Afrika Kusini. Shujaa wa
mapambano dhidi ya utawala wa Kibaguzi, Rais mstaafu wa Afrika Kusini
Nelson Madiba Mandela bado kalazwa hospitalini kutokana na hali yake
kuwa mbaya.
Madiba alilazwa tena baada ya hali yake kuwa mbaya
kutokana na kupata tena maambukizi ya ugonjwa wa mapafu. Mandela mwenye
umri wa miaka 94, ambaye mwaka 1994 alikuwa kiongozi wa kwanza mweusi
kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa za kiuchumi barani Afrika
kutokana na uchaguzi wa kihistoria ulioshirikisha makabila yote, amewahi
kulazwa hospitali mara tatu tokea mwezi wa Desemba
Taarifa ya Serikali ilisema kwamba amekuwa akikabiliwa na maambukizi hayo kwa siku kadhaa sasa.
juzi Serikali ilisema kwamba hali yake ilizidi
kuwa mbaya saa moja na nusu asubuhi na ilibidi kupelekwa katika
Hospitali ya Pretoria ambapo hali yake bado haijakuwa nzuri lakini iko
thabiti.
Msemaji wa ofisi ya Rais Mac Maharaj alisema
madaktari waliwahakikishia kuwa madiba yuko katika hali ya utulivu na
kwamba ameanza kupumua mwenyewe.
Hata hivyo maneno yaliyotumiwa na Serikali hususan
neno la hali yake kuwa “mbaya” ni sababu ya kuwatia wasiwasi wananchi
milioni 53 wa Afrika Kusini ambao kwao Mandela anaendelea kubakia kuwa
alama kuu ya mapambano dhidi ya miongo kadhaa ya utawala wa wazungu
walio wachache nchini Afrika Kusini.
Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alijiuzulu
kuwa Rais mwaka 1999 baada ya kuwepo madarakani kwa muhula mmoja na
amejitenga na siasa kwa muongo mzima.
Mara ya mwisho alionekana hadharani wakati wa fainali za michuano ya soka Kombe la Dunia mjini Johannesburg hapo mwaka 2010.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment