Ndugu zangu,
Naanza kushiriki kuichambua rasimu ya KATIBAkwa kuangalia kipengelea Uchaguzi wa Rais.
Naam, Katiba ya Nchi inatakiwa pia
kuchangia kwenye kuondoa hofu zilizopo kwenye jamii husika. Kwa Nchi
Yetu, moja ya hofu hizo ni UDINI.
Nawapa alama 5 ambazo ni za juu
kabisa( Kwa Kipimo Changu) Wajumbe wa Tume Ya Katiba. Ni kwa
kutanguliza busara na hekima na kutuletea muarobaini wa Udini hapa
nchini kwetu.
TUME imefanya kitu kikubwa sana kwa
kupendekeza kuwa Mgombea Urais atangazwe mshindi anapopata asilimia 50
ya kura zote, hiyo kiufundi itakuwa 50 plus 1.
Tafsiri yake?
Huo ni muarobaini wa udini na hata
siasa za ukanda. Maana, hili la udini kwa kiasi kikubwa limechagizwa na
wanasiasa. Na sasa, ili mwanasiasa au chama cha siasa kiweze kuungwa
mkono na zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania itabidi kijinadi kwa
masuala ya kuwasaidia Watanzania bila kujali tofauti za dini zao au hata
kanda zao.
Maana, kwa nchi yetu, Mungu ameijalia
kwa kutokuwa na dini yenye waumini wanaofikia asilimia 40ya Watanzania
wote. Bado kuna wasio Wakristo wala Waislamu.
Hivyo, ili mgombea Urais aweze kufikia
asilimia 50, atahitaji kuungwa mkono na hata wasio wa dini yake. Na
akianza kuhubiri udini , basi, huyo ajihesabu kuwa atabaki kuwa ’ Rais’
wa Watanzania wa dini yake!
Kwa mara nyingine, pokea 5 zangu,
Tume ya Warioba kwa kuliona hili! ( Soma hapo chini nilichoandika
kwenye moja ya makala zangu kwenye safu ya Mraba wa Maggid, Raia Mwema)
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
Nilipata kuandika;
”Utaratibu huo unaua ukabila na
kujenga vema misingi ya Utaifa. Hata kama itachukua muda kufika mbali
zaidi katika hilo lakini Wakenya wameanza kuondokana na ukabila kwenye
siasa zao, kwa kupitia Katiba.
Kwa mantiki hiyo hiyo, Watanzania
tungeweza kabisa kuondokana na siasa za udini kwa kuweka, kwenye Katiba
yetu ijayo sharti la mgombea Urais kushinda kwa asilimia 50+1 ( Asilimia
50 jumlisha kura 1). Hilo lingewafanya wanasiasa wetu wenye kuwania
Urais na vyama vyao pia ‘ Kutia akili’.
Maana ingekuwa na tafsiri moja kuu;
kuwa mgombea na chama chenye kuendekeza udini kisingekuwa na nafasi ya
kutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wala nafasi ya kushika
dola. Maana, hakuna dini hapa Tanzania yenye idadi ya waumini wanaovuka
asilimia 50 ya jumla ya Watanzania.
Kwa maana, hiyo, muarobaini wa
kumalizana na udini uko kwenye Katiba ijayo, kama tuna nia ya dhati ya
kutoka hapa tulipo. Vinginevyo, udini huu tunaosema kuwa ni tatizo
tutakuwa tunaulea wenyewe.
Hata tatizo la siasa za ukanda nalo
litapotea, maana, hakutakuwa na mgombea au chama kitakachoweza kushinda
na kutoa Urais kwa kuegemea kura za kikanda. Hakuna kanda itakayovuka
peke yake asilimia 50 ya kura zote. Chama na mgombea kitahitaji kuungwa
mkono na wapiga kura wa kanda hata zilizo nje ya anakotoka mgombea
Urais.
Vinginevyo, kama alivyotamka Uhuru
Kenyatta kwenye hotuba yake nzuri iliyojaa utaifa hivi majuzi, kuwa
katika uchaguzi waliofanya, kila kura ilikuwa ina umuhimu. Hivyo, kila
kabila lilikuwa na umuhimu. Na Uhuru Kenyatta akaweka wazi anachotaka
Serikali yake kwa kushirikiana na Wakenya kufanya ili kuitoa Kenya hapo
ilipo na kwenda mbele.
Kenyatta alimalizia na maneno matatu; Forward, Foward. Foward!- Kusonga mbele!
Ndio, Wakenya wameamua; KENYA KWANZA!
And really, The Kenyans are coming, Big Time!”- Maggid Mjengwa, Raia Mwema.
And really, The Kenyans are coming, Big Time!”- Maggid Mjengwa, Raia Mwema.
No comments:
Post a Comment