WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, February 2, 2013

HOTUBA YA RAIS MWEZI JAN


jkk ba817

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JANUARY, 2013

Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi.  Siku ya leo nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia.  Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;

         Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.  Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini.  Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa ushirikiano.  Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010.  Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
         Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu.  Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji wa umeme.  Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
         Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa.  Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya.  Tumepongezwa katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi kuyaboresha.  Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa.  Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa.  Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli moja.
Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam.  Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo.  Katika maandamano yale na baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara.  Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote.  Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa. 
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili.  Leo mwezi mmoja baadae, napenda kusisitiza mambo mawili.  Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini.  Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
         Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.  Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo.  Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa.  Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini.  Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma.  Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza.  Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru.  Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita 56kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani).  Ujenzi wa kilometa 36 za mwanzo ulienda vizuri.  Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi hiyo kufariki.  Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia.  Sasa mambo yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi nzuri.  Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa imekamilika. 
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma.  Tumelikamilisha Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka umekamilika.  Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda Darajani umefikia  mahala pazuri.  Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa.  Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana.  Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea.  Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor”  kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi.  Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa.  Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi.  Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari huru.  Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru.  Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya.  Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo. 
Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68.  Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo.  Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji. 
Ndugu Wananchi; 
         Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri.  Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012 nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012.  Hali kadhalika mipango ya kujenga bandari ya Kilwa iko mbioni.  Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara.  Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi;
         Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta.  Nilisisitiza kwamba tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo.  Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika. 
Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo.  Hivi sasa katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa.  Kampuni ya PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara.  Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility Through Vocational Training.  Programu hii inalenga  kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi.  Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012. 


Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa.  Vile vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani.  Mchakato wa kuwapata wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea.  Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25. 
         Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa.  Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika mafunzo haya.  Wamepatikana watatu.  Wataalamu hawa na wengine wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta hii. 
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
         Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara.  Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa gesi.  Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na kadhalika.  Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi. 
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi.  Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya kujenga, waanze.  Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika.  Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na Watanzania kwa jumla.  Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.  
Ndugu Wananchi;
         Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji.  Kwa upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi.  Bahati mbaya wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa.  Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa inapotoshwa kwa makusudi.  Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka sasa.  Mchakato umefanyika wa kuchambua wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa.  Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji kuanza.  Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi.  Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha mbolea.
 Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika kipindi hicho.  Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine.  Katika kipindi hicho ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele.  Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
         Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili.  Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa.  Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji.  Hivyo, waliamua kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo. 
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na hati miliki nalo.  Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali ilikubali.  Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani.  Kesi ilichukua muda kusikilizwa na kumalizika.  Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo hilo. 
Kampuni nayo ilichukua muda kuanza.  Hivi sasa, timu yake ipo kwenye eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa.  Niliambiwa kuwa katika magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la mradi huu.  Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote.  Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli.   Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali.  Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
         Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu.  Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo.  Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo.  Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki.  Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo.  Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
         Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo.  Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha.  Kwa upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi.  Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi sasa. 


Ndugu Wananchi;  
         Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali.  Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini.  Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini.  Hiyo haitakuwa sawa.  Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine.  Ni kutokana na msimamo wangu huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali  katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa.  Kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.   


Ndugu Wananchi;
         Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika  za Serikali na Mashirika  ya Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013. 
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara.  Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu Uhuru.  Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri.  Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo.  Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
         Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua masuala mbalimbali.  Uvumilivu wao na uelewa wao npyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa ya kawaida.  Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo.  Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu.  Wajiepushe na maneno au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine.  Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
         Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa.  Nawapa pole waliofiwa na kujeruhiwa.  Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao.  Kwa kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na kuiba mali za watu.  Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki.  Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao.  Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo.  Sasa wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;  
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri.  Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza!

Friday, February 1, 2013

Tujifunze kutoka makosa ya wengine, tusisubiri yetu



NIMEKUWA nikisema, na sijachoka kusema, kwamba tunatakiwa kujenga taifa kubwa, na nimekuwa nikisisitiza kuhusu sifa za taifa la aina hiyo, sifa zinazotofautisha baina ya nchi kubwa yenye taifa dogo ndani yake na nchi ndogo yenye taifa kubwa ndani yake.
Sifa hizo ni nyingi, baadhi zikiwa ni kubwa na nyingine zikiwa ni ndogo, nami nimekuwa nikizijadili, pamoja na kujadili sifa zinazofanya taifa kuwa dogo hata pale linapokuwa ndani ya nchi kubwa, kama Kongo mathalan. Sifa moja inayoifanya nchi yo yote isiweze kujenga taifa kubwa, hata kama nchi yenyewe ni  kubwa kama Kongo, ni uroho wa watu wake na watawala wake.
Haitawezekana aslani kwa nchi yo yote, hata ingekuwa kubwa kiasi gani na ikawa na utajiri wa El Dorado, kujenga taifa kubwa iwapo watu wake na watawala wake ni waroho, walafi, waporaji, wanyang’anyi, waongo, wanafiki na mabazazi. Kila nchi ina watu wa aina hii, na ni haki ya kila nchi na kila taifa kuwa nao, lakini wakiwa ndio wengi zaidi kuliko watu wema nchi hiyo haiendi ko kote.
Nimesema pia kwamba nchi inayotarajia kujenga taifa kubwa haina budi kujenga misingi ya haki, usawa, mshikamano na upendo, tabia ya kujuliana hali na kusaidiana inapotokea shida, na pia uwezo wa kujua namna ya kugawana kile kinachopatikana kama riziki ya taifa bila kunyang’anyana kila kakipatikana kanyama kadogo.
Zogo linaloendelea kuhusu gesi asilia nchini linadhihirisha kwamba hatuna nia ya kujenga tafia kubwa na badala yake tumejifunga katika udogo wetu wa siku zote. Tunapoteza akali, mantiki inayeyuka, staha inatutoroka, adala inatuacha, na haya zinatuishia kwa sababu ya kanyama kadogo kama gesi asilia. Najiuliza, hali itakuwa vipi iwapo tutalaaniwa na kupata vitu vikubwa zaidi? Si tutamalizana?
Miongoni mwa sababu zinazotufanya kuwa taifa dogo ndani ya nchi kubwa ni nakisi ya utashi wa kujifunza kutokana na yale yaliyo ndani ya uwezo wetu kujifunza. Tumezungukwa na nchi zenye utajiri mkubwa ambao unawafanya wananchi wake na watawala wake waparurane, wakwaruzane, wachinjane kwa sababu ya utajiri huo. Sisi tunakataa kujifunza kutoka kwao, kana kwamba tunatamani tuwe kama wao.
Tunajua kwamba nchi hizo, pamoja na utajri mkubwa wa maliasili, ni nchi zenye wananchi mafukara kama Lazaro, na kwamba ufukara huo katikati ya utajiri mkubwa ndiyo kichocheo kikubwa cha uhasama na vita, lakini na sisi tunataka kwenda huko huko.
Tumeona kwamba wananchi wanapokuwa wamechoshwa na viongozi waroho wataasi tu, hata kama majeshi yatasambazwa katika kila kijiji na kila mtaa, nasi tunataka kwenda huko huko.
Aidha tumeona, na tunajua kwa sababu hili tumeliona mara kadhaa, kwamba suluhisho la matatizo yetu ni mazungumzo ya kutafuta maelewano, lakini tunaendelea kuamini kwamba tunaweza kumaliza matatizo yetu kwa matumizi ya nguvu, hasa pale inapotumika dhidi ya wananchi wasio na silaha. Tumeingia katika zahma kubwa, zahma isiyo ya lazima, kwa sababu tu tunakataa kufikiri kidogo na kuchukua hatua za kusawazisha mambo kabla hayajawa makubwa.
Mzozo kuhusu gesi na maliasili nyingine si jambo jipya kwa wale wanaojisumbua kuangalia nchi za wenzetu na kusoma na kuielewa historia ya dunia.Tatizo kubwa ni uongozi katika ngazi zote kutokuwa na umakini unaohitajika kukabiliana na changamoto zinazotokana na hii laana tunayokumbana nayo tunapopata neema ya kugundua utajiri.
Imefikia hatua kwamba wanadiplomasia wa nje nao wanatutanabahisha kuhusu maliasili na jinsi ya kuzishughulikia, kana kwamba sisi wenye hatujui nini tufanye. Namsikia balozi akituambia, “Hey, nyie, tahadharini na gesi na mafuta; vitu hivi ni hatari kwa watu kama nyie kwa sababu hamjakaa vizuri; vitawaumizeni!” Hii ni lazima kwa nchi yenye umri wa miaka hamsini u shey?
Tunaijua Angola? Tunaijua Nigeria? Tunazijua Kongo zote mbili? Tunaijua Nigeria? Tunaijua Equatorial Guinea? Tunaijua Gabon? Tunaijua Libya? Nini tumejifunza huko kote? Hekima inatufundisha kwamba ni vyema kujifunza kutokana na makosa yaliyopita… siyo makosa yako, bali makosa ya wengine, kwani ukisubiri kujifunza kutokana na makosa yako mwenyewe, gharama zake zitakuwa kubwa mno.
Wakuu wa serikali, wakuu wa siasa, mashirika mbali mbali na wananchi kwa ujumla, sote tunahitaji kutulizana na kufanya tafakuri ya lazima. Nilipodokeza kwamba mchakato wa ‘Katiba Mpya’ unaoendelea sasa ulikosewa kwa sababu ni sawa na kutanguliza mkokoteni mbele ya punda, inawezekana sikueleweka, lakini sasa tunaona athari zake.
Wakati ule nilisema kwamba kuna haja ya mjadala mkuu wa kitaifa ili kuweka misingi ya maelewano ya kitaifa kuhusu mustakabali wa nchi yetu. Hii ni rai niliyoitetea tangu wakati Rais Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995. Mara kadhaa nilisisitiza kwamba taifa letu limepoteza mwelekeo na linahitaji kuketi na kujitafuta. Bila shaka kwa nia njema, Mkapa hakuiona mantiki hiyo.
Niliirejea rai hii Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani, katika Barua Ndefu ya Wazi kwake (sikuzungumza naye ana kwa ana jinsi nilivyozungumza na Mkapa), lakini naye hajaliona hili, na badala yake ameanzisha mchakato wa kupata ‘Katiba Mpya.’
Bado nasisitiza kwamba hatujajiweka sawa, hatujatulizana, hatujaelewana na hatujaridhiana na hatujaafikiana. Mengi tunayoyafanya tunayafanya kwa kupuyanga, alimradi liende, ilhali tukijua kwamba haliendi. Uwezekano wa kuumia huko tuendako ni mkubwa mno, hususan iwapo tutapata bahati mbaya ya kulaaniwa kwa mkosi wa kugundua mafuta ya petroli.
source: Raia mwema:Jenerali Ulimwengu

Hoja ya Mbatia yaliteka Bunge


NA RESTUTA JAMES

Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia,
Bunge jana lilijigawa vipande viwili kati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao waliunga mkono mapendekezo ya serikali kwa upande mmoja dhidi ya wabunge wa vyama vya upinzani waliokuwa wakiunga mkono hoja ya mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, kwa upande mwingine.

Tofauti hizo za kiitikadi na kivyama zilijidhihirisha baada ya Mbatia kuwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta ya elimu nchini. Tofauti hizo za wabunge zilijitokeza mapema baada ya Mbatia kutoa hoja yake na kuungwa mkono na wabunge wa upinzani pekee.Hoja ya Mbatia ilileta tofauti zaidi pale alipohitimisha kwa kuliomba Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza kwa kina udhaifu wa kimfumo katika sekta ya elimu nchini ambayo pia itapendekeza hatua za kuchukua ili kuinusuru sekta ya elimu.Alisema utafiti alioufanya kwa miaka 17 sasa umebaini kwamba sekta ya elimu ina udhaifu mkubwa kuanzia kwenye sera, mfumo rasmi wa elimu, mitaala, mihtasari na udhaifu katika vitabu vya kiada na ziada.Alisema matatizo hayo yana harufu ya ufisadi kwa kuwa vitabu vinavyotumika nchini ambavyo vimethibitishwa na kupewa ithibati vina makosa mengi ambayo kimsingi, yanadidimiza elimu.Alisema hata nyaraka za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zilizoandikwa kwa Kiswahili zinaonyesha kwamba malengo ya elimu ni 10 wakati malengo yaliyoandikwa kwa Kiingereza tisa na malengo ya elimu ya msingi kwa lugha hiyo yameainishwa kuwa ni 18, lakini kwa Kiswahili ni 10 pekee.Mbatia alisema tangu Tanzania ipate uhuru, haijawahi kuwa na mitaala ya elimu na kuitaka serikali iwasilishe bungeni kama ipo.Alisema inasikitisha kwamba baadhi ya vitabu vilivyopewa ithibati mwandishi mkuu, mhariri mkuu na msomaji mkuu ni mtu mmoja, jambo ambalo halikubaliki kitaaluma.Alisema tatizo hilo la kitaaluma linachangiwa na mgongano wa kimaslahi kati ya watendaji wa kamati inayotoa ithibati ambao nao ni waandishi wa vitabu ya kiada na ziada.Alisema elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hailengi kulikomboa Taifa na kuwajengea walengwa uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya kuhitimu.Alisema Sera ya Elimu ya Taifa inayotumika kwa sasa imekuwapo kwa muda mrefu na kwamba kuna haja ya kuifanyia tathmini ili kuangalia nini kimetekelezwa na nini hakijatekelezwa na kujirekebisha kulingana na mahitaji ya sasa. Alisema masuala mengi ya kisera katika elimu yanayotekelezwa nchini, yametokana na masharti yanayotolewa na vyombo vya kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).Alitoa mfano kwamba miaka ya 1980 vyombo hivyo viliitaka serikali ipunguze matumizi ya rasilimali za umma katika kugharamia huduma za jamii ikiwamo elimu, jambo ambalo limechangia uduni wa shule za umma nchini.Alisema vyombo hivyo pia viliwahi kuielekeza serikali ielekeze zaidi rasilimali katika elimu ya msingi tu kwa maelezo kwamba elimu ya juu ni anasa na katika miaka ya hivi karibuni vimebadili ushauri huo na kudai rasilimali zaidi zielekezwe katika elimu ya juu.Alisema serikali imekuwa ikikubali maelekezo yote hayo jambo lililopelekea nchi kuwa jalala la sampuli bila kuangalia ubora wa sera hizo na matunda yake kwa taifa.Alisema rasimu mpya ya sera ya elimu ambayo inaandaliwa inaeleza kwa ujumla maana ya mtaala kwamba ‘Ni jumla ya mambo ambayo mlengwa anatakiwa kuyapata katika mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa lengo la kufikia matarajio ya jamii na taifa’.Alisema nchi zote duniani wazazi au walezi wa kila mtoto wana haki ya kujua mitaala ya masomo husika ya shule na kwamba vyombo vya elimu huwajibika kumpatia kila mzazi au mlezi nakala ya mtaala, jambo ambalo nchini halipo.“Mihutasari yote iliyopo inaonyesha kwamba, kama taifa tumeshindwa kutofautisha madhumuni na malengo ya elimu ya Mtanzania,’’ alisema Mbatia. Alisema kamati ya wizara inayotoa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada (EMAC), imeshindwa kutekeleza wajibu wake kama ipasavyo na kusababisha mafuriko ya vitabu vinayopotosha dhana ya elimu kwa kuthibitisha vitabu vingi vya  kiada vikiwa na makosa mengi ya kitaaluma.Alisema mwaka 2009 kupitia mpango uitwao ‘Teaching and Learning Materials Programme (TLMP)’ Tanzania ilipata msaada wa dola za Marekani milioni 13 (Sh. 20,400,000,000) kutoka Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), kwa ajili ya kuandika na kuchapisha vitabu na kugharamia vifaa vya kufundishia masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na Biolojia kwa idadi ya vitabu 2,250,000.Alisema inatisha na kusikitisha kutokana na vitabu vilivyochapishwa kwa kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilipata uwezeshwaji wa jopo la wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha South Carolina cha Marekani.“Mathalani, katika vitabu vya ‘Mathematics for Secondary Schools, Volume I, II, III and IV’ vilivyoratibiwa na EMAC; kama inavyoonekana kwenye utangulizi wake, mwandishi mkuu ndiye huyo huyo mhariri mkuu na mhakiki mkuu. Taaluma na maadili ya uandishi wa vitabu, inazuia mtu kuandaa, kuhariri na kuhakiki andiko lake mwenyewe. Wataalamu walioshiriki kuandaa vitabu hivyo walikuwa na majukumu mengi ikiwamo kuandika, kuhariri na kuhakiki vitabu walivyoandaa wenyewe chini ya uratibu wa EMAC,’’ alisema Mbatia.Alisema utaratibu huo ulitumika pia kwa wataalamu wa masomo mengine yote yaliyoandaliwa wakati huo chini ya uratibu wa EMAC na tayari vimepewa ithibati.“Elimu iliyopangwa kwa sera bora na mitaala bora pekee yenye mihitasari na vitabu vilivyotayarishwa kwa umakini mkubwa na uadilifu ndiyo yenye uwezo wa kujenga Taifa la watu waadilifu, wazalendo, wachapakazi, watambuzi wa haki na wajibu wao,” alisema.Alisema mfumo wa elimu uliopo unatia wasiwasi ikiwa Tanzania itaweza kufikia Dira ya Taifa (2025) ya kuhakikisha mwaka huo, Taifa linakuwa na watu walioelimika kwa upeo wa juu.Alitahadharisha pia kwamba udhaifu katika sekta ya elimu utaisababisha nchi kushindwa kufikia lengo la pili la Milenia la elimu bora kwa wote.WAZIRI KAWAMBWABaada ya Mbatia kuwasilisha hoja yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliwasilisha maelezo ambayo pamoja na mambo mengine, alilitaka Bunge kutounda kamati teule kwa kuwa serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya elimu ambayo itaainisha mitaala na mihutasari.Alisema mfumo wa elimu wa Tanzania una mitaala na mihutasari na kwamba siyo kweli kuwa hakuna mitaala. Alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi lakini serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuiboresha kama kununua vifaa vya kufundishia, kujifunzia, kuandaa walimu na kujenga madarasa ya kutosha.Alisema sekta ya elimu inaongozwa na sera kubwa tatu ambazo ni sera ya elimu na mafunzo (1995), sera ya elimu ya ufundi na mafunzo (1996) na ile ya elimu ya juu (1999).Alisema mwaka 1997 serikali ilianzisha programu ya maendeleo ya sekta ya elimu iliyowezesha kuongeza fursa za utoaji wa elimu, ubora, usawa wa kutoa elimu na kuimarisha mbinu za uongozi, utawala na ugharimiaji wa elimu.Alisema sera hizo pamoja na programu hiyo zimesaidia ongezeko la shule za msingi, sekondari, vyuo vya elimu ya ufundi, vya ualimu na vyuo vikuu.Alipinga hoja ya Mbatia kwamba sekta ya elimu inaongozwa bila mitaala rasmi na kusema kwamba ipo na pia mihtasari.Alisema serikali imeanza kufanya mapitio na marekebisho makubwa ya sera ya elimu na mafunzo ya ufundi.“Naomba Bunge lako Tukufu liitake serikali kuzingatia hoja zilizotolewa kwenye hoja hii (ya Mbatia) na kuzifanyiakazi kwa kina wakati ikikamilisha mapitio ya sera ya elimu na mafunzo,” alisema.Pendekezo hilo la Dk. Kawambwa liliungwa mkono na mawaziri pamoja na wabunge wa CCM, jambo ambalo liliibua mvutano.Mbatia alipoulizwa kama anakubaliana na pendekezo la Waziri, alikataa akieleza kwamba ni kamati teule ya Bunge ndiyo itaweza kubaini kiini cha udhaifu katika sekta ya elimu.KITI  CHA SPIKA CHAYUMBAHata hivyo, kiti cha Spika kilionekana kuyumba baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyeanza kupinga uundwaji wa kamati teule akieleza kwamba Mbatia hajataja jambo mahsusi ambalo litachunguzwa na kamati hiyo.TUNDU LISSUMbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliomba mwongozo kupitia kanuni ya 57 (7), na kukumbusha kwamba kanuni za Bunge zinaeleza kwamba badiliko lolote halipaswi kupingana na hoja ya msingi, lakini pendekezo la waziri linataka kuondoa hoja ya kulitaka Bunge lisiunde kamati teule.Hata hivyo, hoja ya Lissu ilipingwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, ambaye aliomba wabunge wakubali hoja ya serikali ili ikamilishe kazi ambayo ilikuwa imeanza.WAZIRI LUKUVIWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alilitaka Bunge kukubali mapendekezo ya serikali na kuahidi kwamba hoja za Mbatia zitazingatiwa katika mchakato huo. Alisema serikali haijadharau hoja ya mbatia na kwamba mapendekezo yake ni mazuri na ya msingi.Hata hivyo, alipinga uundaji wa kamati teule kwa maelezo kwamba haitaweza kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa Mbatia amezungumzia mambo mengi.Maelezo ya Mbatia yaliwainua wabunge wengi wa upinzani ambao walikuwa wakipinga pendekezo la serikali.OLE SENDEKAMbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema hoja za Mbatia ni za msingi, lakini Bunge haliwezi kuunda kamati teule kwa kuwa hoja imetaja mambo mengi ambayo hayawezi kuchunguzwa na wanasiasa hasa suala la mitaala ambalo ni la kitaalamu.MCHUNGAJI MSIGWAMbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alitaka Bunge lifanye kazi yake ya kuisimamia Serikali badala ya kuondoa hoja ya Mbatia; akitahadharisha kwamba elimu ni gharama na hivyo ni lazima nchi igharamie sekta hiyo.FELIX MKOSAMALIMbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema ibara ya 117 ya kanuni za Bunge inaeleza kwamba Bunge linaweza kuunda kamati teule kuchunguza jambo mahsusi na kwamba hoja ya Mbatia ndilo jambo mahsusi la kuundiwa kamati.NAIBU SPIKANaibu Spika, Job Ndugai, alisema kamati teule ingeweza kuundwa kama Mbatia angekuja na hoja mahsusi moja.JOSHUA NASSARIMbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema kupinga hoja ya Mbatia kunadhihirisha kwamba wabunge wanakimbia kazi yao ya kibunge ya kuisimamia serikali.Alisema mfumo wa elimu ni mbovu ndiyo maana vyuo vinazalisha watafuta ajira badala ya wazalisha ajira.Baada ya mvutano wa muda mrefu, Spika Makinda aliamuru hoja hiyo iamuliwe kwa kura za ndiyo na hapana na wabunge wengi wakaunga mkono pendekezo la serikali.MOSES MACHALIMbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alipinga pendekezo la serikali na kusema kwamba serikali inahofu ya kuundiwa kamati teule kwa sababu ina mambo inayaficha.SUZAN LYIMOMbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo aliitaka serikali kueleza bayana ni lini itarekebisha hali hiyo kwa kuwa sekta ya elimu ni kama ipo chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU).Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba hoja ya Mbatia ya kutaka iundwe kamati teule ni ya msingi kwa sababu kuna upotevu mkubwa wa fedha zikiwamo Sh. bilioni 20 za wafadhili zilizotolewa kwa ajili kuchapisha vitabu.JABIR MAROMBWAMbunge wa Kibiti (CCM), Jabir Marombwa, aliunga mkono mapendekezo ya serikali na pia hoja ya Mbatia na kuitaka serikali kuzingatia mambo yote ya msingi yaliyoainishwa kwenye hoja hiyo.MARGARET SITTAMbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, alipendekeza kuwa tume ya utumishi wa walimu irudishwe wizarani kwa kuwa ilipoondolewa imeathiri sana kada ya ualimu. Hoja hiyo itahitimishwa leo kwa Waziri Kawambwa na Mbatia kutoa maelezo ya kuhitimishwa.
CHANZO: NIPASHE

MUUNGANO UKIVUNJIKA NINI KITATOKEA?



seif 43e19
Katika mfumo gandamizi watawala wakitumia system zao za propaganda potofu wameweza kuteka fikra za watu kwa sababu maalumu za kulinda nafasi zao: Ukisema ukweli mweupe usiokuwa na doa hata chembe moja, basi utaambiwa aidha wewe ni Mchochezi au una Jaziba! Haya maneno mawili ni silaha kubwa sana ya tawala gandamizi kote duniani, na maneno haya yamesaidia sana
kuwadhibiti wale wote wanaopenda kudai haki zao au haki za watu wengine. Watawala wanapowagandamiza raia hawaelewi kabisa kwamba wao ndiyo wanaoweka jiwe la msingi wa Uchochezi, lakini wale wanaoonewa na kugandamizwa wanapotaka kujinasua toka mikononi mwa wagandamizaji, tayari wameshaonekana wanataka kutoka, hivyo neno linalotumiwa ili kuwadhibiti ni “Uchochezi” ! Sasa mchochezi hapo ni nani!? Mchochezi ni yule anayeukataa Ugandamizaji, au Mchochezi ni yule Anayemgandamiza mwenzie!? Hapa huhitaji kusomea sheria ili ujibu maswali haya.
Wakati wa utawala wa Idd Amin waandishi wa habari walioandika kwamba Amin anauwa watu; utawala wake uliwaita waandishi hao kwamba ni wachochezi! Viongozi wa kidini waliokemea mauaji ya Idd Amin waliambiwa wana ni Wachochezi na wana Jaziba! Jella anaposema nchi hii kuna mbegu mbaya ya udini ambayo inaharisha amani ya nchi hii; anaambiwa aache Jaziba!  Na wakati mwingine anaweza kutokea mwanasiasa akasema niache Uchochezi!
Mwaka 1990 kuna mcheza sinema mmoja wa Kimarekani Spike Lee alicheza sinema inayoitwa “Do the Right Things”, sinema hii inaonyesha jinsi mfumo gandamizi ulivyokuwa unawagandamiza watu weusi na kujiona kwamba wapo sahihi kufanya hivyo; na watu weusi nao badala ya kufuata taratibu za kisheria, wao wakaamua kupata haki kwa kutumia nguvu; na katika mazingira kama haya wote walipoteza: Wagandamizaji na Wagandamizwaji! Ndiyo maana sinema hii inatufundisha kwamba kila mtu afuate sheria; watu wote wapo chini ya sheria moja bila ya kujali imani za dini zao, rangi zao, elimu zao, kazi zao, makabila yao, uwezo wao kifedha au nyadhifa zao.
Kutumia Maneno ya Jaziba au Uchochezi tukidhani ndiyo tunadumisha Amani na Utulivu kama tulivyozoea kusema; tutakuwa hatupo sahihi asilimia mia moja; bali usahihi ni kutafuta chanzo cha tatizo na kuangalia ni namna gani tunaweza kulitatua bila ya kuidhuru jamii inayotuzunguka.
Wote tumezaliwa hapa hapa, tumesoma hapa hapa, tunaishi hapa hapa, tunafanya kazi hapa hapa, tunazeekea hapa hapa, tutastaafu hapa hapa, tutafia hapa hapa, na tutazikwa hapa hapa, lakini hatujui mambo ya hapa!
A. Ukishabikia Udini, ukajiona kwamba dini yako ni bora kuliko dini zingine, basi jua kwamba Dhehebu lako halikubaliki!
B. Ukishabikia Dhehebu, ukajiona dhehebu lako ni bora kuliko madhehebu mengine, basi jua kwamba Kabila lako halikubaliki!
C. Ukishabikia Ukabila, ukajiona Kabila lako ni bora kuliko Makabila mengine, basi jua kwamba Elimu yako haikubaliki!
D. Ukishabikia Elimu, ukajiona Elimu yako ni bora kuliko Elimu za wengine, basi jua kwamba kazi zako hazikubaliki!
E.  Ukishabikia Kazi, ukajiona Kazi zako ni bora kuliko kazi za wengine, basi jiandae kwa lolote, na kwa wakati wowote kwa vile Wanakitengo wapo kazini watakutafutia tu sababu na watakubana!
Dr. Jella
source: mjengwablog.com

Mbowe ambana Pinda bungeni



Mboye 

SAKATA la gesi limetua rasmi bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuitaka Serikali iweke hadharani mikataba ya utengenezaji wa bomba la kusafirishia gesi hiyo kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ili kuondoa usiri uliogubika mradi huo.
Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda maswali bungeni katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu.
“Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kuwa vurugu za Lindi na Mtwara zimesababishwa na mawasiliano hafifu kati ya Serikali na wananchi, ikiwamo kauli za viongozi wa Serikali na CCM je, ni kwa nini Serikali isiwachukulie hatua za uwajibikaji watumishi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanaonekana dhahiri kuhusika,” alihoji Mbowe.

Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka Waziri Mkuu kueleza ni kwa nini Serikali isiweke wazi mikataba yote ya gesi ili kuondoa hofu iliyojengeka kwa wananchi kwamba kumekuwa na hali ya ufisadi.

Akijibu swali hilo, Pinda aliwataka wabunge kutumia utaratibu mzuri wa kupata mikataba hiyo akisema haiwezekani ikawekwa hadharani.

Mbali na jibu hilo, Pinda alivitupia lawama vyama vya siasa akisema vimechangia kwa kiasi kikubwa mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Licha ya juzi kueleza kuwa kulikuwa na mgogoro wa viongozi ndani ya mkoa huo pamoja na CCM, jana alikwepa swali la kutaka wahusika wawajibike na badala yake akasema suala hilo liko juu yake.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali lingine la Mbowe ambaye alimtaka Pinda kutoa kauli juu ya nani aliyesababisha mgogoro wa Mtwara uliosababisha maafa.

Hata hivyo, alitangaza neema kwa waathirika kwamba Serikali inaangalia namna ya kuwapunguzia gharama wale wote waliopatwa na matatizo hayo ikiwamo kuwalipa fidia.
“Vyama vya siasa vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupotosha jambo hilo, ushindani wa chaguzi zinazokuja umejitokeza pia,” alijibu Pinda.

Kiongozi huyo alisema wanaofanya uchochezi huo wanafanya bila ya kujua kwamba unaweza kuwakumba watu wote wakiwamo hao wanaofanya hivyo.
“Tutalaumiana wengi lakini ni vyema kuweka mambo hadharani na kwamba ni hatari kufanya mambo kama hayo kwani amani ya nchi ni lulu ambayo ikipotea inaweza kuwa tabu kuipata.”

Alipinga hoja ya Mbowe kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya shinikizo na maandamano ya wanasiasa.
Alilieleza Bunge kuwa wananchi wa Mtwara wanaweza kupoteza fursa nyingi kutokana na wawekezaji kuanza kuondoka wakikwepa vurugu na kukimbilia Msumbiji ambako kuna dalili za gesi pia.

Kamati ya Makinda yayeyuka
Jana, Spika wa Bunge Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa Kamati aliyotarajia kuiunda haitakuwapo kutokana na ukweli waliokuwa wakiutaka kutoka Mtwara kuelezwa na Waziri Mkuu. 
Akiahirisha Bunge mchana wa Januari 29, mwaka huu, Makinda alitangaza kuwa angeunda kamati ya Bunge kwenda Mtwara kuangalia mgogoro huo.
“Kutokana na ukweli uliotolewa na Waziri Mkuu leo bungeni, naomba nimshukuru sana kwa dhati kwa kulishughulikia tatizo la Mtwara, lakini nieleze kuwa nilikusudia kuunda tume kwa ajili ya kwenda kutazama suala hilo, lakini tayari tumepata ukweli hivyo naona haina haja ya kuunda tume hiyo,” alitangaza Makinda.

Moto bungeni
Hoja binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia inayokosoa mfumo wa elimu Tanzania kwa shule za msingi na sekondari kuwa ni dhaifu na hauleti matumaini kwa wanafunzi, ilizua mjadala mzito bungeni jana baada ya Serikali kukataa pendekezo lake la kuunda kamati maalumu ya kutafuta chanzo cha tatizo hilo.

“Kutokana na hayo, ninaliomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kina cha udhaifu huo wa kimfumo katika sekta ya elimu hapa nchini na kupendekeza hatua za kuchukua ili taifa liondokane na aibu ya udhaifu huo,” alisema Mbatia.

Baada ya hoja hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipangua hoja moja baada ya nyingine na kuliomba Bunge lisikubali kuundwa kwa kamati teule, bali liiagize Serikali kushughulikia suala hilo.

Baada ya Dk Kawambwa kutoa hoja hiyo, Mbatia alisimama na kuikataa akisema kile alichokiainisha juu ya udhaifu hakifanani na kutaka kuundwa kamati kupitia kila hatua yenye udhaifu.

Baada ya Mbatia kusema hayo, ulizuka ubishi baada ya Spika Makinda kutaka kujadiliwa kwa mabadiliko ambayo Serikali inataka au hoja ya Mbatia iendelee.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kuna kila sababu ya kuunda kamati lakini iwe teule ya Bunge.
“Tunatakiwa tujadili kwanza hoja iliyoko mezani na si kujadili mabadiliko ya hoja Mheshimiwa Spika, hoja aliyotoa Mbatia isibadilishwe kwa kuwa ni kinyume na kanuni za Bunge lako tukufu,” alisema Lissu.

Baadaye walisimama wabunge zaidi ya watatu wakitaka kuchangia lakini Spika Makinda alitoa nafasi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ambaye alisema: “Tukiunda tume itachukua muda... Hoja iliyotolewa na Mbatia ni ya msingi, sasa kamati za Spika zishirikiane na Wizara ya Elimu kufanya kazi hiyo.”

Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje alisema haiwezekani Bunge likakubali Serikali ijichunguze yenyewe kwa kuwa ni kitu ambacho hakikubaliki na ni kinyume cha kanuni za Bunge.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM) alisema kuna matatizo katika sera, mitalaa na muhtasari na kusema sasa ni kazi ya Bunge kupata tume stahiki..

source: mwananchi