MWAKA 1976 nilikuwa mtoto wa miaka kumi
tu. Hata hivyo, nilikuwa na uelewa wa kujua baadhi ya mambo, likiwemo tukio la
kule Soweto, Afrika Kusini, yalipotokea mauaji makubwa, ya kutisha na ya
kusikitisha ya watoto wengi wa shule. Ilikuwa ni Juni 16, 1976.
Mauaji yale yamepelekea Juni 16
kufanywa kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika. Mwaka 1976 sikuweza kufikiri kuwa tukio
kama lile la Soweto lingeweza kutokea katika nchi niliyozaliwa. Juzi hapa, siku
moja kabla ya Juni 16, tumepokea habari ya mauaji ya kutisha kwenye viwanja vya
Soweto, Arusha.
Kuna watoto wamekufa pia. Na picha za
watoto waliojeruhiwa, tumeziona magazetini na kwenye runinga. Kama alivyotamka
AGP Said Mwema, kilichotokea Arusha kinaashiria vitendo vya ugaidi. Hivyo basi,
vilaaniwe na wote wenye mapenzi mema na nchi yetu.
Huu ni wakati pia wa kushikamana kama
Watanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kiimani. Maana, hapa
tulipo ni vigumu pia kujua hasa, kama taifa, adui wetu ni nani na anatoka wapi!
Tuviachie na tuvipe ushirikiano vyombo vya mamlaka ili vifanye uchunguzi wa
kina juu ya kilichotokea Arusha. Vifanye hivyo ili vije na ukweli wa
kilichotokea, na hivyo kutupunguzia hofu ya ugaidi kwa raia wa nchi hii na hata
wageni wa kutoka mataifa ya nje.
Nchi yetu hii imekuwa na sifa ya kuwa
na amani na utulivu. Hakuna shaka yoyote kwamba sisi Watanzania kwa ujumla
wetu, ni watu wenye kupenda amani. Tusikubali wachache wapandikize mbegu za
chuki miongoni mwetu, na hata kufikia hatua ya kuvuruga amani yetu. Kutufanya
tuishi kwa hofu na hata kuhofia kukusanyika kwa pamoja kwenye sherehe zetu za
harusi na nyinginezo.
Wanadamu kwa kawaida, ni viumbe wenye
kutegemeana. Nimepata kuandika kuhusu Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre aliyepata
kusema: “Hell is the other people.” Kwamba jehanam ni wale wengine. Anataka pia
tukubaliane kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.
Kwa hakika kabisa, tofauti ya mwanadamu
na mnyama iko kwenye kufikiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu
anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndiyo maana ng’ombe anaweza kumpanda mama yake.
Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.
Kwa hiyo, mwanadamu kwenye mambo ya
msingi, hapaswi kabisa kuongozwa na hisia, ikiwamo ushabiki. Anapaswa kufikiri,
na zaidi kufikiri kwa bidii. Vinginevyo, ni ukweli kuwa kijamii, mwanadamu
anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye uhusiano wa kirafiki na kiadui na wenzake.
Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama
ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha,
mashamba, mapenzi na hata kivuli cha mti. Ndiyo, unaweza kabisa kuwakuta
wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa
kivulini.
Wanaweza kugombana hadi akatokea
mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Wanadamu hao watabaki
wakitazamana juani. Mara nyingi, migogoro husababishwa na kugombania kisichotosha.
Hivyo, lililo la msingi ni kutambua kuwa wanadamu tunategemeana.
Kwamba panapo kushindania jambo,
mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima
na busara. Kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya
pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano.
Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta
amani, panakosekana mazungumzo, basi, ina maana ya uwepo wa mazingira ya
kuvunjika kwa amani. Wanadamu sisi tumekuwa wepesi sana wa kunyosheana vidole
na hata kuhukumiana pasipo kudadisi ili kuujua ukweli.
Na hapa nawaletea leo kisa cha wanandoa
waliokaa miaka mingi bila kupata mtoto. Wakaamua wamfuge paka nyumbani. Naye
paka huyo wakampenda sana kama mtoto wa kumzaa. Paka naye aliwapenda sana bwana
na bibi nyumbani.
Ikatokea mke yule akapata mimba na hata
kuzaa salama mtoto. Ikawa kama miujiza. Furaha nyumbani ikaongezeka. Siku moja
bwana na bibi walimwacha mtoto wao amelala kitandani. Nao wakaenda zao
kuwasabahi jamaa na marafiki.
Walipokaribia nyumba yao wakati
wakirudi nyumbani, wakashtuka sana. Walimwona paka wao nje ya mlango akiwa na
kipande cha nyama mdomoni. Sura yake ilitapakaa damu pia. Wote wawili
wakachukua muchi wa kutwangia nafaka.
Kwa hasira wakamtwanga paka yule
kichwani. Alikufa papo hapo! Walipoingia chumbani, wakamkuta mtoto wao amelala
salama kitandani. Kando kuna nyoka mkubwa aina ya chatu. Nyoka amekufa baada ya
kujeruhiwa kwenye mapambano na paka. ‘Hell is the other people!’ Jehanam ni
wale wengine. Lakini hata pepo yaweza pia kuwa ni ya wale wengine. Nahitimisha.
No comments:
Post a Comment