Ndugu zangu,
Asubuhi ya leo hapa Iringa nilishangaa kuona makundi ya watu yakitokea maeneo ya Kihesa kuelekea katikati ya mji.
Nilipouliza nikaambiwa wanakwenda
kwenye maombi. Ndio, Alhamisi asubuhi, watu wanafunga safari kwenda
kwenye maombi. Nimeambiwa maombi hayo ni ya siku kadhaa. Ni siku kadhaa
za watu kutokufanya kazi.
Na wengi ni watu wazima, na zaidi wanawake. Kwa kuwaangalia,
kuna wenye kwenda kuombewa kwa hofu
ya kuwa wamerogwa, au wanahofia wasije wakarogwa. Ni hofu ya
ushirikina. Na wengi wanaumwa kisaikolojia. Kuna wenye kujihisi
wamerogwa, ama , wanaishi na wachawi kama majirani. Hawa wako gizani
kwenye wengine tunachokiona ni nuru.
Inanikumbusha kisa cha Julius Nyerere
na mwandishi wa Kimagharibi. Miezi ya mwanzo kabisa ya Tanganyika huru,
mwaka 1961, Julius Nyerere alitembelewa na mwandishi wa habari kijana
wa Kimagharibi. Mwandishi yule alimwuliza Julius Nyerere, Rais kijana
kwenye nchi changa swali lifuatalo;
“ Mheshimiwa Rais, unadhani kwa sasa ni kitu gani kimetawala fikra za watu unaowaongoza kwa maana ya Watanganyika ?”
Julius Nyerere alitulia kidogo, kisha akajibu;
“ Kwa kweli kilicho mbele kabisa
kwenye fikra za watu wangu ni ushirikina. WaTanganyika wengi wanafikiri
sana juu ya mambo ya kishirikina, hasa zaidi watu wa vijijini”.
Miaka mingi ikapita, na kabla ya
Julius Nyerere hajang’atuka uongozi, mwandishi yule alirudi tena
Tanzania. Akakutana na Julius Nyerere. Akamwuliza swali lile lile la
mwaka 1961, akitaka kujua Watanzania wa sasa ni kitu gani kilicho mbele
kwenye fikra zao.
Julius Nyerere hakuchukua muda mrefu
kutoa jibu. Alisema;“ Ooh! Kwa sasa hali ni mbaya zaidi. Watanzania wa
sasa wanafikiri zaidi mambo ya ushirikina, na sasa si vijijini tu, hata
watu wa mijini nao wanatanguliza sana mambo ya ushirikina kwenye fikra
zao!”
Ndio, msafara ule niliowaona leo asubuhi wakitokea Kihesa na kwingineko ni WaTanzania wa mijini!
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment