WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, August 27, 2015

DR. JOHN POMBE MAGUFULI VS MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA

 


MACHO YETU YANAWANGALIA DR.MAGUFULI VS MHESHIMIWA LOWASA NA TANZANIA TUNAYOITAMANI BAADA YA UCHAGUZI 2015

JE KIONGOZI GANI KATI YA HAWA WAWILI NI:
 •  MWADILIFU
 •  MWAJIBIKAJI
 •  MKWELI
 •  MTETEZI WA AMANI
 •  RAFIKI NA MTETEZI WA WANYONGE
 •  SHUPAVU KATIKA MAAMUZI
 •  AWE TAYARI KUTUVUSHA KAMA TAIFA KUTOKA KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI
 • MTU WA WATU
 •  MKUZAJI WA DEMOKRASIA
 •  MWOGOPA MUNGU
 •  ANAYEWEZA KUKEMEA MAFISADI BILA WOGA
 
Taifa letu linaelekea katika uchaguzi wa viongozi ambao kupitia vyama vyao vya siasa wataunda serikali ya kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya uchaguzi wa October 2015.

Mimi jicho langu kubwa ni kwa kiongozi Yule ambaye atashika hatamu ya kuongoza Taifa letu na ambaye atahamishia makazi yake IKULU.


Kama taifa ni wakati mzuri umewadia sasa tuweze kumchagua mtu makini, mbunifu, mwaminifu, mwadilifu na mzalendo wa kweli kwa wananchi wanyonge na masikini wa Taifa letu.Kiongozi ambaye tunamwitaji lazima atambue kuwa kuwa wananchi wana haki ya kupata chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora bora huduma bora ya afya na usalama wa mali zao.


Akumbuke kuwa wanaompeleka Ikulu ni wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na sio marafiki wachache wenye pesa. Na ajue kuwa anapochaguliwa kuongoza, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri awe tayari kuongoza kwa kuonyesha njia awe ni mfano wa uwajibikaji.


Kiongozi tutakaye mchagua lazima awe na tabia ya kuongoza kwa kutofikiria zaidi maslahi binafsi wazo hili liwe mwiko. Tutataka atumie ustadi wa uongozi ambao utasimamia haki za waongozwa; wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.

Hatuki kumchagua kiongozi ambaye baada ya kuchaguliwa ataigeuza ikulu kuwa Ni pango la wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji wa rasilimali za watanzania kwa masilahi binafsi pamoja na marafiki wachache au chama chake.  Tunahitaji kiongozi ambaye uadilifu kwake utakuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku bila kujali au kupendelea mtu au kikundi cha watu au vile vile awe na uwezo wa kuwajibisha viongozi watakao kuwa chini yake wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kiongozi wetu tunataka aongoze katika misingi hiyo.

Kiongozi lazima ajue kuwa hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani ataongoza watu wake wateule. Tukiangalia katika historia ya dunia sehemu nyingi, Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na kubarikiwa katika njia nyingi. Walipomsahau Mungu kupitia rushwa na ufisadi na dhuluma shida na dhiki zilianza.
Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Kiongozi anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake unapatana na Neno la Mungu.

Itakuwa jambo bora tuweze kupata kiongozi Mkuu Raisin a viongozi ambao kwa kweli nao watakuwa bora katika kuongoza Taifa letu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila mtanzania. Tanzania ya leo inahitaji kiongozi  ambaye atawajibika; na kuonyesha uzalendo na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.Pengine katika msingi huu tutahitaji kiongozi ambaye anauelewa mpana wa kuelewa shida za wananchi mwenye UWEZO wa kufikiri kwa usahihi, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa usahihi wakitambua dhamana ya uongozi ambao taifa linampa. Kwa hivyo tutahitaji  RAISI pamoja na mambo mengine awe na UWEZO kuongoza kwa usahihi. 


