MWAKA 1990, Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere, akiwa anastaafu uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), katika
ukumbi wa Diamond Jubilee alitamka yafuatayo: "Wananchi wenye shida za
kweli hutapatapa mno siku hizi kutafuta msaada,”
Akaendelea; “Na sasa tumefikia hali ya
hovyo kabisa kwamba Rais wa nchi yetu analazimika kutatua matatizo madogo
madogo katika sehemu mbalimbali za nchi, kusaidia raia mmoja mmoja. Hali hii ni
hali ya aibu kwetu wote, na inadhihirisha tu jinsi vyombo vya serikali
vinavyofanya kazi vibaya. Iko faida kubwa inayotokana na kazi anazofanya Rais wetu,
lakini ni kupoteza muda na nguvu za Rais wetu anazozihitaji kutimiza majukumu
yake maalumu ambayo ni magumu na yanadai muda wake wote."
Zaidi ya miaka 20 sasa imepita tangu
Mwalimu alipotamka hayo ya aibu na hali imezidi kuwa ngumu. Hakuna ubishi
kwamba uongozi duni umechangia wananchi “kutapatapa mno” kiasi cha kuelekea
kuchanganyikiwa. Mwalimu mwenyewe kwa bahati mbaya ana sehemu ya mchango wake
kwa kuwaacha madarakani watu wengi dhaifu kiuongozi.
Popote duniani, uongozi duni
unajidhihirisha mara nyingi kwa viongozi kupenda waonekane wanachapa kazi kwa
kushugulikia matatizo madogo. Kuna mifano mingi ya viongozi kuwa miungu-watu;
kwamba wakikutana na wananchi kazi iwe moja tu, wapigiwe magoti na si kuhojiwa
kuhusu mambo magumu.
Lakini haya matatizo yetu yaliyofikia
kwenye sura ya aibu, si tu viongozi wa nchi wakulaumiwa, bali hata wa vyama vya
upinzani na jamii kwa ujumla.
Kuna tatizo kubwa la watu kuwa na
kumbukumbu fupi. Sijui ni wangapi wanakumbuka wakati Mwalimu Nyerere
anachaguliwa kuiongoza nchi, ilijulikana wazi kiasi gani cha mshahara
alichokuwa akipokea. Na ilipotokea vurugu za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) kwenye miaka ya 1960, ambao pamoja na mambo mengine walidai
viongozi wa nchi wana mishahara mikubwa, Mwalimu alikiri na kupunguza mshahara
wake.
Ukiondoa suala la itakidi yake ya
kisoshalisti, naamini tuliweza kufahamu mshahara wa Mwalimu, si tu kutokana na
uadilifu wake, bali pia alitambua athari za wananchi kujenga fikra kwamba Rais
ana vyanzo vingi vya mapato.
Kutokana na msingi huo mzuri wa uwazi
kwenye mshahara aliotuachia Mwalimu, cha ajabu, suala la mshahara wa Rais na
mawaziri kwa muda mrefu sasa ni siri. Nimejitahidi kuwauliza waliowahi kushika
nyadhifa za juu serikalini juu ya hili, majibu yao ni ya kuchanganya.
Viongozi wengi serikalini wanajibu
mshahara, kwa mfano wa Rais si kitu, kwamba ana marupurupu mengi. Nimewauliza
pia baadhi ya viongozi wa upinzani waliowahi kugombea urais nikiamini
haiwezekani mtu kuwania nafasi yoyote bila kujua atalipwaje.
Cha ajabu, wote niliowahoji hawajui
mshahara wa Rais hadi mmoja alithubutu kuniambia; “Jinsi mimi ninavyowashangaa
viongozi wa serikali kushindwa kutaja mshahara wa Rais, basi na wao
wananishangaa kutokana na nchi yetu tunavyoijua.”
Swali nililojiuliza ni je, hawa watu wanatania?
Yaani mtu kweli unagombea nafasi ya uongozi wa nchi bila kufahamu utapokea
mshahara kiasi gani? Hata katika kazi yoyote ile, haiwezekani mtu ukaambiwa tu
usijali kuhusu mshahara, mambo mengine yote ni mazuri mno.
Mshahara una nafasi yake muhimu katika
kujenga nidhamu ya kila siku. Matokeo ya kupuuza suala hili ni sawa na
kukaribisha viongozi kula nchi kama "mchwa".
Unakuta mgombea wa urais anajua
akifanikiwa tu kukamata uongozi basi ameula.
Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo,
mgombea mmoja wa urais aliwahi kutamka maneno ambayo kwa sasa naona ni kama
almasi kutoka kwenye ulingo wa siasa.
Alitamka: "Siingi kwenye harakati
hizi kwa lengo la kujipatia utajiri. Mapato ya Rais hayawezi yakamtajirisha mtu
na wala sina ndoto za kujipatia utajiri. Nilivyo navyo vinaniridhisha."
Hii kauli inatuambia kwamba raia wa
Tanzania tunamwajiri kiongozi wa nchi na tunaelewa vema mazingira ya kazi zake.
Hatupaswi kutegemea afanye mambo ya kukurupuka nje ya mapato yake ya kila
mwezi.
Kama Rais hana uchungu na mshahara wake,
ambao unaweza kutumika kwa mfano, kwa ajili ya kulipia ada za elimu ya
wanafamilia, ndugu na jamaa, kama si kukaribisha ufujaji wa pesa, ni nini? Na
isitoshe halipi hata kodi kama raia namba moja wa nchi.
