Msuguano huo unatokea katika kipindi ambacho nchi iko katika mchakato wa kupata Katiba na rasimu yake.
Zanzibar. Chama cha Mapinduzi
(CCM) kwa upande wa Zanzibar imemshutumu Makamu wa kwanza wa Rais,
Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kumchonganisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein na viongozi wastaafu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi
Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali
Vuai alisema kauli za Seif zinaweza kusababisha mitafaruku isiyokuwa ya
lazima.
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama
cha Wananchi (CUF), alikaririwa jana Jumapili akieleza kuwa marais wa
zamani, Dk Aman Karume na Dk Salmin Amour walikuwa wanaunga mkono haja
ya Zanzibar kuwa na mamlaka ya doka kamili ndani ya Muungano.
Akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na
Kamati ya Maridhiano huko Zanzibar juzi, Maalim Seif alikwenda mbali
zaidi na kumsifia Dk Karume kuwa alikuwa Rais bora wa Zanzibar.
Hata hivyo, kitendo cha Maalim Seif kumsifia
Karume ni cha kushangaza kwani aliwahi kutomtambua baada ya kushindwa na
Rais huyo wa zamani kwenye chaguzi za urais za miaka ya 2000 na 2005.
Vuai alisema jambo hilo linakwenda kinyume na
matakwa ya Katiba ya Zanzibar na linaonyesha dharau kwa Serikali
iliyokuwa madarakani.
“CCM kinalaani kwa nguvu zote kauli za uchochezi,
kejeli, fitna na dharau zilizotolewa na Katibu Mkuu huyo wa CUF dhidi ya
Dk Shein.
“Maalim Seif ametoa kauli zinazoweza kuleta mtafaruku wa maelewano kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alionya Vuai.
Vuai pia ameipinga Kamati ya Maridhiano, ambayo
ilihusika kuandaa maandamano huko Zanzibar juzi. Alistaajabu kuwepo kwa
kamati hiyo yenye wajumbe sawa kutoka vyama vya CCM na CUF.
“Chama cha CCM hakijawahi kufanya kikao cha pamoja
kwa kukubaliana kuunda kamati kama hiyo ya maridhiano wala hakuna kikao
chochote cha CCM cha kikatiba kilichowahi kujadili na kuwateua baadhi
ya wanachama wake kuwa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano,” alisema Vuai.
Vuai alishauri wananchi wa Zanzibar kutumia fursa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kutoa ushauri kuhusu Katiba Mpya.
“Kama kuna mtu ana mawazo yake kuhusu katiba basi aheshimu mchakato wa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya,” aliongeza Vuai.
Malumbano haya ya CCM na CUF yanaashiria mpasuko wa ndoa ya vyama hivyo vinavyounda Serikali ya Umoja wa Taifa huko Zanzibar.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment