Ndugu zangu,
Jana nikiwa viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa niliweza pia kuongea na baadhi ya wasomi wa Chuo hicho wakati tukiangalia mpira.
Mmoja wao alikuwa Mwalimu Mgaya
aliyeniambia kuwa anakwenda kuwa mwalimu wa historia.Hapo tukaingia
kwenye mada ya Daladala. Nikamwuliza kama anaijua historia ya Daladala.
Hapana, hajawahi kuisoma au kusikia mahali popote. Kwake yeye Daladala
ni Daladala.
Basi, akashangaa sana nilipomsimulia,
kuwa asili ya Daladala ni jina tulilolitohoa kutoka sarafu ya Marekani,
yaani, Dola. Nakumbuka kwenye miaka ya 80 mwanzoni , na katikati ya
shida kubwa ya usafiri Dar, nauli za usafiri wa vibasi vidogo vidogo
ikaongezeka na kufikia shilingi tano kwa safari. Ndipo hapo tuliweza
kumsikia konda akiita; " Kariakoo Dala ..dala..dala... dala!"
Maana, shilingi tano yetu iliyokuwa
nzito kidogo hata kuishika na yenye pembe sita ilikuwa na thamani sawa
na dola moja ya Marekani. Ndipo hapo, shilingi tano yetu ikabatizwa jina
la ' Dala'.
Jana jioni niliongea kwa simu na ndugu
yangu Mrisho Mpoto, nikamwuuzia wazo, kuwa siku moja tukutane
tulijenge wazo la kuwa na kitu kwa jamii kitakachotufanya tuzungumzie
tulikotoka kwa nia njema ya kukumbushana historia yetu. Jambo hilo
lingeenda sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Usafiri wa Mabasi yaendayo
kwa Kasi jijini Dar.
Maana, kuna mengi ya kutafakari
kuhusiana na uchumi na jamii yetu. Tujiulize; wakati wasafiri wa
daladala enzi hizo walikuwa ni watu wa kipato cha chini na hata cha
kati, je , wasafiri wa daladala wa leo ni watu wa aina gani?Je,
anayepanda daladala leo anatazamwa vipi; ni mtu asiye na uwezo kifedha
au anaweza kuwa ni mtu anayeona kuliacha gari lake nyumbani na kupanda
dala dala amefanya mawili; amebana matumizi na kuelekeza fedha zake
kwingine na hata kutunza mazingira. Maana, magari mengi mijini
yanachafua mazingira.Je, ni kwa nini uchumi wetu wakati huo ulikuwa na
nguvu kutuwezesha kubatiza sarafu zetu kwa fedha za kigeni kama dala kwa
shilingi tano. Wengine waliita gwala.
Tuliweza pia kuibatiza noti ya
shilingi 20 kwa kuiita ' Paundi' ikiwa na maana, thamani ya paundi moja
ya Uingereza wakati huo ilikuwa ni sawa na shilingi 20 za Tanzania. Ni
kwenye miaka ya 80.Je, rasilimali zetu ikiwamo gesi na mafuta vinaweza
kuturudisha kwenda kuwa ' Taifa Kubwa' kama tulivyokuwa wakati fulani.
Maana, nakumbuka nikiwa mdogo nilisikia redioni taarifa ya habari
ikisema kuwa ' Tanzania imetoa msaada wa magunia ( Sikumbuki idadi) ya
kunde na maharage kwa nchi ya India kutokana na mafuriko yaliyowakumba.
Nilisikia pia Tanzania ikitoa msaada wa chakula kwa nchi ya Msumbiji na
kwingineko zilizokumbwa na maafa.
Je, tunaweza kurudia kuwa ' Taifa
Kubwa' kiuchumi kama tutaendelea kuruhusu karibu kila nchi kubwa
kiuchumi kuwa na benki zao hapa kwetu? Maana siku hizi hapa kwetu kuna
benki za Wahindi mpaka Wapakistani! Je, na sisi tuna mabenki kwao?
Na tafsiri ya benki hizo si ina maana
pia kuwa nchi hizo zimeamua kujenga ' Vihenge' vyao kwetu kuhifadhia
wanavyovuna hapa kwetu na kusafirisha kwenda kula kwao.
Na tuendelee kujadili daladala na uchumi wetu...!
Picha hiyo juu niliilipiga mwaka 1988
pale Posta ya Zamani. Huo ulikuwa ni usafiri tulioutumia ennzi hizo,
maarufu kama ' Chai- Maharage'. Ni moja ya picha zangu za zamani sana
zilizo kwenye Maktaba yangu.
Maggid,
Iringa.
0754 678 252
0754 678 252
No comments:
Post a Comment