Vile vile tunahitaji viongozi wajao katika serikali zetu mbili wawe ni watu wa WATU; viongozi ambao wataweza kuona matatizo ya wananchi wao ni yao na yanawakera na hata kuwanyima usingizi, hivyo itakuwa jukumu lao kuongeze nguvu ya uwajibikaji wa kusimamia rasilimali za Taifa. Nasi kama wananchi tuwe na uwezo wa kuwapima kwa watakacho kifanya wakiwa madarakani.

Pengine tutahitaji kidogo aina ya viongozi wetu wawe wakali japo sio sahihi kutumia msemo huu lakini wakati mwingine ile tuweze kupiga hatua ya maendeleo tutahitaji viongozi wenye mawazo ya  uwajibikaji chanja; ili tuweze kubadilisha kidogo maadili ya utendaji wetu wa kazi kwa  Watanzania; Tunahitaji  Maraisi katika serikali zetu mbili ambao wanaweza  kuwawajibisha mara moja watendaji wake ambao wanashindwa kuwajibika, tuwapate viongozi ambao wanaweka pembeni huruma ambazo hazina msingi kwa Taifa;

  
Nafikiri itakuwa ni jambo la busara kama sisi kama watanzania na wapiga kura tukiweza kuepuka tabia ya kuwachagua viongozi wetu kwa  Mazoea, Mkumbo na kwa kutumia Hisia na mapenzi binafsi juu ya wagombea au chama. Nafikiri umefika wakati tuwachagua viongozi wetu kwa upeo wao wa kuona mambo mbalimbali nauwezo wao wa uongozi kama kiongozi na sio kama chama, hapa nazungumzia uzoefu wa kiongozi kabla ya kuchaguliwa kuwa raisi je amefanikiwa kwa kiasi gani katika idara ambayo amewahi kuongoza? Ana mzigo gani wa hisani ambao anatakiwa arudishe baada ya kuchaguliwa.

kama taifa tunafahamu kuwa taifa letu bado linaogelea sana katika tope nzito la matumizi mabaya ya rasilimali ya Taifa Rushwa na Ufisadi vimekuwa ni wimbo wa kila siku. Tumeendelea kuona jinsi pesa za walipa kodi zikipotea na tumeendelea kuona jinsi umasikini wa watanzania ukiendelea kuongezeka.

Basi tunahitaji Raisi ambaye analiona hili kuwa ni tatizo na linahitaji utatuzi wa haraka. Lazima tukubali kuwa mabadiliko yoyote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yenye kulenga kuletea faida wananchi walio wengi hayawezi kufanikiwa bila ya kutokomeza rushwa na ufisadi. Kiongozi wetu aweze kuliona hili na kuwa tayari kupambana nalo akiamini kuwa Tanzania rushwa imeshaota mizizi, NA TANZANIA BILA RUSHWA INAWEZEKANA.

Nafahamu mamilioni ya watanzania wamepoteza matumaini na hali zao za maisha lakini kupitia yeye ataweza kulitatua tatizo hili na kuwachukulia sheria wale wote ambao wamehusika katika uchafu huu,


Tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kufanya kazi na watanzania na kuendelea kuwaelimisha kuwa ni jukumu la mtanzania mmoja mmoja kuwajibika kwa vitendo na kupunguza kulalamika kila siku kama Mheshimiwa Yusuph Makamba alivyowahi sema kuwa “maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao wenyewe, kwa kufanya kazi. Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba kila kitu wanategemea kitafanywa na serikali … Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,”. Kauli hii ni nzito kiongozi wetu anayetaka kuongoza taifa hili lazima awe tayari kuwaeleza wananchi bila kuogopa kukosa kura katika kipindi kingine cha uchaguzi kuwa uvivu ni adui wa maendeleo.


Daima tunapofikiria kuwachagua viongozi wa juu wa Taifa letu tunayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa  Mwalimu Nyerere aliwahi sema kuwa kazi ya uraisi ni ngumu na inahitaji busara na kuchukua maamuzi magumu, ili kuweza kutimiza haki wananchi wanyonge “ walala hoi ”; aliendelea kushauri kuwa “Ole wale wanaokimbilia Ikulu, wanakimbilia nini, Ikulu hakuna biashara ya kufanya, Ikulu ni mahali patakatifu na kama kuna mtu anadhani kuwa kukaa Ikulu ni raha basi angeniuliza mimi katika kipindi cha miaka 21 niliyokaa Ikulu nimefanya biashara gani,Ikulu ni mzigo mzito”


Mwandishi Nyenyembe aliwahi andika kuwa “Kwa maana hiyo mtu anapoamua kuulilia uraisi;uraisi sio pambo la nchi,uraisi ni jalala, uraisi ni chumba cha kuhifadhia maiti,uraisi ni njaa,uraisi ni magonjwa,uraisi ni bakuli la kukingia machozi ya watu wanyonge wanaolia kila siku wakihitaji msaada na kama hawapati anayetazamwa hapo ni raisi”

Katika demokrasia wananchi ndio wenye dhamana na uwezo wa mwisho wa kumrejesha mwanasiasa kuendelea kuhozi madaraka; pamoja na umaarufu wake, uadilifu na utaalam katika kushughulikia maswala ya siasa bila ridhaa ya mwananchi sio rahisi kurejea madarakani; Hebu tuanagalie historia ya vyama vingi na chaguzi za Zambia zinaainisha kwa ukomavu wa demokrasia ndani ya Zambia wananchi ndio wenye sauti ya mwisho wananchi wa Zambia wanapima na kuamua kulingana na utendaji wa viongozi wao na sio ushabiki wa vyama vyao;wamejitahidi sana kuweka nchi mbele vyama baadae.

Tukiendekeza sana kushabikia sana vyama ndilo linalotuponza sana na wakati mwingine kurudisha maendeleo yetu nyuma katika nchi nyingi za kiafrika; wananchi wanakumbatia zaidi chama na sio utendaji wa viongozi wa vyama vyao; pamoja na uganganianyi wa madaraka kwa baadhi ya viongozi waliomaliza muda wao.

Kama wananchi tunatakiwa kuanza kuangalia upya maamuzi yetu dhidi ya viongozi wetu; tunahitaji viongozi waadilifu na viongozi wa namna hii  wataweza kuchukua hatua kwa maslahi ya jamii kwa manufaa ya wote, na wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo kulingana na utaratibu wa nchi husika na kukendelea kukubalika kwako kwa masilahi ya wengi; Katika mfumo wa kidemokrasia wa serikali, ambapo nguvu ya utawala ina inapatika upya kila baada ya miaka mitano kama ilivyo katika nchi ya Tanzania ni wananchi ndio wenye dhamana ya kuwarejesha madarakani viongozi wanaowapenda kufuatia sera za vyama vyao na ubora wao.

Nchi ya Zambia imetufundisha kuwa  hakuna kiongozi anayemiliki watu, hakuna chama chenye hatimiliki ya kuongoza nchi Milele; au kuwa kikundi cha wananchi ambao wao matakwa yao lazima kila mwananchi akubaliane nayo;kama itakuwa hivyo basi kuna tatizo na wananchi katika nchi hiyo; wananchi mara zote wanategemea na wanataka  mabadiliko makubwa ya kiuchumi hawahitaji propaganda za chuki, wanahitaji kufaidi raslimali zao  wazambia walikuwa wanashangaa utajiri wote unaotokana na shaba unakwenda wapi? Pale ambapo hawakuridhika hawakuwa na papara walisubiri tu wakati ulipofika walimweka pembeni kiongozi na kumpa dhamana kiongozi mwingine. Lazima tukubali kuwa katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika  Zambia imekuwa na imeonyesha kwa vitendo kukabiliana na  changamoto za mabadiliko ya kisiasa kwa ustarabu mkubwa wenye tija kwa Taifa:

Maamuzi ya wananchi katika awamu tofauti Zambia umeendelea kuwashangaza viongozi walioko madarakani kuanzaia enzi  Kaunda, pamoja na ukongwe wake wa kutawala kwa miaka 27 hadi awamu ya Banda; Kiini cha msukumo huu nini? Wananchi wanatamani kupata maisha bora na kuwa viongozi wenye kiwango cha juu kabisa cha uadilifu kuweza kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo sio kwa nadharia bali vitendo;Viongozi wetu wa vyama vya siasa wamesahau kuwa, Kimsingi, raia huzaliwa wakiwa huru dhidi ya mikingamo ya kijamii, kwa lugha ya kitaalamu tabula rasa. Lakini mikingamo hii ya kijamii huingizwa katika fikra za wananchi kupitia itikadi na elimu ya siasa katika vyama ambavyo wanafuata; na wakati mwingine hata kupitia shule na sehemu za ibada.

Cha ajabu haitoshi kuivuruga jamii peke yake tumeona na tunaendelea kuona kuwa viongozi wetu wa kisiasa hapa nchini wamekuwa wakigombana kila mara katika mambo ya msingi na yasiyo na msingi. Kugombana si kubaya kama kunaleta tija, lakini kule kugombana kunakofanywa kwa misingi ya kujitafutia umaarufu kunasabaisha viongozi kushindwa kutekeleza majukumu yao ambayo yanatokana na ahadi wakati wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, ni dhambi ambayo haiwezi kuvumilika hata kidogo. 

Wakati tunaelekea katika kipindi cha kuchagua viongozi wetu; sisi kama wananchi tuanze kujipima na kujua ni kiongozi wa namna gani tuna mwitaji; tuziangalie khali zetu za uduni wa maisha  sisi bado ni masikini, tunahitaji barabara bora; huduma za afya nzuri, elimu bora kwa vijana wetu; ajira za kutosha kwa wenye sifa za kuajiriwa; 


Kama Raisi John Kenedy wa Marekani alivyowahi kusema ‘Wewe UMELIFANYIA NINI TAIFA LA LAKO’ ni wajibu wa msingi kwetu kama wapiga kura kujiuliza swali hili je tumelitendea haki Taifa kwa kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya serikali zetu mbili? Yatupasa kutimizAa wajibu wetu kwa maisha bora kwa kila mtu kwa kuchagua viongozi bora na sio bora kiongozi. Miaka mitano ni mingi sana tukichagua viongozi mbovu.

Wananchi tujiulize je kama taifa  tumaini letu ni lipi dhidi ya viongozi wetu wa siasa ambao tunatarajia kuwachagua; tunahitaji viongozi wakuu wa nchi ambao wataweza  kutupeleka kwenye nchi yenye neema na amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa, kidini .

Niliwahi andika huko nyuma kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya tusiendelee;tukumbuke kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe, juhudi zetu na misimamo yetu;  tukiangalia kwa ujumla wanasiasa  wanapoteza muda mwingi katika propaganda na sio kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.

Wanasiasa wetu ndio wapiga majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia sisi wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya utamaduni wa siasa za Tanzania kwa kuwachagua viongozi watakao endeleza umasikini wa Taifa letu kwa faida ya wachache.

Kiongozi tunaemtaka tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda sisi kama Taifa. 

Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?


Taifa letu katika kipindi cha miaka ya karibuni kiliingia katika vurugu za Mtwara, Dar es salaam Zanzibar Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika; Je kiini cha vurugu hizi kimepata jibu? Kama jibu ni hapana sasa tutahitaji viongozi wetu wakuu tutakao wachagua wawe wanaweza kuona na kutumia muda wao katika kuleta majibu ya matatizo ya wananchi wao;Wananchi tunatakiwa tuamke na tusiwape nafasi wanasiasa kutufanya sisi kuwa  daraja la wao kuweza kutimiza malengo yao bila sisi kujitambua kwa haraka; matokeo yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunaendelea kuwa masikini.

Imefika wakati sasa hata viongozi wengine tutakao wachagua tusirudie kosa la kuchagua viongozi ambao wanasilka na tabia ya
kuzomeana, kulaumiana, kutukanana;mwelekeo huu hautatusaidia sisi kufikia lengo letu la kuwa na maisha bora

Nafikiri linalowezekana leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina na mikono ya Muumba wetu tu;

Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “Kupanga ni kuchagua”. Wananchi kwa kweli inatakiwa tujipange sasa kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa masilahi yetu binafsi ili kupata viongozi wetu wakuu walio bora na makini. Tunataka tupate viongozi waadilifu kweli kweli.

Tukumbuke kuwa Uadilifu ni karama, ya utambuzi wa kujifahamu kwa mtu binafsi hususa kiongozi wa serikali, ambaye anatakiwa kufanya kazi zake kulingana na sheria na taratibu ambazo hujenga, utamaduni, wa kuwajibika kulingana na  sheria husika. Kwa kufuata taratibu nzuri za utendaji kazi  Uadilifu katika kazi husaidia uimarishaji wa misingi ya utawala bora.

 

Kwa kujumuisha kabisa uadilifu na utimilifu kwa uhusiano wa biashara yetu inayoendelea na kufanya uamuzi, tunaonyesha kujitolea kwa utamaduni ambao unakuza kiwango cha uadilifu wa hali ya juu kabisa; ni kweli kuwa uadilifu inahitaji uaminifu binafsi wa kiongozi husika; uadilifu unahitaji  uaminifu wa kupinga ubinafsi kwa kiongozi ambaye amepewa dhamana. Uadilifu unaendana na Kuwa mkweli katika utendaji na kuishi kulingana na maadili ya kazi na kuheshimu rasilimali kwa faida ya wengine.

Wajibu wa kutenda ukweli ni wajibu wa juu kabisa wa uadilifu kwa viongozi wa umma; kiongozi wa umma lazima  atambue hali halisi ambayo inaendana na wajibu kwa kufuata maadili hivyo kusambaza cheche ili hata jamii nzima nayo iweze kuishi kulingana na maadili ya Taifa.

Kiongozi mwadilifu daima hutakiwa kuonyesha uhusiano kati ya maadili yake ya utendaji na kwa urahisi kabisa aweze kusema na nafsi yake ili  isitawaliwe na tama ya rushwa ambayo itapingana na dhana nzima ya maadili kulingana na kiapo chake. Hapa ni jukumu la serikali kuweka mipaka bayana wa uhusiano kati ya maadili binafsi na sheria za utendaji wake kwa manufaa ya umma. Uadilifu daiama huashiria haki, ikiwa na maana kuwa kiongozi wa umma lazima aweka maslahi binafsi pembeni;

Uadilifu hujenga amani, huleta ufanisi, kwani Watumishi wa umma watakuwa wanauwezo wa kuhakikisha matumizi sahihi, ufanisi wapesa za umma. dhana na misingi ya uwajibikaji anatarajiwa kufanya ya viongozi wa umma kuwajibika kwa matendo yao au kutotenda

Ni zinatakiwa kuongeza uwazi wa serikali, kusisitiza na kuimarisha mwitikio wa kiserikali na uhalali na kuboresha utekelezaji wa sera. Mwalimu Nyerere katika hija ya maisha yake, alijitahidi kutanguliza masilhai ya watu wake, bila ya kujikita katika ubinafsi, uroho na uchu wa madaraka; uchoyo na ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa viongozi wengi ndani ya Taifa letu.Maadili ni muhimu zaidi na katika siasa na kwa maendeleo ya wananchi. Maadili ya kweli yatapunguza wanasiasa kujishughulisha na rushwa. 

MUNGU IBARIKI JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA UTUVUSHE SALAMA ILI TUWEZE KUWAPATA VIONGOZI BORA KWA MANUFAA YA WATU WAKO KATIKA UCHAGUZI WA MWAKA 2015.


No comments:

Post a Comment