Katika Marekani, imefikia Rais halipiwi
kila kitu hovyo hovyo. Inabidi achangie sehemu ya gharama ya chakula kila mwezi
nyumbani kwake. Ndio maana kuna usemi kwao "there is no such thing as a
free lunch".
Haiwezekani kiongozi akawa tu anakula
na familia yake na wapambe kwa pesa za walipa kodi. Naamini raia wa Tanzania
wanapaswa sasa kuwa makini na maisha ya Rais wao. Nisingependa kusikia maneno
ya kipuuzi kutoka kwa raia kama 'ooh Rais hata hapokei mshahara au mshahara
kama anapokea basi umetulia tu benki.
Mara hapokei zaidi ya milioni 20 au
anapokea milioni tatu. Kama ni milioni tatu, Waziri analipwa nini?'
Vile vile, mwandishi mmoja wa habari,
kutokana na maswali yangu kwake, alisema "mshahara wa mtu yeyote unapaswa
kuwa siri", halafu tena "ukiandika mshahara wa Rais bila shaka
utamchonganisha na wananchi wake."
Jambo la pili linalopaswa kutazamwa
kutokana na kutia aibu kwa nchi inayojisifu kwa amani ni jinsi viongozi
wanavyosumbua raia na misafara yao mikubwa kana kwamba kuna hatari ya kuuawa.
Mbona wakati wa Nyerere hakukuwa na fujo kama sasa barabarani, pamoja na
majukumu mazito yaliyomkabili ndani na nje ya nchi.
Kuna hadithi kwamba kipindi cha
Nyerere, kuna gari la kawaida ambalo liligongana na gari la msafara kutokana na
kinachoonekana kutokufahamu kuna kiongozi anapita. Sasa tunashuhudia usumbufu
wa misafara mikubwa, hata kwa mke wa Rais, Spika wa Bunge na marais wastaafu.
Hivi kweli kama ni usalama, walinzi
wachache makini hawatoshi kwenye foleni za mjini? Na sasa tunakutana mara
nyingi na watu wanaoongozwa na pikipiki ambao hawajulikani kiasi cha swali
kuulizwa bungeni kwamba ni nani hasa anapaswa kuongozwa kwa msafara?
Tumeanza pia kuona polisi wa usalama
barabarani wakipoteza maisha wakiwa wanaongoza misafara ya viongozi. Hii yote
ni aibu kwa taifa.
Nadhani wakati umefika kwa Watanzania
kujifunza na kuwaeleza viongozi watarajiwa ambao hawajaonyesha kukerwa na
mbwembwe za viongozi kwamba, tuige mfano wa Botswana.
Botswana kweli ni nchi ya amani kiasi
cha mtu kuweza kushindwa kujua Rais ametembelea eneo fulani kama hospitali.
Nieleze mfano, kuna hadithi ya daktari mmoja wa Kitanzania nchini Botswana,
ambaye alikuwa anahangaika kuitambua sura ya Rais wa Botswana alipotembelea
hospitali alikokuwa anafanya kazi na kisha huyo Rais kuamua kujitambulisha.
Tujiulize hii kweli inaweza kutokea
hapa Tanzania? Nakumbuka ile hadithi ya Rais wa nchi moja ya jirani
aliyetembelea hospitali ya wagonjwa wa akili. Mapema tu, akiwa anazungumza na
mgonjwa mmojawapo, naye Rais aliulizwa kama ni yeye tu aliyesindikizwa na
magari mengi hivyo na watu waliobeba silahi nyingi. Baada ya kujibiwa ndiyo,
yule mgonjwa wa akili alitamka, basi wewe kesi yako ni nzito
sana.
La mwisho katika hili la amani,
nilipata bahati ya kufika nchi ya Argentina mwaka juzi na kufurahishwa jinsi
ambavyo inaruhusiwa kwa mtu yeyote kutembelea eneo fulani la Ikulu ya nchi
hiyo, katika mji mkuu wa Buenos Aires, bila kutozwa fedha.
Sehemu hiyo ina picha nyingi za marais
na maelezo mengi. Iko wazi hadi saa mbili usiku. Ni ruksa kupiga picha na
matokeo yake ni kivutio cha utalii. Askari wapo wanaolinda bila bughudha.
Nadhani hata Marekani kuna utaratibu fulani wa kutembelea sehemu ya Ikulu ya
Washington DC.
Jambo kama hili katika Tanzania ya
amani na utulivu ni kama ndoto. Hata kama wangetoza kiwango kidogo tu cha
fedha, mtu yoyote kuingia ndani itakuwa shughuli nzito! Tafakari je, ni kweli
hakuna picha nzuri sana za Mwalimu na wageni mbalimbali za kuwavutia wananchi
na watalii?
Tungekuwa na umakini katika ubunifu,
mapato hayo yangeweza kusaidia kutunza mandhari katika Ikulu au kusaidia kazi
nyingine. Kweli walinzi wapo kwa ajili ya kuwatisha watu tu? Tujitahidi kadri
tunavyoelekea kwenye Katiba Mpya, tuhakikishe mambo ya aibu tunayashugulikia
kikamilifu.
Source: www.raiamwema.co.tz: Andrew Bomani
No comments:
Post a Comment