hapa chini.
SURA YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA
1(1)    Irekebishwe na kuandikwa upya na isomeke
Tanzania ni Nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa Nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
1(2) neno Shirikisho lifutwe na kuongeza maneno ....Nchi ya.... baada ya neno 'ni' na kabla ya neno 'kidemokrasia'
Ongeza ibara ya mpya ya 3 itakayosomeka
3(1)  Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya Utendaji, vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo vitatu vyenye madaraka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma
3(2) Vyombo vyenye Mamlaka ya Utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika; vyombo vyenye Mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni mahakama  ya Juu ya Jamhuri ya Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Mahakama ya Zanzibar na vyombo vyenye Mamlaka ya ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
3(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba hii, kutakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja na kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo mambo ya Muungano na yasiyo ya uratibu wa pamoja.
3(4) Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake na Katiba za Serikali za Washirika na kwa kufuata masharti ya katiba hii.
3(5) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Tanganyika au Serikali ya Zanzibar Bunge laweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika Mikoa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge Isipokuwa kwamba Bunge litapata kwanza Azimio la Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kwa mikoa ya Tanganyika au Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa mikoa ya Zanzibar.
SABABU ZA MAREKEBISHO YANAYOPENDEKEZWA.
Rasimu ya Katiba imetangaza tu kuwa 'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(JMT) ni Nchi' na kuacha 'ambiguity' ya kwamba Tanzania ni nchi ngapi.
Katiba ya sasa imetamka bayana kuwa 'Tanzania ni Nchi Moja'. Rasimu pia imetamka kwamba JMT inatokana na 'muungano wa nchi mbili'. Hivyo basi ni vema kuweka wazi kabisa kuwa Nchi hizi mbili zimeunda nchi moja. Hii itaepusha migongano ya siku za usoni kuhusu tafsiri ya Katiba na Mamlaka za Nchi. Ifahamike wazi kuwa idadi ya Serikali haina uhusiano na uundaji wa nchi moja.
Rasimu imetangaza kuwa Tanzania ni Shirikisho ingawa bado imetamka 'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United Republic of Tanzania). Dhana za 'Union' na 'Federation' ni dhana mbili tofauti katika miungano.
Idadi ya Serikali haina mahusiano ya moja kwa moja na aina ya Muungano kama ni 'Union' au ni 'Shirikisho'. Kwa mazingira ya Nchi za Kiafrika ni salama zaidi kuwa na 'Union' kuliko Shirikisho. Kwa kutumia maneno ya Mwanasheria gwiji na mwandishi wa Katiba ya India Bwana B M Ambedkar, "Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la Washirika". Ni vema kuwa na Muungano wenye Serikali ya Muungano yenye nguvu iwezekanavyo ili kuhimili vishindo na changamoto dhidi ya Nchi yetu na umoja wetu bila kuathiri uhuru wa Serikali za Washirika kuendesha mambo yao wenyewe bila bugudha.
Rasimu imeweka sura ya Kwanza bila kutaja vyombo vya Jamhuri ya Muungano. Ni vema ili kuondoa 'ambiguity' vyombo vya Jamhuri ya Muungano kutajwa kinagaubaga katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika sura ya 'uundwaji wa nchi'. Mapendekezo ya ibara mpya za sehemu ya kwanza ya sura ya kwanza yanazingatia tahadhari hiyo. Katika kutaja vyombo mapendekezo haya yanaonyesha dhahiri kuwa ugawaji wa Nchi katika Mikoa inakuwa ni mamlaka ya Bunge. Serikali za Washirika zaweza kuwa na mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mikoa inapaswa kuwa mamlaka ya Bunge la Muungano kwa sababu yaweza pia kutumika katika kupata Wabunge wa Muungano lakini pia itasaidia kuondoa tabia ya kugawa mikoa hovyohovyo.  Kimsingi ilipaswa Mikoa yote ya Nchi itajwe ndani ya Katiba kuongezeka au kupunguka kwake kutokane na maamuzi maalumu ya Bunge hata ikibidi iwe kwa theluthi mbili.
SURA YA SITA
Ibara ya 60(1) maneno shirikisho yafutwe na kubaki uwepo wa Serikali 3.
60(3) isomeke
Muundo, madaraka na mambo mengine ya kiutendaji yahusuyo Serikali ya Tanganyika, na Serikali ya Zanzibar yataanishwa katika Katiba za Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
Ibara ya 63 iitwe 63(1)
Iongezwe 63(2)
Kwa ajili ya uratibu bora wa shughuli za Mamlaka za Nchi na kwa ajili ya kuhakikisha ufanisi na weledi katika uendeshaji bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgawanyo wa madaraka, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya uratibu juu ya mambo ya uratibu kama yalivyoorodheshwa katka nyongeza ya pili ya Katiba hii.
64(1) maneno nchi washirika yaondoke na kubakia neno Washirika au Washirika wa Muungano.
64(5) isomeke
Serikali za Washirika zitakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano na zitatekeleza majukumu yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka za Serikali za Washirika kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Serikali za Washirika kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
65 maeneo yote yenye maneno Nchi Washirika yafutwe na kuandikwa Washirika wa Muungano
67 ifutwe yote
69 maneno Nchi yafutwe ....katiba za Washirika.......
69 (2) maneno Viongozi wakuu yafutwe na kuandikwa ' Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni Viongozi Wakuu wa Nchi'
69(3) isomeke
Viongozi wanaohusika na masharti ya ibara hii ni
(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano
(b) Mkuu wa Serikali ya Tanganyika ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
(c) Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ambaye pia atakuwa  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Ongeza ibara ya 70
(1) Mkuu wa Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataitwa Rais atapatikana kwa kuchaguliwa kwa kura na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano kwa Mujibu wa masharti ya Katiba hii. Rais atakuwa pia Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Wakuu wa Serikali za Washirika watapatikana kutoka kwenye Mabaraza ya Wawakilishi ya Washirika kutoka Chama cha siasa chenye wawakilishi wengi kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
SABABU ZA MAPENDEKEZO
Lengo ni kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano inabakia ni nchi moja yenye serikali 3 zenye mamlaka na madaraka yake yaliyofafanuliwa na katiba. Kwa kuwa tunaamua kuwa na Nchi moja basi Serikali zinazoundwa zitakuwa ni Serikali Washirika na sio nchi Washirika tena kama rasimu inavyoita. Kuweka wazi kuwa ni kiongozi mmoja tu wa Serikali ndio atachaguiwa na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano naye ni Rais - Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na usalama.
Majina ya Wakuu wa Serikali za Washrika yatatolewa na kwa mujibu wa Katiba zao na hivyo hakuna sababu kwa Katiba ya Muungano kuunda majina isipokuwa tu Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia kuwa iwapo Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, makamu wa kwanza atatoka upande wa pili wa Muungano. Makamu wa Rais wanaweza kukaimu Urais kwa masharti maalumu yatakayowekwa na Katiba.
Mapato na mgawanyo wa Mapato ya Muungano katika Serikali Tatu
Dola inapasa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa kwa Washirika na Mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana. Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano. Kuna haja ya kuangalia kwa umakini mkubwa suala hili la mapato ya Serikali ya muungano kama kweli kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano. Mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo;
Mapato ya Muungano
1. Ushuru wa Forodha
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye mikoa kwa mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3. Ushuru wa Bidhaa na huduma ambapo 60% itagawiwa kwa nchi Washirika kwa ajili ya miradi maalumu ya muungano.
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Mapato ya Serikali za Washirika
1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni 2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au kodi kama hiyo 3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu wa sheria 4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.
Mapato ya Mikoa
1. 25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika mkoa husika 2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika 3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano 4. Mgawo kutoka Serikali ya Washirika 5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa
Dodoma,
Aprili 2014

