Ndugu zangu,
Leo jijini Dar wanakutana wanahabari
na wadau wa habari zaidi ya 150. Watajadili maadili na wajibu wa
wanahabari kwenye hali ya migogoro. Watachambua pia hatari ya lugha za
chuki, udini na mengineyo. Wataangalia pia namna njema ya kukabiliana
na hali hizo.
Ni hatua njema kabisa na imekuja
wakati muafaka. Na hapa nawasifu MCT kwa kufanikiwa kuwakutanisha
wanahabari katika hili. Kila la kheri.
Na kwenye hili la wanahabari na
migogoro tunaweza kuona mfano wa moja ya habari kubwa jana Jumapili;
Iliwahusu Wabunge Mwigulu Nchemba ( CCM) na Peter Msigwa ( CHADEMA)
Hakika niliamka nikisikia vichwa vya habari vya uhasama vikitamkwa
redioni. Kisha nikajionea mwenyewe nilipoyanunua magazeti kadhaa ya jana.
Naam; “ Mwigulu na Msigwa nusura
wazichape!”. Mengi ya magazeti yalibeba habari hiyo katika staili ya
kufanana- Waheshimiwa nusura wachapane! Na picha kubwa ya waheshimiwa
hao ikawekwa mbele kwenye magazeti hayo.
Kabla hata sijaisoma habari yenyewe,
nilipoangalia picha tu, nikajiuliza; hivi walio kwenye nusura ya
kuchapana makonde ndio hawa?!
Picha tu ilijieleza, kuwa Msigwa na
Mwigulu ni watu wenye kufahamiana na pengine hukutana kunywa kahawa
pamoja. Kwamba pale, na kwa mujibu wa habari yenyewe, walikuwa kwenye
mabishano ya hoja. Ni kawaida. Maana, sikuona hata mahali wametukanana.
Masikini Msigwa na Mwigulu, hawa ni
watu wazima na familia zao. Fikiri mtoto wa mheshimiwa anaambiwa na
mwenzake shuleni; “ Eeh, nimesikia baba yako anataka kuzichapa na
mwenzake huko bungeni!” Ni mambo ya kudhalilisha kwa kweli, si kwa
familia tu. Hata kwa Mheshimiwa kwa wapiga kura wake. Naam, Waheshimiwa
wakianza kuchapana makonde hadharani badala ya kuzungumza wanaacha kuwa
waheshimiwa. Wanabaki kuwa wahuni tu, kama wale wa mitaani.
Na hapa ndipo tunauona udhaifu wetu
wanahabari, kuwa tunapenda sana kushabikia ‘vurugu mechi’. Maana,
utotoni tulipokuwa tukenda viwanjani, moja ya burudani tuliyoona ni ya
kufurahisha ni pale ilipotokea ‘ vurugu mechi!’ Kwamba hapo rafu mtindo
mmoja na kinachofuatia refa kukimbia mwenyewe au kukimbizwa kwa fito.
Naziona dalili za media yetu kuanza
hulka ya kushabikia ‘ vurugu mechi’ badala ya mambo ya msingi. Ona jana,
wabunge wale wapambanaji wa UKIMWI waliudhuria semina ya UKIMWI.
Lakini, kilichoongewa na wabunge hao kuhusu UKIMWI hatukukisikia hata
kimoja!
Hivyo, wakati wanahabari wakikusanyika
hii leo pale Dar kujadili maadili ya kazi zao na wajibu wao kwenye
migogoro waiangalie pia mifano kama ya jana kwenye media. Maana, badala
ya media kuchangia kwenye kupunguza tension na migogoro, inaweza
kuchangia kwenye kuichochea! Na hilo si jukumu la media yenye
kuwajibika na kuzingatia uzalendo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
No comments:
Post a Comment