BUNGE MAALUM LA KATIBA MPYA LIMETAWALIWA NA LONGO LONGO ZA KIITIKADI:




Wakati Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ipo katika mchakato wa kupata katiba mpya baada ya tume ya Jaji warioba kuwasilisha rasimu ya pili ya katiba mpya na mheshimiwa Rais wa Jamuhuri kuwatangaza rasmi wajumbe  zaidi ya 600 ambao ni wawakilishi wa wananchi wa Tanzania katika upatikanaji wa Katiba hiyo Mpya.

Safari hii ya maandalizi ya kuandaa katiba mpya kwa kweli imekuwa haionyeshi mwelekeo mzuri ambao unaleta matumaini kwa taifa letu. Tunafahamu fika kuwa Mheshimiwa Rais kupitia washauri wake ametuteua watu wazuri na ni tegemeo letu kuwa wawakilishi hao ni watu wenye hekima na uwezo mzuri wa kutuandalia Katiba Bora kwa vizazi vijavyo.

Kutangazwa kwa bunge hili la katiba kwa upande mmoja iliamsha matumaini ya wananchi kuwa kazi hii itakuwa nyepesi na yenye tija nzuri kwa maendeleo ya Taifa na wananchi wake ndani ya miezi mitatu ambayo  Bunge hili limepewa ili kukamilisha kazi yake kuanzia February  2014.

Lakini cha kushangaza mpaka niandikapo waraka huu, inasikitisha kuwa  kuwa mwendo wa bunge hili ni wa kusuasua.  Kwa maneno mengine hakuna mwelekeo mzuri ambao bunge hili maalumu limeonyesha baada yake bunge limepewa majina ambayo hayaendani na wadhifa wake.

Bunge lililojaa mizengwe , malumbano, kashfa, mivutano na kadhalika.

Kama wananchi tuna mengi ya kujiuliza hawa waheshimiwa wabunge wanafanya haya yote kwa faida ya nani?

Je waheshimiwa wajumbe wanaelewa nini wanatakiwa wafanye kwa faida ya Taifa hili?

Je kupitisha kanuni za kuendesha bunge maalum  ni lazima watukanane?

Ni ukweli ambao haufichiki kuwa  hata Aristotle katika maelekezo yake kuhusu Demokrasia alikuwa anahimiza katika Majadiliano ya hoja; na sio kuzomeana na kutukanana; lakini ukifilisika kifikra matokeo yake ni kuzomea au kutukanana.

Na kutika kufikia hitimisho lazima kuwe na mshindi ambaye atapatikana kwa uwingi wa kura kama kura itatumika kama kigezo, hii ndio demokrasia; Lakini wachache wanaweza kuwa na hoja nzito ambazo zinaweza kulegeza msimamo wa wengi. Lakini sio kufikia hitimisho kwa malumbano na matusi.

Wajumbe wanatakiwa wafahamu kuwa  misimamo binafsi na ya kichama hapa sio mahali pake; kama mwandishi mmoja alivyoandika kuwa “Inasikitisha kuona baadhi ya wajumbe wakitoa kauli zisizo na staha, wakishindana kwa hoja zisizo na mashiko na hata kusisitiza misimamo yao binafsi kwa ajili tu ya kukomoana, kutokana na tofauti za kiitikadi”.

 
Kwa kufanya hivi tuelewe fika kuwa waheshimiwa wajaumbe wa Bunge maalum watakuwa hawajefanikiwa kukonga roho za watanzania ambao kiu ya kupata katiba mpya na Bora;

Ni kweli kuwa wajumbe hawa walichaguliwa kutokana na ubora wao? Au wamechaguliwa kutokana na misimamo yao na vitisho ambavyo wamekuwa wakivionyesha kwa serikali ili kuwazima mdomo? Ndio maana tunashuhudia longo longo zaidi kuliko busara ya kiutendaji? Tulitegemea kuwa wangeanza safari hii ya miezi Mitatu kwa busara na hekima, kwa kuheshimiana na kwa kuzingatia zaidi hoja na kujadiliana kwa staaha na undugu na sio longo longo..

Kinachoendelea Dodoma ni kutegemea sana busara za wajumbe wachahce ambao wanaweza kulivusha bunge hili salama kama sio hivyo  liataendelea na longo longo na kupoteza mwelekeo.

Mwandishi mmoja aliwahi kuandika kuwa “Sisi kama watanzania tunatamani kujua viongozi wetu wanasimaia wapi na tujue mitazamo yao kisiasa.” Kinachopiganiwa na watanzania ni hiki  hoja ya wengi lazima iwe hoja yenye maslahi ya taifa na sio kunufaisha itikadi Fulani au kundi Fulani tu.

Itakuwa vizuri kuwa wajumbe watakao simama upande wa wengi  wahakikishe kuwa  wanantetea haki za wote na tuweke misingi itakayohakikisha kuwa maslahi binafsi au ya kichama hayatawali. Kwaq msingi huu nguvu ya walio wengi isiwe ya ubabe na dhuluma, bali iwe ni nguvu ya kweli na yenye kujitambua inayotaka kujenga utaifa na kujali raia wote na haki zao.

Longo longo  hizi zitokanazo na wajumbe ambao sisi tunawaona kuwa wana busara zinazoendelea kutolewa ndani na nje ya Bunge haziashirii mwisho mzuri. 

Kauli ya mheshimiwa Freeman Mbowe, ambayo aliitoa wakati longo longo na mabishano inaendelea imeonyesha busara “amesema kwamba bado wataendelea kushiriki kwenye vikao, ingawa wataendelea kupigania mageuzi ya msingi kwenye uendeshaji wa Bunge hilo ambalo linatakiwa kutoka na Katiba Mpya itakayopigiwa kura ya maoni ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili kutoka sasa”.

 Tatizo la wanansiasa na vyama vyao  kama mwandishi mmoja alivyoandika “Vyama vya kisiasa vimekuwa vinafikia muafaka katika mambo mbalimbali na kutoa taswira kwamba kuna muelekeo mzuri, lakini baadae wanasiasa haohao wanabadilika na kuyabadili maridhiano hayo na kuanzisha mijadala mipya inayoturudisha nyuma.”
 

Waheshimiwa wajumbe tunawaomba sana achane hizi  longo longo za kiitikadi ambazo hazina faida kwa Taifa na Amani yetu ambayo imedumu kwa miaka 50 sasa.

Tuesday, April 1, 2014

Ukawa wahamishia vita serikali 3 uraiani

  Sasa serikali mbili kupingwa nchi nzima
  Prof. Shivji ashambuliwa kuwa kigeugeu
 
 
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Tundu Lissu na Ismail Jussa,Wakizungumza na wandishi wa habari jana mjini Dodoma.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umehamishia mapambano yake nje ya Bunge la Maalumu la Katiba ili kuhakikisha kwamba Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haichakachuliwi.
Kuanzia jana viongozi wa Ukawa inayoundwa na vyama vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi walianza kukutana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara jijini Mwanza na kuwaeleza kwamba ikiwa rasimu itachakachuliwa waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya kuipitisha Katiba hiyo.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mirongo, Katibu  Mkuu  Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliwataka Watanzania  wapige kura ya hapana, ikiwa CCM kupitia  wingi wa wabunge  wao katika Bunge Maalumu  la Katiba watashinikiza muundo wa serikali mbili badala ya serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Hata hivyo, alimshangaa Prof. Issa Shivji  kwa kuunga mkono muundo wa serikali tofauti na kauli aliyowahi kuitoa miaka kadhaa iliyopita kuwa Zanzibar inastahili kuwa nchi kamili.

“Mimi ninawashauri Watanzania wenzangu  msikubali kuburuzwa iwapo CCM kwa kutumia  wingi wa wajumbe kwenye Bunge Maalum la Katiba wataamua muundo wa serikali mbili badala  ya maoni yenu kuwa mnataka muundo wa serikali tatu...kwa hiyo mpige kura ya hapana," alisema Dk. Slaa huku  akishangiliwa na umati wa wananchi.

Alisema hotuba ya Rais Kikwete baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba    haikuwa na nia njema kwa wananchi, kwa vile ililenga kuwatisha juu ya kuwepo kwa serikali tatu, jambo ambalo ni kuinglia uhuru wa  wananchi na kinyume  cha katiba iliyopo.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, pamoja na kupokea vitisho kutoka CCM na serikali yake, Ukawa  wataendelea kutoa elimu kwa wananchi  kuhusu wajibu wao katika mchakato wa kupa Katiba mpya.

Alisema baada mkutano wa Mwanza, yeye na makatibu wengine  wa NCCR-Mageuzi na CUF  watapanga ni lini mikutano kama hiyo itafanyka kayika mikoa ya Mbeya, Tanga, Rukwa, Ruvuma na visiwani Zanzibar.

Kaimu Katibu Naibu Katibu Mkuu  wa CUF Bara, Abdul Kambaya, alisema hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete iliegemea upande wa chama chake.

Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mozena Nyambabe, aliwataka wananchi kupiga kura ya hapana ikiwa CCM inayotetea serikali mbili itashinikiza muundo wa sasa wa muungano uendelee.

LISSU, JUSSA WAMSHANGAA SHIVJI
Katika hatua nyingine, siku moja baada ya Prof. Shivji kuonya juu ya muundo wa serikali tatu, wajumbe wawili wa Bunge Maalum la Katiba, wamemjia juu na kusema kuwa anasaliti msimamo na machapisho yake aliyoyasimamia kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kwa lengo la kuifurahisha serikali na CCM.

Wakizungumza na wandishi wa habari jana mjini Dodoma, wajumbe hao, Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu, walisema wanamshangaa Prof. Shivji kwa matamshi yake na kutoamini kama aliyoyasema ilikuwa ni kwa akili yake au alishinikizwa.

Lissu alisema kuwa msimamo wa sasa wa Prof. Shivji kwamba Muungano wa serikali mbili unapaswa kudumishwa, umeshtua kwa kuwa unapingana na maandiko yake aliyochapisha kwenye vitabu mbalimbali yakipinga Muundo wa serikali mbili.

Lissu ambaye ni mwanafunzi wa Prof. Shivji alisema kutokana na kumpenda mhadhiri huyo aliitwa ‘Mtoto wa Shivji’ na kwamba mwaka 1990 Prof. Shivji alitoa mhadhara wa kiprofesa uliosababisha apewe u-profesa akizungumzia misingi ya kisheria na uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema kuwa katika mhadhara huo, Prof. Shivji alisema kuwa ili makubaliano ya Muungano yaweze kupata uhalali, ni lazima yatungiwe sheria ya kuridhia makubaliano hayo na mabunge ya nchi washirika.

Alisema kwa mujibu wa Prof. Shivji, upande wa Tanganyika ipo sheria iliyotungwa na Bunge la Tanganyika ya kuridhia Muungano huo, lakini kwa wakati huo hakuwa na ushahidi wowote kama upande wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilitunga sheria hiyo.

“Katika mhadhara huo, Shivji alisema kuwa Bunge la Tanganyika lilitunga sheria kuridhia mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini hakuwa na ushahidi wa sheria ya aina hiyo kutungwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar,” alisema Lissu akimnukuu Prof. Shivji.

Alisema kuwa miaka 18 baadaye Prof. Shivji aliandika kitabu kingine akisema kuwa katika utafiti wake sasa anao ushahidi kwamba Baraza la Mapinduzi la Zanzibar halikutunga sheria ya kuridhia mapatano ya Muungano.

Alisema Prof. Shivji katika kitabu hicho alichokiita ‘Pan Africanism or Pragmatism’, alisema kuwa sheria ya kuridhia muungano kwa upande wa Zanzibar ilighushiwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali la Tanganyika mwaka 1964.

Alisema kwa machapisho hayo, Prof. Shivji alikuwa akipinga muundo wa Muungano wa serikali mbili, lakini anashangazwa na hatua ya sasa ya mhadhiri huyo kugeuka ghafla na kutamka hadharani kuwa muundo huo unapaswa kudumishwa.

Lissu alisema kuwa wamejipanga na wanazo nyaraka zote za kupambana ndani ya Bunge Maalum la Katiba kuhakikisha sasa unaanzishwa muundo wa Muungano usiokuwa na kero kama ilivyo hivi sasa na anaamini kuwa muundo mzuri ni ule uliopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wa serikali tatu.

“Tumejipanga, tutamjibu Prof. Shivji kwenye vikao vya Bunge Maalum ambapo ndio mahali sahihi pa kujadili Rasimu ya Katiba na kufanya marekebisho yenye maslahi kwa Watanzania wote,” alisema Lissu.

Kwa upande wake Jussa alisema machapisho ya Prof. Shivji ndiyo yaliyochangia kuamsha vuguvugu la Wazanzibari kudai haki kwenye muundo wa Muungano, hivyo anashangazwa na kitendo cha Prof. Shivji kuyageuka machapisho yake na kutangaza hadharani kuunga mkono muundo ambao alikuwa akiukosoa kwa miaka mingi.

Alisema kitendo hicho kimemkwaza kwa kuwa yeye ni miongoni mwa Wazanzibar waliompatia ushirikiano mkubwa wakati akifanya utafiti wa masuala ya Muungano Visiwani Zanzibar.

“Mimi binafsi niliujua vema msimamo wa Prof. Shivji kwa sababu nilitoa mchango wangu kwake wakati akifanya utafiki kiasi cha kufikia hata yeye mwenyewe kunipa heshima kwa kunishukuru katika kitabu chake cha Pan African or Pragmatism kuwa hakuupenda muundo wa serikali mbili, lakini ghafla amegeuka na kuunga mkono, kwa kuwa mhadhara alioutumia uliandaliwa na serikali inawezekana amefanya hivyo kwa shinikizo,” alisema Ladu.

Alisema mbali na Prof. Shivji kutumika kupiga propaganda za CCM, lakini yeye na wenzake waliofundishwa na Prof. Shivji wataendelea kubaki na msimamo thabiti wa kuhakikisha unapatikana muundo wa Muungano wenye usawa kwa nchi zote washirika.

Imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza na Emmanuel Lengwa, Ashton Balaigwa, Dodoma
 
CHANZO: NIPASHE

Jaji Warioba atukanwa kongamano la Muungano

warioba_f27d9.jpg
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, juzi alishambuliwa katika kongamano la kujadili Muungano lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu huku mmoja wa washiriki akidiriki kumtukana.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na wanafunzi takribani 300 kutoka Tanzania Bara ba Visiwani, liliandaliwa kujadili namna ya vijana wanavyoweza kuulinda Muungano usivunjike.
Peter Magoti, mwanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, alimshambulia Jaji Warioba kwa kudai asubiri afe ndipo Muungano uvunjike kwani amebakiza miaka mitano kufa na kwamba hawezi kuishi zaidi ya miaka mitano. (J.G)
"Huyu Warioba amekuwa kiongozi katika serikali ya Muungano, alikuwa waziri mkuu pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali na ameona faida ndio maana mpaka leo yupo na anaendelea kupata mshahara kama waziri mkuu mstafu, haoni hayo ni matunda ya serikali ya Muungano?" alihoji.
Magoti aliendelea kudai: "Warioba anatakiwa kujua kwa sasa serikali ipo mikononi mwa vijana ambao hawataki Muungano uvunjike kama anavyofikiria yeye."
Mwanafunzi mwingine kutoka Zanzibar, Juma Juma, alisema kumekuwa na upotoshaji wa kuhusu maoni yaliyotolewa na wananchi wa Zanzibar kuwa wanataka Muungano uvunjike, lakini ukweli Wazanzibari wanachotaka ni kwamba Muungano uboreshwe kwa maslahi ya pande zote mbili.
"Katika kila nchi lazima wanakuwapo wasaliti na hawa wanatumia mbinu nyingi kuwahadaa wananchi ili wawaamini, Maalim Seif Sharif Hamad ameonekana kuwa msaliti na mpenda madaraka toka kipindi akiwa CCM mpaka hivi sasa, anatumia uongo wa dhahiri kwa wananchi katika mikutano yake kuhusu maslahi ya Zanzibar katika Muungano," alidai.
Juma alisema viongozi wanatakiwa kujua kuwa kuwapo Muungano ndiyo heshima iliyonayo Tanzania, hivyo kama Muungano ukivunjia, nchi itakosa heshima hiyo.
Tangu Jaji Warioba alipowasilisha Rasimu ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu, amekuwa akishambuliwa yeye binafsi na wanasiasa wa chama tawala-CCM na baadhi ya watu binafsi, wakidai anataka kuuvunja Muungano, ingawa tume hiyo ilikuwa na wajumbe 30.

source: mjengwa blog